Habari za Punde

Jambo la Kutia Moyo Kuwaona Wakulima Wengi Nchini Wanatumia Teknolojia za Kisasa Kilimo.


Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Balozi Seif akizungumza na Wananchi wa Mikoa Miwili ya Pemba wakati akiyafunga Maonyesho ya Siku ya Kilimo Duniani hapo Chamanangwe na kutoa siku mbili za ziada kuendelea na zoezi hili ili kuwapa fursa wananchi kuendelea kupata taaluma.

Na. Othman Khamis OMPR.                                         
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema ni jambo la kutia moyo kuwaona Wakulima wengi Nchini wanatumia Teknolojia ya Kisasa katika uzalishaji wa mazao yao kwa vile tayari wameshafikia hatua ya kufuata miongozo tofauti inayotolewa na Wataalamu wa Sekta ya Kilimo.
Alisema mabadiliko hayo yanatokea kutokana na juhudi kubwa zinazoendelea kuchukuwa na Wataalamu wa Sekta ya Kilimo Nchini katika kuleta Mapinduzi makubwa ya Kilimo.
Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo wakati akiyafunga Maonyesho ya Kilimo katika kuadhimisha Siku ya Chakula Duniani yaliyofanyika katika Kijiji cha Chamanangwe Wilaya ya Wete Kisiwani Pemba ambapo Makundi ya Wananchi kutoka maeneo mbali mbali ya Pemba walipata fursa ya kuyatembelea na kujifunza mbinu tofauti za Kilimo.
Alisema kwa hatua hiyo wakati umefika sasa hasa kwa Vijana kuelewa kwamba Kilimo ni Biashara kubwa Duniani kama zilivyo Biashara nyengine  ambacho kinaweza kumbadilisha Kimaisha Kijana atakayeamuwa kuelekeza nguvu na maarifa yake katika Sekta hiyo.
Balozi Seif alisema Vijana wengi wakiwa na mtazamo huo wanaweza kubadilika kitabia na kuondokana na utegemezi wa Familia kwenda katika mfumo wa kujitegemea wenyewe Kimaisha na kuondokana na umaskini wa Chakula na kipato.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliuagiza Uongozi wa Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi kuchukuwa jitihada za makusudi kupandikiza mawazo hayo ya kupenda Kilimo miongoni mwa Vijana badala  ya kundi hilo kubwa kusubiri Serikali kuwapatia ajira za Ofisini ambazo hata zilizopo ni chache mno.
Alisema Serikali inafahamu wazi kwamba Wakulima, Wafugaji, Wavuvi na hata Wazalishaji wengi Nchini bado wanakabiliwa na kipato kidogo kinachohitaji kupewa msukumo ili kuhakikisha wanapata nyenzo katika kukuza uzalishaji wa Chakula Nchini.
Hata hivyo Balozi Seif  aliwatanabahisha Washirika hao wa Sekta ya kilimo licha na uhaba wa kipato lakini bado wana wajibu wa kuendelea kushirikiana na Serikali ushirikiano utakaoibua upatikanaji wa mbinu zitakazotatua changamoto ya upatikanaji wa masoko na kutoharibika kwa mazao yao baada ya mavuno.
Aliziomba Taasisi za Kifedha Nchini na hata zile za Kimataifa kuendelea kutoa Mikopo nafuu kwa Wakulima pamoja na Wazalishaji wadogo wadogo kwa lengo la kuongeza uzalishaji wa Chakula Nchini sambamba na kulijengea Uchumi wa Viwanda Taifa.
Balozi Seif alisema Sekta ya Kilimo ni ya kila Mwajamii akiwa na wajibu wa kutoa misaada na nguvu zake ili kufanikisha Sekta hiyo ambayo kuzorota kwake ni sawa na kuzorota kwa usalama wa Wananchi wote.
Aliwanasihi Wafanyabiashara Kisiwani Pemba kununuwa bidhaa zinazozalishwa na Wakulima Visiwani ili kuwatia moyo kwa vile tayari wameshahamasishwa kujitegemea kupitia mfumo wa kazi za Ujasiriamali.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alizishukuru Taasisi zote zilizokubali kushirikiana na Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi katika matayarisho ya maonyesho hayo yaliyosaidia kuwakutanisha Wakulima na Wadau wa Sekta hiyo muhimu.
Alisema ushirikiano huo umeonyesha jinsi gani Taasisi hizo zilivyojitokeza kuunga mkono jitihada za Serikali katika kuleta Mapinduzi ya Kilimo kama zilivyoainishwa katika ujumbe wa Mwaka huu unaoeleza “ juhudi zetu ndio khatma yetu, Dunia bila ya njaa inawezekana ifikapo mwaka 2030”.
Balozi Seif alifahamisha kwamba mshikamano huo ulioonyeshwa  kati ya Taasisi , Wananchi na Serikali hauna budi kuendelezwa kwa faida ya Maendeleo ya kudumu ya Sekta za Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi hapo baadae.
Akisoma Risala ya Maonyesho hayo Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Maliasili Mifugo na Uvuvi Nd. Ahmad Kassim Haji alisema Eneo la Kilimo la Chamanangwe lililotengwa kwa shughuli za Maonyesho lina ukubwa wa Eka 85 ambapo Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi imetenga Eka 17 kwa shughuli hizo za Maonyesho.
Nd. Ahmad alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ilitoa agizo Maalum la kuitaka Wizara ya Kilimo Zanzibar iandae Maonyesho ya Siku ya Chakula Duniani Chamanangwe na kuwa ya kudumu ili kutoa fursa kwa Wakulima, Wafanyabiashara na Wajasiri amali kujifunza mbinu za uzalishaji sambamba na kutangaza bidhaa zao wanazozalisha.
Alisema zaidi ya washiriki 500 wanaweza  kutoa huduma katika eneo hilo la Chamanangwe ambalo matayarisho yake yamefikia gharama ya shilingi za Kitanzania Milioni 140,000,000/-.
Naibu Waziri wa Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi alizishukuru Taasisi na Mashirika ya Kimataifa yaliyojitokeza kushirikiana na Serikali kupitia Wizara hiyo kuunga mkono Maonyesho hayo katika Taaluma na kupelekea mafanikio makubwa ya kupigiwa mfano.
Akimkaribisha Mgeni rasmi kuyafunga Maonyesho hayo Naibu Waziri wa Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi Dr. Makame Shauri  Ussi alisema Meonyesho ni falsafa iliyobeba mambo mengi ikiwemo mafunzo,  Biashara, na haiba inayowapa Wananchi kujumuika pamoja.
Dr. Makame alisema ni jambo la faraja kuona kwamba Wakulima wengi wa Mjini na Vijijini Pemba na Unguja walitumia fursa ya Maonyesho hayo kujifunza mbinu mbalki mbali za Kilimo cha Kisasa.
“ Nimefarajika Kuona Makundi hya Wananchi na Wakulima wa Mikoa Miwili ya Pemba jinsi walivyojitokeza kutembelea Maonyesho hayo yaliyofanyia kwa mara ya kwanza kisiwani Pemba.
Aliwataka Wananchi kuendelea kujifunza Kilimo cha kisasa kwa lengo la kukabiliana na mabadiliko ya Tabia Nchi yanayoikumba Dunia hivi sasa na kuonyesha ishara ya maharibiko ya Mazingira.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alikabidhi Vyeti kwa Washiriki wa Maonyesho hayo pamoja na kutoa zawadi kwa washindi wa shindano la Maonesho hayo ya Siku ya Kilimo Duniani inayofikia Kilelechake ifikapo Tarehe 16 Oktoba hya kila Mwaka.
Katika kuunga mkono jitihada za Wakulima, Wafanyabiashara na Wajasiriamali Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwa kujadiliana na Viongozi wenzake, akatoa uamuzi wa kuongeza siku mbili kuendelea kwa Maonyesho hayo ya Siku ya Chakula Duniani hapo Chamanangwe Wilaya ya Wete.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.