Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Balozi Seif Ahutubia Maadhimisho ya Siku ya Maafa Duniani Kisiwani Pemba Katika Ukumbi wa Makonyo Wawi Chakechake Pemba.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Balozi Seid Ali Iddi akihutubia wakati wa Maadhimishi ya Siku Maafa Duniani yalioadhimishwa Kitaifa Kisiwani Pemba katika Ukumbi wa Kiwanda cha Makonyo Wawi Chakechake.




Na. Othman Khamis OMPR.                                                                                                                                       




Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema ujenzi wa Misingi ya kupitishia Maji ya Mvua  pamoja na kuimarisha Miundombinu ya Bara bara Nchini ni muendelezo wa Mipango mbali mbali inayochukuliwa na Serikali katika juhudi zake za kujiandaa na kujikinga katika kukabiliana na Maafa.
Hata hivyo alisema Serikali Kuu pekee haiwezi kufanikiwa na jitihada hizo inazozichukuwa za kupambana na Maafa bila ya ushiriki kikamilifu wa Wananchi wote Unguja na Pemba.
Balozi Seif Ali Iddi alitoa kauli hiyo wakati wa Kilele cha maadhimisho ya Siku ya Maafa Duniani zilizofanyika Kitaifa katika Ukumbi wa Kiwanda cha Makonyo kiliopo Wawi Mjini Chake Chake Pemba.
Alisema mafanikio ya Taifa kupunguza hasara za Kiuchumi zinazotokana na Majanga ya Maafa yanatokana na utii wa Sheria pamoja na miongozo inayotolewa kila mara na Viongozi pamoja na Wataalamu wa Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa.
Balozi Seif alisema pale  Serikali inapotoa miongozo na utaratibu wa kuwataka Wananchi kuacha kujenga sehemu za mabondeni au kutokata Miti ovyo haikusudii kuwakomoa Raia zake bali imelenga kuchukuwa hadhari kabla ya kusubiri athari inayoishia kupatikana kwa makovu yanayotokana na Majanga.
Alieleza ni vyema Wananchi wakaelewa kuwa Taifa linapoamua kupunguza hasara za Kiuchumi zinazosababishwa na Maafa ni kuijengea uwezo Serikali kuelekeza Fedha zake katika Miradi Mipya ya Maendeleo badala ya kushughulikia matengenezo ya miradi ya zamani iliyoathirika na Maafa ambayo yanaweza kudhibitiwa.
Alisema Wananchi wote ni mashahidi wakati Taifa lilipokumbwa na Maafa Mwaka uliopita ambayo yalisababisha hasara kubwa za Kiuchumi zilizokatisha kwa muda huduma mbali mbali za Kijamii ikiwemo Usafiri, kukatika kwa Bara bara, kujaa Maji kulikosababisha ugumu wa usafiri.
Balozi Seif alifahamisha kwa mujibu wa Ripoti zilizotolewa Mwaka 2017 ikiwemo ile ya Kitaalamu ya kubaini sababu zilizopelekea Zanzibar kuathirika na Mvua za Masika kila mwaka pato la Taifa lipatalo Bilioni 11.67 sawa na asilimia 0.38% zilikadiriwa kupotea kutokana na Maafa.
Alisema kiasi cha shilingi Bilioni 4,800,000,000/- zilihitajika kwa ajili ya matengenezo ya Miundombinu ya Bara bara na Mawasiliano kiwango ambacho ni sawa na asilimia 3.42% ya thamani ya pato la Taifa.
Aidha alisema jumla ya ekari 2,822.5 za mazao mbali mbali ya kilimo yenye thamani ya shilingi Bilioni 5,444,750,000/- ziliathirika ikiwa ni sawa na upotevu wa karibu asilimia 1% ya thamani ya Pato la Taifa linalotokana na Mazao.
Balozi Seif alisema hasara kama hizo pia ziliripotiwa kijitokeza katika Sekta za Mifugo ambapo Ng’ombe wapatao 157 wenye thamani ya shilingi 28,350,000/- waliripotiwa kufa kwa kukumbwa na maradhi mbali mbali, wakiwemo pia kuku wapatao 6,181 wenye thamani ya shilingi Milioni 92,715,000/- walifariki.
Hata hivyo Balozi Seif alifafanua kwamba jumla ya ekari 875 za Misitu zenye thamani ya shilingi Milioni 17,826,500/- sawa na asilimia 0.02% ya thamani ya pato la Taifa litokanalo na misitu iliungua Moto.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwaeleza Wananchi kupitia Maadhimisho hayo ya Siku na Maafa Duniani kwamba jumla ya Nyumba za Makaazi zipatazo 6,005 ziliathirika.ambapo jumla  ya shilingi za Kitanzania Milioni 145,009,328/- zilikadiriwa kutumika.
Alikumbusha kwamba Umoja wa Mataifa umetangaza Rasmi Siku ya Maafa Duniani ukizitaka Nchi Wanachama kuweka utaratibu wa kila Mwaka kushajiisha Makundi ya Kijamii, Taasisi za Kiraia pamoja na za Kiuchumi juu ya majukumu na wajibu wao katika kujiandaa na kujikinga katika kukabiliana na Maafa.
Alisema Siku hii kama ilivyoasisiwa Kimataifa ina lengo la kuhamasisha Jamii juu ya matumizi sahihi ya rasilmali za Bahari na Nchi Kavu pamoja na kuifuata mifumo ya njia za Kiusalama katika kukabiliana na maafa hasa kwa zile Jamii zilizo katika hatari kubwa ya kuathirika na Maafa.
Akitoa Taarifa ya Siku naMaadhimisho ya Siku ya Maafa Duniani Mkurugenzi Mtendaji wa Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar Nd. Makame Khatib alisema Sekriterieti na Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa itaendelea kutoa Elimu kwa Umma kwa kuwashirkisha  Wananchi Vikundi tofauti pamoja na Wanafunzi ikiambatana na utolewajin wa Vipeperushi.
Alisema hatua hiyo imelenga kuiandaa Jamii kuwa na Utamaduni wa kuchukuwa athari za kujikinga naMaafa kabla haijaikumba Jamii husika ili kuungana na Azimio la Umoja wa Mataifa la kuiteuwa siku ya Tarehe 13 Oktoba ya Kila Mwaka kuwa ni siku ya Maadhimisho ya Kukabiliana na Maafa Duniani Kote.
Alisema Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar kwa kuitumia Sekriterieti ya Kamisheni hiyo  iliyojumuisha Watendaji na Wataalamu kutoka Taasisi mbali mbali za Umma na zile Binafsi imeanzisha utaratibu wa kufanya ukaguzi katika Majengo ya Taasisi tofauti Nchini ili kujiridhisha na mfumo wa Majengo hayo yanayoweza kuhimili athari zinazotokana na Maafa.
Alisema Ukaguzi huo tayari umeshafanywa kwa baadhi ya Hoteli kama  Ocean Paradise, Karafuu Hoteli, Pemba Misali, Boti iendayo kwa Kasi ya Azam IV, Sea Link, pamoja na baadhi ya Vituo vya uuzaji wa Mafuta.
Alifahamisha kwamba kwa vile Maafa wakati wote yanaigusa Jamii moja kwa moja Wananchi wanapaswa kujiepusha na tabia ya kuchafua mazingira kwa kuchoma taka ovyo, kukata misitu au matumizi mabaya ya Bahari.
Alitahadharisha kuwepukwa kwa changamoto zilizomo ndani ya uwezo wa wanaadamu wenyewe akitolea mfano wa ujenzi wa majengo yasiyozingatia tathmini za kukabiliana na Maafa, Mipango Miji sambamba na usafi wa Mazingira.
Akitoa Takwimu za baadhi ya majanga ya Maafa yaliyotokea Nchini katika Matukio mbali mbali Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Nd.Abdullah Hassan Mitawi alisema Zanzibar imekuwa ikikumbwa na Maafa kutokana na Mvua, upepo, ajali za Bara barani, moto pamoja na mbadiliko ya Tabia Nchi.
Nd. Mitawi alisema majanga hayo ndio yaliyopelekea Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuanzisha Kamisheni ya Kukabiliana na maafa ndani ya Sheria nambari 5 ya Mwaka 2015.
Alisema yapo mafanikio makubwa yaliyopatikana Zanzibar kutokana na jitihada mbali mbali zinazochukuliwa na Serikali kupitia ushiriki wa Taasisi, Jumuiya na hata Washirika wa Maendeleo.
Alisema janga la maradhi ya kipindu pindu lililoikumba Zanzibar mnamo Mwaka 1977 hadi mwaka 2016 na kugharimu upotevu wa Wananchi wapatao elfu 14,000 limeweza kudhibitiwa ambapo Mwaka uliopita wa 2017 hakukutokea kesi ya ugonjwa huo kutokana na juhudi hizo.
Nd. Mitawi alifahamisha kwamba kasi ya Serikali ya kuimarisha miundombinu ya kukabiliana na Maafa Nchini imekwenda mbali zaidi kutokana na uimarishwaji wa Vituo vya kukabiliana na Maafa katika Maeneo ya Mtoni na Nungwi kwa Kisiwa cha Unguja na Mkoani kwa Kisiwa cha Pemba.
Alieleza kwamba Vituo hivyo tayari vimeshawezeshwa kwa kuwa na vifaa vya kisasa vya uokozi ikiwemo Boti iendayo kwa kasi yenye uwezo wa kuokoa Watu 500 kwa wakati Mmoja na ndege zisizo na rubani zenye uwezo wa kutoa taarifa ili kujua mienendo ya athari zinazojitokeza wakati wa Maafa.
Akimkaribisha Mgeni kwenye kilele cha Maadhimisho hayo Naibu Waziri, Wizara ya Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Mihayo Juma Nh’unga alisema Jamii ina uwezo wa kushiriki kikamilifu katika kukabiliana na Maafa licha ya uwepo wa changamoto zinazosababishwa  na athari za kimaumbile.
Hata hivyo Mh. Mihayo alisema changamoto sugu za mafuriko katika baadhi ya maeneo Nchini hasa eneo la Kibonde mzungu zimeanza kutafutiwa muarubaini kwa kujengwa miundombinu itakayosaidia kuondosha tatizo hilo.
Aliwapongeza Wananchi wa Kijiji cha Bubujiko  Mkoa wa Kaskazini Pemba kwa kushirikiana na Halmashauri pamoja na Viongozi wa Jimbo kwa kufanikisha Ujenzi wa Mtaro uliowakomboa Wananchi wa Maeneo hayo waliokuwa wakiathiriwa na mvua za Masika.
Katika kwenda sambamba na azma ya Serikali ya kukabiliana na Maafa Naibu Waziri Mihayo aliziomba Taasisi za Umma wakiwemo Wakuu wa Wilaya kufanya juhudi za kupata Sheria zinazoelekeza miongozo na kanuni za kukabiliana na Maafa Nchini.
Ujumbe wa Mwaka huu wa kuadhimisha Siku ya Maafa Duniani unasema:- “Punguza hasara za Kiuchumi kutokana na Maafa ili kubadili Maisha”.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.