Habari za Punde

Vijana watakiwa kuheshimu maamuzi ya viongozi wao

Na Takdir Ali,  Maelezo                                                     

Vijana wametakiwa kuheshimu maamuzi yanayotolewa na Viongozi ili kuweza kudumisha Amani na Utulivu hapa nchini.
Kauli hiyo imetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Vijana,Utamaduni,Sanaa na Michezo Amour Hamil Abdallah wakati alipokuwa akitoa maelezo katika mkutano mkuu wa pili wa Baraza la Vijana Zanzibar,Mkutano ambao umefanyika Hoteli ya Golden Tulip Malindi.
Amesema kuna baadhi ya vijana wamekuwa wakibeza na kutothamini maamuzi yanayotolewa na Viongozi jambo ambalo linaweza kuleta mtafaruku na kudumanza maendeleo ya Taifa.
Amefahamisha kuwa Serikali inachukuwa juhudi mbali mbali katika kuwapatia maendeleo Vijana lakini baadhi yao wamekuwa wakiyabeza maendeleo hayo na kurudisha nyuma mipango ya Serikali.
“Vijana tuacheni dharau kwa Viongozi wetu kwani hata wakifanya jambo mujuwe tayari wameshalifanyai uchunguzi wa kutosha,” Alisema katibu huyo.
Aidha amesema katika kuhakikisha Serikali inawapa kipao mbele imetenga kiasi ya Sh. Bilioni 3 kwa ajili ya ajira za vijana na kuepukana na hali tegemezi walionayo,hivyo ni vyema Vijana hao kuchangamkia fursa hiyo muhimu kwa kuanzisha miradi mbali ya kimaendeleo itakayoweza kuwaletea maendeleo.
Hata hivyo amewataka Vijana hao kujuwa mipaka yao hasa pale Viongozi wakuu wanapotoa maamuzi ili kuepuka kuvunja sheria na kuitia nchi doa.
“Hii nchi inakwenda kwa mujibu wa Katiba na Sheria hivyo kitendo cha baadhi ya vijana kuwadhihaki viongozi wao ni kuenda kinyume na Taratibu,Sheria na katiba ya nchi”,Alisisisitiza Naibu huyo.
Akifungua Mkutano huo Naibu Waziri wa Wizara ya Vijana,Utamaduni,Sanaa na Michezo Lulu Msham Abdallah amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imefanya juhudi kubwa ya kuanzisha na kuliendeleza Baraza la Vijana ili kukuza ushirikishwaji wa Vijana katika mbambo mbali yanayowahusu.
Mbali na hayo amesema Vijana wanapaswa kushiriki kikamilifu katika kuleta maendeleo ya nchi na wasijaribu kulitumia Baraza hilo tofauti na malengo yalikusudiwa na Serikali bali walitumie kwa ajili ya kujiletea maendeleo.
Wakichangia mada Washiriki wa Mkutano huo wamewapongeza Viongozi wa Serikali kwa juhudi wanazochukuwa za kuwasaidia Vijana ikiwa ni pamoja na kuanzishwa Baraza la Vijana ambalo ni chombo muhimu kinachowawezesha kuelezea mikakati mbali mbali waliojipangia.
Imetolewa na Idara ya Habari Maelezo Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.