Habari za Punde

Rais akutana na ujumbe wa Maspika wa Mabunge ya Nchi za Jumuiya ya Madola Barani Afrika

 Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed SheiN akisalimiana na Naibu Spika wa Bunge la Rwanda Mhe.Edda Mukabagwiza akiwa miongoni mwa ujumbe wa Maspika wa Mabunge ya Nchi  za Jumuiya ya Madola Barani Afrika walipofika Ikulu Mjini Zanziobar jana,[Picha na Ikulu.] 04/10/2018. 


 Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein (kulia) akizungumza na Ujumbe wa  Maspika wa Mabunge ya Nchi  za Jumuiya ya Madola Barani Afrika unaoongozwa na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pia Mwenyekiti wa Maspika kutoka Nchi za Wanachama wa Jumuiya ya Madola Mhe.Job Ndugai (wa pili kulia),walipofika Ikulu Mjini Zanziobar jana,[Picha na Ikulu.] 04/10/2018. 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed SheiN akibadilishana mawazo na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pia Mwenyekiti wa Maspika kutoka Nchi za Wanachama wa Jumuiya ya Madola Mhe.Job Ndugai wakati alipoongoza ujumbe wa Maspika wa Mabunge ya Nchi  za Jumuiya ya Madola Barani Afrika walipofika Ikulu Mjini Zanziobar jana,[Picha na Ikulu.] 04/10/2018

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein (kushoto) akiagana na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pia Mwenyekiti wa Maspika kutoka Nchi za Wanachama wa Jumuiya ya Madola Mhe.Job Ndugai baada ya mazungumzo na Ujumbe wa  Maspika wa Mabunge ya Nchi  za Jumuiya ya Madola Barani Afrika,ulipofika Ikulu Mjini Zanziobar ljana,[Picha na Ikulu.] 04/10/2018.


STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar                                    04.10.2018
---
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein ameipongeza Jumuiya ya Madola kwa kuendelea kuiunga mkono Zanzibar na kuwapongeza Maspika wa Mabunge ya Jumuiya hiyo wa nchi za Afrika kwa kuja kufanya vikao vyao hapa Zanzibar.

Dk. Shein aliyasema hayo leo Ikulu mjini Zanzibar wakati alipokutana na viongozi wa Umoja wa Mabunge ya Jumuiya ya Madola wa nchi za Afrika wakiongozwa na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye ndiye Mwenyekiti wa Maspika hao hivi sasa Job Yustino Ndugai aliyefuatana na mwenyeji wake Spika wa Baraza la Wawakilishi Zubeir Ali Maulid.

Katika maelezo yake Rais Dk. Shein alieleza kuwa Jumuiya ya Madola inathamini na kutambua juhudi kubwa inazozichukua Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwemo Zanzibar katika  kuiendeleza na kuiimarisha Jumuiya hiyo yenye historia kubwa.

Aidha, Rais Dk. Shein alipongeza juhudi za Jumuiya ya Madola za kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuendeleza na kuimarisha sekta mbali mbali za maendeleo.

Alieleza kuwa ujio wa viongozi wa Jumuiya hiyo mara kwa mara hapa Zanzibar inaonesha wazi jinsi Jumuiya hiyo inavyovutiwa na juhudi za Zanzibar katika kujiletea maendeleo endelevu.

Aliongeza kuwa mnamo mwezi Agosti mwaka jana Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola Bi Baroness Patricia Scotland alitembelea Zanzibar na kufanya nae mazungumzo ambapo Katibu huyo aliahidi kuwa Jumuiya hiyo itaendelea kuiunga mkono Zanzibar kwa kutambua juhudi inazozichukua katika kujiletea maendeleo.

Rais Dk. Shein alitumia fursa hiyo kutoa pongezi zake za pekee kwa Maspika wa Mabunge ya Nchi za Jumuiya ya Madola Barani Afrika kuja Zanzibar kwa ajili ya kufanya mkutano wao wa maandalizi ya Mkutano Mkuu.

Hivyo, Rais Dk. Shein aliwapongeza Maspika hao wote chini ya Mwenyekiti wao Spika Job Yustino Ndugai ambaye alimpongeza kwa kuchaguliwa kwake kushika wadhifa huo kwa kipindi cha muda wa miaka miwili.

Rais Dk. Shein alieleza kuwa kutokana na anavyomfahamu Spika huyo wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jinsi alivyomchapa kazi na mwenye ari, juhudi na maarifa katika utendaji wake wa kazi anaimani kubwa Jumuiya hiyo itazidi kupata maendeleo.

Spika Ndugai ambaye alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Maspika na viongozi wa Bunge katika Umoja wa Mabunge ya Jumuiya ya Madola Barani Afrika manmo Julai 27 mwaka jana 2017, katika mkutano uliofanyika mjini Abuja nchini Nigeria.

Dk. Shein alisema kuwa kufanyika kwa mkutano huo hapa Zanzibar ni fursa moja wapo ya kuendelea kuitangaza Zanzibar kiutalii ambapo Rais Dk. Shein aliwakaribisha viongozi hao wote wakiwemo Maspika wa Jumuiya hiyo kuja kutembea Zanzibar wakati wowote.

Aliongeza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inatoa pongezi zake na kuunga mkono hatua hiyo ya Maspika hao kuja kufanya vikao vyao muhimu hapa Zanzibar na kueleza kuwa nchi zote za Bara la Afrika zina uhusiano na ushirikiano mzuri kwani watu wake wote ni wamoja kama historia inavyoeleza.

Nae Spika wa Bunge la Tanzania Job Yustino Ndugai alimueleza Rais Dk. Shein kuwa viongozi hao wapo Zanzibar kwa muda wa siku mbili wakifanya vikao vyao kwa ajili ya kuandaa ajenda za mkutano mkuu wa Jumuiya hiyo kwa Maspika wa Mabunge ya Nchi za Jumuiya ya Madola Barani Afrika utakaofanyika Oktoba 2019 mjini Arusha, Tanzania.

Spika Ndugai alitoa pongezi kwa mapokezi na matayarisho mazuri waliyoyapata chini ya mwenyeji wao Spika wa Baraza la Wawaklishi Zanzibar na kueleza kuwa vikao vyao vinafanyika katika ukumbi wa Ofisi ndogo za Bunge zilizopo Tunguu, Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja

Spika Ndugai alitumia fursa hiyo kupongeza hatua za maendeleo zilizofikiwa Zanzibar huku akieleza jinsi mafanikio makubwa yatakayopatikana katika suala zima la ulinzi na usalama hapa Zanzibar baada ya kuzinduliwa mradi wa ulinzi wa mji salama na Rais Dk. Shein hapo jana.

Alieleza kuwa kwa vile Zanzibar ni visiwa ambavyo vimekuwa vikiitegemea sana sekta ya utalii mradi huo utasaidia kwa kiasi kikubwa kuimarisha sekta hiyo kwani uwepo wa usalama ndio kivutio kimoja wapo cha watalii.

Nae Naibu Spika wa Bunge la Rwanda Edda Mukabagwiza alitoa salamu za Rais Paul Kagame kwa Rais Dk. Shein na kupongeza hatua kubwa za maendeleo zilizofikiwa Zanzibar huku akitumia fursa hiyo kusifu mazingira ya Zanzibar ambayo yanavutia kiutalii.

Katika maelezo yake Naibu Spika huyo alisisitiza kuwa Rwanda itaendeleza uhusiano na ushirikiano wake wa kihistoria uliopo kati yake na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwemo Zanzibar.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.