Na Grace Semfuko-MAELEZO
Serikali ya Norway imeingia
makubaliano ya kuisaidia Tanzania katika kuijengea uwezo na kuimarisha mifumo
ya ukusanyaji kodi ambapo imetoa kiasi
cha shilingi bilioni 25 kwa ajili ya shughuli hiyo lengo likiwa ni kuongeza
mapato ya Serikali ambayo yatasaidia ujenzi wa miradi ya maendeleo kwa ajili ya
kunufaisha jamii.
Aidha Norway imesema kupitia
Mfuko wa Dunia (Global Fund) itaendelea kuifadhili Tanzania kutokana na kuridhishwa
kwake na Sera za kuimarisha uchumi,kuondoa rushwa na ufisadi hali ambayo
wamesema inaimarisha na kuongeza ufanisi kiuchumi.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa
Maendeleo ya Kimataifa wa Norway Bwana Nikolai Astrup wakati yeye na masafara
wake walipokutana na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt Ashatu Kijaji,
Ofisini kwake Jijini Dar Es Salaam.
Norway imekua ikichangia zaidi ya
Dola Milioni 660 kwenye mfuko wa Dunia (Global Fund) huku Tanzania ikinufaika
zaidi ambapo kwa mwaka huu kiasi cha Dola Milioni 56 sawa na zaidi ya Sh.
Bilioni 127 zimetolewa kwa ajili ya
kuanzisha na kuimarisha miradi ya maendeleo.
“Tunatambua kuwa Wananchi
wanataka Maendeleo na ndio maana sisi Norway tunafadhili kiasi hiki cha fedha
ili kuhakikisha kuwa wananchi wanapata huduma za kijamii, tutaendelea
kuifadhili Tanzania hasa kwenye Sekta za Elimu, Kilimo, Nishati na Gesi.”
Alisema waziri huyo na kuongeza kuwa lengo la ziara yake ni kuangalia kwa namna gani pande mbili zitaendelea
kushirikiana zaidi.
Katika mazungumzo yao ,Bwana
Astrup amesema kuimarisha mifumo ya ukusanyaji wa kodi, ni hatua muhimu kwa
Serikali zote Duniani kwani fedha zinazokusanywa ndizo zinazofanya maendeleo na
hivyo hatua ya Serikali yake ya kuisaidia Tanzania katika eneo hilo imekuja
wakati muafaka na wanamatumaini makubwa kuwa lengo litafanikiwa.
Kwa Upande wake, Dkt Ashatu
Kijaji alisema wakati Serikali ya awamu ya tano inaingia madarakani mwaka 2015,
ukusanyaji wa mapato ulikuwa ni wastani
wa Shilingi Bilioni 800 kwa mwezi ambapo
kufuatia mifumo ya kodi kuimarishwa, wastani huo umeongezeka kutoka kaiasi cha awali hadi Shilingi Trilioni
1.4 kwa mwezi.
“Serikali ya awamu ya tano
ikishirikiana na Norway katika kuimarisha mifumo ya kodi tumeongeza asilimia 75
ya ukusanyaji wa mapato, ongezeko hilo ni kubwa na tunawashukuru sana kwani
mnaona jinsi ambavyo Rais Magufuli anavyotekeleza miradi ya maendeleo kupitia
fedha hizi,nyote ni mashahidi” Alisema Dkt Ashatu Kijaji, Naibu Waziri wa Fedha
na Mipango.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya
Ulaya na Amerika katika Wizara ya Mambo ya Nje, Jestas Nyamanga alisema Norway imekuwa ikiisaidia Tanzania kwenye
miradi mingi ikiwepo ya Afya kwenye maeneo matatu kupiga vita masuala ya ukimwi
, malaria na kifua kikuu.
Alisema katika Sekta ya nishati
wamesaidia kufadhili usambazaji wa umeme
wa vijijini (REA) katika Mikoa ya Shinyanga, Tabora,Iringa , singida na Dodoma,
ambapo zaidi ya vijiji 121 vimepata umeme huo kwa ufadhili wa Nchi za Norway na Sweeden.
Waziri wa Maendeleo ya Kimataifa
Nicolai Astrup aliwasili Nchini Novemba 28, mwaka huu kwa ziara ya kikazi akiwa
na ujumbe wake, ambapo atafanya
mazungumzo na viongozi mbalimbali wa Serikali, kutembelea Wilaya ya Korogwe
kukagua mradi wa umeme wa REA unaofadhiliwa na nchi yake na pia atakagua mtambo
wa kuzalisha umeme wa maji uliojengwa na Norway, Sweden na Finland kwenye miaka
ya 1990 na kukarabatiwa hivi karibuni na Serikali ya Norway, ambapo ataondoka
Novemba 30 mwaka huu.
No comments:
Post a Comment