Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein (kulia) akizungumza na Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Nchini Uganda Mhe.Dk.Aziz Ponary Mlima alipofika Ikulu Mjini Zanzibar leo kumuaga Rais,Balozi aliteuliwa hivi karibuni na Rais wa Jamhri ya Muungano wa Tanzania Dkt.John Pombe Magufuli,[Picha na Ikulu.] 12 Oct 2018.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.
Ali Mohamed Shein amesisitiza haja ya kuimarisha ushirikiano na uhusiano wa
kihistoria kati ya Uganda na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kama
zilivyoshirikiana katika kupigania uhuru.
Dk. Shein aliyasema
hayo leo Ikulu mjini Zanzibar, wakati alipofanya mazungumzo na Balozi wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Uganda Dk. Aziz Ponary Mlima, aliefika
Ikulu kwa ajili ya kumuaga Rais.
Katika maelezo yake Rais
Dk. Shein alisema kuwa Uganda na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwemo
Zanzibar zina uhusiano wa kihistoria tokea wakati wa kupigania uhuru wa nchi
hizo, hivyo ni vyema uhusiano na ushirikiano huo ukaendelezwa kwa maslahi ya
pande zote mbili.
Alieleza kuwa mbali ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwemo pia Zanzibar wakati huo wa kupigania
uhuru mashirikiano na uhusiano mwema ulikuwepo kwa nchi hizo pamoja na nchi jirani
ikiwemo Kenya ambapo hatimae nchi zote hizo zilipata uhuru.
Alieleza kuwa licha ya
kuwepo kwa mazingira tofauti ya kupata uhuru ambapo zipo nchi katika ukanda wa
Afrika Mashariki zipipata uhuru kwa njia ya demokrasia lakini pia kwa upande wa
Zanzibar ilipata uhuru wake kwa njia ya Mapinduzi.
Hivyo, Rais Dk. Shein
alisisitiza kuwa juhudi, maarifa, ari na upendo uliooneshwa wakati huo chini ya
waasisi wa nchi hizo akiwemo Hayati Mwalimu Julisus Kambarage Nyerere na wenziwe
ni vyema ukaendelezwa kwa manufaa ya wananchi wa pande hizo.
Aidha, Rais Dk. Shein alieleza
kuwa historia inaonesha kwamba sekta ya elimu ndio kiunganishi kikubwa
kilichowaunganisha watu wa Uganda na Zanzibar ambapo wananchi wa Uganda waliowemgi
walifuata elimu ya dini ya Kiislamu hapa Zanzbar.
Aliongeza kuwa kwa
upande wa wananchi wa Zanzibar wengi wao waliosoma vyuo vikuu vya nje wakati
huo walisoma nchini Uganda katika Chuo Kikuu cha Makerere ambapo historia
inajirejea ambapo hivi sasa hapa Zanzibar wapo wanafunzi wanaosoma katika vyuo
vikuu vya Zanzibar wanaotoka nchini Uganda.
Pamoja na hayo, Rais
Dk. Shein alitumia fursa hiyo kueleza juhudi za Rais Yoweri Kaguta Museven wa
Uganda anazozichukua katika kuendeleza uhusiano na ushirikiano mwema uliopo
kati ya Uganda na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Dk. Shein alimueleza
Balozi huyo kuwa anafahamu kwamba Serikali zote mbili zimedhamiria kutekeleza Diplomasia
ya uchumi katika kuhamasisha uwekezaji hasa katika sekta ya viwanda kwani ndio
kiu ya uchumi wa Tanzania hivi sasa hivyo, ni matumaini yake hilo atalifanyia
kazi.
Rais Dk. Shein
alimtakia kazi njema Balozi huyo na kumueleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar itaendelea kumpa mashirikiano makubwa.
Nae Balozi wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania nchini Uganda, Dk. Aziz Ponary Mlima alimuhakikishia
Rais Dk. Shein kuwa atahakikisha uhusiano na ushirikiano wakihistoria uliopo
kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiemo Zanzibar na Uganda unaendelezwa.
Alieleza kuwa juhudi
za makusudi atazichukua katika kuhakikisha mahusiano mema kati ya Tanzania na pande
mbili hizo yanaimarika huku akieleza kuwa sekta ya utalii pamoja na masuala ya
kuwavutia wawekezaji kuja kuekeza Tanzania ikiwemo Zanzibar yote kwa pamoja
yatapewa vipaumbele.
Pamoja na hayo, Balozi
Mlima alimueleza Rais Dk. Shein haja ya Watanzania kukitumia ipasavyo kituo
kipya cha Uongozi kiliopo nchini Uganda kilichoitwa “Julius Nyerere Leadership
Centre” ili wananchi pamoja na vijana waweze kujifunza historia na mambo mengi
hasa yanayomuelezea Hayati Julius Nyerere katika uongozi wake.
Kituo hicho kilichozinduliwa
hivi karibuni na Rais Yoweri Museveni ambapo katika hotuba yake ya ufunguzi
alisema “ nimefurahi sana kuanzishwa kwa kituo hiki na hasa kwa kuitwa jina la
Julius Nyerere kwa kuamini ya kwamba wanasiasa wa Uganda, Afrika ya Mashariki,
Afrika na hata duniani kwa ujumla watakitumia ili waweze kujifunza aina mbali
mbali za siasa na uongozi kama urithi wake mwenyewe Baba wa Siasa za ukombozi
barani Afrika Mzee Nyerere”.
Balozi Mlima alieleza
kuwa katika mambo mengi ambayo ameyafanya Mwalimu Nyerere na kumjengea sifa
kubwa ndani na nje ya Bara la Afrika ni pamoja na kuasisi Muungano wa
Tanganyika na Zanzibar waliouasisi yeye na Hayati Mzee Abeid Amani Karume ambao
ulionesha mfano kwa viongozi wa bara la Afrika.
Balozi Mlima
aliteuliwa na Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli na kumuapisha Septemba 12, 2018
Ikulu ya Chamwino Jijini Dodoma, ambapo katika historia yake ya kazi Balozi
Aziz Ponary Mlima aliwahi kuwa Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini
Malaysia.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment