Habari za Punde

Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dr.Mabodi Afanya Ziara Wilaya ya Magharibi B Unguja leo.

NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk. Abdulla Juma Mabodi akivuna Tungule katika Shamba la wakulima waliopewa mafunzo ya kilimo cha kisasa huko shehia ya Kisauni.
 NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk. Abdulla Juma Mabodi akikagua  akikagua shamba la mboga mboga aina ya bamia na mchicha kwa kikundi cha wajasiriamali wanaonufaika na ugatuzi huko Kisauni.
NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk. Abdulla Juma Mabodi akizungumza na Watendaji na Viongozi wa Baraza la Manispaa ya Magharib 'B' kabla ya kutembelea miradi.
BAADHI ya Watendaji wa Baraza la Manispaa Magharib 'B ' wakisikiliza hotuba ya mgeni rasmi
NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk. Abdulla Juma Mabodi akikagua kiti maalum cha kung'olea meno katika kituo cha Afya cha Kombeni.


Na.Is-haka Omar - Zanzibar.
NAIBU katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk. Abdulla Juma Saadalla Mabodi amesema CCM itawachukulia hatua za kali za kisheria Watendaji watakaoruhusu kutekelezwa chini ya kiwango miradi mbali mbali katika  Mabaraza ya Manispaa na Halmashauri za Wilaya Zanzibar. 

Kauli hiyo ameitoa katika mwendelezo wa ziara yake katika Manispaa ya Magharib 'B' ,amesema lazima miradi yote hasa inayotekelezwa na mamlaka hizo chini ya mpango wa ugatuzi iwe ni miradi imara iliyopo katika viwango bora.

Amewambia Watendaji hao kuwa lazima wahakikishe miradi yote inayotekelezwa kwa lengo la kurahisisha upatikanaji wa huduma bora za kijamii ziwe na viwango vinavyoridhisha na sio vya kuitia hasara Serikali za Mitaa pamoja na wananchi kwa ujumla.

Dk. Mabodi amesema yeye akiwa ni msimamizi Mkuu wa  Ilani ya CCM ya mwaka 2015/2020 kwa upande wa Zanzibar, ataendelea kufuatilia kwa karibu miradi yote inayotekelezwa na ugatuzi kwa lengo la kujiridhisha kama ina viwango vinavyostahiki. 

Dk. Mabodi ameeleza kuwa miradi ya kijamii inayotekelezwa katika kiwango bora,inasaidia kupunguza gharama zisizokuwa za lazima na kuwawezesha wananchi kupata kwa wakati mahitaji muhimu ya kijamii. 

"Wananchi wanahitaji huduma bora na sio bora huduma ni lazima watendaji mliopewa dhamana kupitia mfuko wa ugatuzi muwe waadilifu wa kuhakikisha miradi yote inayotekelezwa inafuata taratibu zote za kisheria na inakuwa na viwango vinavyositahiki. "ameeleza Dk. Mabodi. 

Pia amesisitiza manispaa hiyo kuendelea kutumia mfumo wa kisasa wa ukusanyaji wa mapato  ili kudhibiti ukwepaji wa kodi. 

Akizungumza Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Mhe. Ayoub Mohamed Mahmoud amesema dhana ya ugatuzi imetekelezwa kwa ufanisi katika Manispaa ya Magharib 'B' kwa kuwanufaisha wananchi wa Shehia mbali mbali zilizomo katika Manispaa hiyo.

RC Ayoub ameleza kwamba pamoja na mafanikio yaliyofikiwa bado Manispaa hiyo inakabiliwa na changamoto ya vitendo vya udhalilishaji, jambo ambalo Mkoa wa Mjini Magharib wanaendelea kuchukua juhudi mbali mbali za kuthibiti uhalifu huo.

Naye Mkurugenzi wa Manispaa ya Magharib 'B' ndugu Ali Abdalla Natepe amesema katika kipindi cha nusu muhula wa awamu ya saba Manispaa hiyo ilijipangia kukusanya mapato kiasi cha shilingi bilioni 4,097,703,098 na kufanikiwa kukusanya jumla ya shilingi bilioni 3,964,119,200 sawa na asilimia 90 ya makadirio.

Amesema jumla ya wakulima 72 wa kikundi cha mboga Mwanakwerekwe (ULEZI KAZI)  wamepatiwa mafunzo ya mboga mboga ikiwemo njia bora ya umwagiliaji wa taka.

Mkurugenzi huyo amesema jumla ya mikarafuu 7,000 imetolewa kwa wakulima wa sheria za Maungani, Kisauni, Kombeni pamoja  na Kibondeni.

Amebainisha kwamba jumla ya lita za maziwa 692,664,Mayai ya kuku trea 826,152 ,kuku wa nyama 714,120 na Mtindi glasi 48,712 zimezalishwa na kukusanywa.

Amebainisha kwamba katika sekta ya uvuvi jumla ya wavuvi 1,000 wamepatiwa mafunzo ya uvuvi endelevu, umuhimu wa mikoko kwa mazao ya baharini pamoja na mabadiliko ya tabia nchi. 

Akizungumza Suleiman Amour Hassan Mkulima wa shehia ya Kisauni ambaye amenufaika na mfumo wa ugatuzi amesema ni miongoni mwa wakulima waliopatiwa mafunzo ya kilimo cha kisasa ambacho kimeinua hali za kiuchumi kwa zaidi ya wakulima 200 wa eneo hilo.

kwa upande wake Muhudumu wa Afya ya Jamii katika Kituo cha Afya ya Mama na Mtoto huko Maungani, ameeleza kuwa kabla ya kujengewa jengo la kisasa Manispaa ya Magharib 'B' walikuwa wakitoa huduma ya elimu ya afya chini ya muembe lakini kwa sasa wamepata Ofisi ya kudumu.

Dk.Mabodi ametembelea miradi mbali mbali iliyotekelezwa na ugatuzi na kutoa miongozi, ushauri na maelekezo ya kuimarisha utendaji wenye ufanisi katika miradi hiyo.

Maeneo yaliyotembelewa ni pamoja na Kituo cha Afya cha Kombeni, Kituo cha Afya ya Mama na Mtoto Maungani, Machinjio ya Kisakasaka, Kikundi cha wajasiriamali cha Ukweli njia Safi kilichopo Bweleo, Shamba darasa la Mboga mboga za aina mbali mbali Kisauni, Bweni la Wanafunzi wa skuli ya Sekondari ya Kiembesamaki pamoja na Jengo la Kituo cha Kisasa cha Jeshi la Polisi katika maeneo ya Chukwani.

Kupitia ziara hiyo Dk. Mabodi akiwa ameambatana na Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa wa Magharib, Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Zanzibar Uongozi wa Mkoa wa Mjini na Magharibi Pamoja na Watendaji na viongozi wa Baraza la Manispaa ya Magharib 'B'.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.