Habari za Punde

Makabidhiano ya Komputa Kwa Ajili ya Kuazisha Mfumo wa Utoaji wa Dawa Kwa Njia ya Kieletroniki Katika Hospitali ya Kivunge Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Mfamasia  Mkuu Zanzibar Habib Ali Sharif akimkabidhi Compyuta Daktari dhamana wa Hospitali ya Kivunge  Tamim Hamad Said kwa ajili ya kuanzisha Mfumo wa Kieletroniki wa dawa  katika ghafla iliyofanyika Hospitali hiyo iliyoko  Mkoa wa Kaskazini Unguja
Mkurugenzi wa Bohari Kuu ya Dawa Zanzibar  Zahrani Ali Hamad akizungumza na wafanyakazi wa Hospitali ya Kivunge namna ya kuanzisha Mfumo wa Kieletroniki wa dawa  katika ghafla iliyofanyika Hospitali ya Kivunge Mkoa wa Kaskazini Unguja
Mfamasia  Mkuu Zanzibar Habib Ali Sharif akieleza namna  mfumo  wa kielektroniki  utakavyosaidia upatikaniji wa dawa kwa haraka wakati dawa zinapopungua kwenye vituo vya Afya
Daktari Dhamana  Hosipitali ya Kivunge  Tamim Hamad Said akitoa shukurani baada ya kupokea compyuta za kuanzisha Mfumo wa Kieletroniki wa dawa  katika ghafla iliyofanyika Hospitali ya Kivunge Mkoa wa Kaskazini Unguja
 (Picha na Abdalla Omar Maelezo  -  Zanzibar).
Na  Khadija  Khamis   - Maelezo  Zanzibar.
Hospitali ya Kivunge Mkoa wa Kaskazini Unguja inatarajiwa kuanza kutumia mfumo mpya wa utoaji wa Dawa kwa njia ya Kielektroniki ili kuboresha utoaji wa huduma Hospitalini hapo.
Hatua hiyo inakuja kufuatia Wizara ya Afya Zanzibar kukabidhi vifaa mbali mbali ikiwemo Komputa zitakazorahisisha mfumo huo.
Akikabidhi vifaa hivyo huko Kivunge Mfamasia Mkuu wa Zanzibar, Habib Ali Sharif amesema mfumo huo Kielectroniki utasaidia kudhibiti Dawa na kujua upungufu uliopo katika Hospitali hiyo.
Aidha amefahamisha kuwa Mfumo huo pia utarahisisha kutathimini jinsi ya dawa zinavyotumika katika Vituo mbali mbali.
Mfamasia huyo alibainisha kuwa zoezi la Mfumo wa Kielektroniki mbali na kutumika katika Hospitali ya Kivunge linatarajiwa pia kufanyika katika hospitali ya kendwa.
Alieleza vifaa vitakavyofungwa katika Hospitali hiyo kurahisishia mfumo huo kuwa ni Komputa, UPS, Network Switch na Rauters Internet.
Hata hivyo aliwasisitiza Watendaji wa Hospitali ya Kivunge kuzidisha mashirikiano ya pamoja katika utendaji wa kazi zao ili kuwapatia Wananchi huduma zinazofaa.
Mfamasia Habib alisema kuwa Wakufunzi kutoka Zambia watatoa mafunzo kwa wafanyakazi mbali mbali wa Wizara ya afya ili kutumia mfumo huwo wa kisasa ambao unarahisisha ufanisi wa kazi.
“Lengo ifikapo mwaka 2020 sisi ndio tunaotoa mafunzo kwa wengine na tunaiomba serikali izidi kutuunga mkono katika jambo hili”alisema Mfamasia Mkuu wa Zanzibar.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Bohari Kuu ya Dawa Zanzibar Zaharan Ali Hamad alisema Serikali itaendelea na azma ya kuwapatia Wananchi wake matibabu ya maradhi mbalimbali.
Naye Daktari dhamana wa hospitali hiyo Tamim Hamad Said alishukuru kupata  vifaa hivyo ambavyo vitasaidia kutunza program na kurikodi data.
“Kupitia mfumo huu wa kisasa tutajua mahitaji ya dawa tunayotaka kulingana na wagonjwa ambao tunawapokea. Pia tutajua upunguvu wa dawa pamoja na dawa  tunazohitaji ili lengo la hospitali kutoa dawa kwa Wananchi wote liweze kupatikana .”alisema Daktari huyo.
Komputa na vifaa vingine vya kurahisisha mfumo wa utoaji Dawa kwa njia ya Kielektroniki ni msaada uliotolewa na Mfuko wa Kimataifa wa kupambana na Ukimwi, Kufua Kikuu na Malaria Global Fund wenye thamani ya Shilingi za Kitanzania Milioni 287.
IMETOLEWA NA MAELEZO ZANZIBAR

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.