Habari za Punde

Bopar Akabidhi Msaada wa Madawati na Viti Skuli ya Sekondari Umoja Uzini Wilaya ya Kati Unguja

Mfanyabiasha Maarufu Zanzibar wa Kampuni ya Bopar Enterprise, Ndg. Said Nassir Nassor, Bopar akimkabidhi Madawati na Viti Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe. Riziki Juma Pemba akimpokea msaada huo kwa ajili ya Skuli ya Sekondari ya Uzini Mkoa wa Kusini Unguja. Hafla hiyo imefanyika katika viwanja vya Skuli hiyo Uzini Wilaya ya Kati Unguja.

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe. Riziki Pembe Juma amewataka walimu wa Skuli ya Sekondari Umoja Uzini pamoja na kamati ya skuli hiyo kutunza madawati waliyo patiwa na Nd. Said Bopar.

Akizungumza katika makabidhiano ya madawati kutoka kwa Nd. Said Nassir Nassor (Bopar) Jana  katika skuli ya Sekondari Umoja Uzini iliyopo wilaya ya kati Mkoa wa Kusini Unguja.

Mhe. Waziri amemkabidhi mwalimu Mkuu wa skuli ya Sekondari Umoja Uzini meza 50 za watu wawili wawili na viti 100 baada ya kupokea kutoka kwa Nd. Said Nassir kwa lengo la kupunguza tatizo la upungufu wa vikalio maskulini.

Mhe. Waziri amewataka walimu pamoja na kamati ya skuli kuweza kutunza na kuuenzi msaada huo ambao Nd. Said Nassir  amejitolea kwa moyo wa imani kuweza kutoa msaada kwa skuli hiyo.

Hata hivyo, aliwasihi wadau wengine wenye uwezo waweze kuisaidia sekta ya elimu kwani bado inachangamato nyingi ambazo zinahitaji kutatuliwa ili kuwafanya wanafunzi wasome vizuri na kwa utulivu.

Aidha Mhe. Waziri aliwasisitiza wanafunzi kusoma kwa bidii zaidi na kujiwekea malengo ya kupata DIV. I na DIV II kwa wale wanaotarajia kufanya mitihani ya taifa.

Mwisho alimshukuru Nd. Said (Bopar) kwa moyo wa uzalendo aliokuwa nao kwa kuweza kutoa  misaada katika skuli mbali mbali kwa lengo la  kusaidia sekta ya elimu iweze kuimarika.

Kwa upande wa Mwalimu Mkuu wa skuli ya sekondari Umoja Uzini  Nd. Vuai Sabur Muya alimshukuru Bopar kwa msaada wake huo na kusema kuwa umekuja wakati muafaka kwani walikuwa na tatizo la vikalio skulini hapo hali iliyofikia kwa baadhi ya wanafunzi kukaa chini, hivyo madawati hayo yatasaidia sana kuondoa tatizo hilo.

Pia aliiahidi Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kuwa watavitunza vikalio hivyo na watajitahidi sana kuwasimamia wanafunzi wao katika utunzaji wa vikalio hivyo ili na wengine wapate kuja kutumia.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.