Habari za Punde

Wafanyakazi sekta ya Umma watakiwa kujituma na kufanya kazi kwa uaminifu na uadilifu


                                                                                                            
Raya Hamad OR-KSUUUB

Wafanyakazi wa sekta ya utumishi wa umma wametakiwa kujituma na kufanya kazi kwa uaminifu na uadilifu katika kuitumikia nchi.

Waziri wa nchi Ofisi ya Rais Katiba, Sheria, Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Haroun Ali Suleiman ameeleza hayo kwenye  sherehe ya kuwaaga wastafu wa ofisi hiyo  iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano uliopo mazizini, unguja.

Mwalimu Haroun amesema serikali ya Mapinduzi Zanzibar ya awamu ya saba imefanya mambo mengi kwa maendeleo ya wananchi  na mabadiliko ya kwenye utumishi wa umma ikiwa ni pamoja na kuongezewa pencheni pale mfanyakazi anapostaafu  kwa lengo la kuongeza ufanisi katika utumishi serikalini.

Aidha amewapongeza wastafu hao kwa kuwa wazalendo na  kuweza kufanya kazi kwa uadilifu kwa muda wote walipokuwa watumishi wa serikali na kustaafu wakiwa nasifa nzuri na mfano wa kuigwa.

Nae Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Katiba Sheria Utumishi wa Umma na Utawala Bora ndugu  Seif Shaaban  Mwinyi amasema mnamo mwaka 2011Serikali ilifanya  utafiti  wenye lengo la kuimarisha mazingira ya wastaafu kabla na baada ya kustaafu .

Ameyataja mazingira hayo kuwa ni pamoja na kuongezewa pencheni, kuhakikisha wastaafu wanapatiwa mafunzo kabla ya kustaafu, kupewa taarifa ya kustaafu miezi sita kabla, kupatiwa cheti cha heshima, kuagana na kupewa zawadi “ni jambo la faraja pale mtu anapostaafu wenzio wakakuaga na kukuandalia tafrija fupi inapendeza na kujisikia kama wenzangu wananijali wananipenda na wananiombea mazuri” .

Naibu Seif amesema mafunzo kwa wastaafu yanasaidia kujiimarisha mapema ili kuondokana na khofu iliyojengeka kwa baadhi yao pamoja na kujiwekeya mazingira mazuri ya kujiendeleza watakapokuwa nje ya Ofisi mara baada ya kustaafu

Mkurugenzi wa uendeshaji na utumishi  ndugu Bakari   Khamis Muhidin amesema ofisi  ina kila sababu za kuwatunukia vyeti na zawadi za ukumbusho kutokana na utendaji wao mzuri katika kuitumikia Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Kwa niaba ya wastaafu ndugu Ali Shaaban amesema suala la mafunzo ya kujitayarisha kustaafu ni muhimu hivyo ni vyema jambo hilo kutiliwa mkazo na kuendelezwa  kwani kwa upande wake ameiona faida ya kupata mafunzo hayo.

Nao wafanyakazi wa Ofisi hio katika risala ya kuwaaga wafanyakazi hao  wamewapongeza kwa kufikia hatuwa ya kustaafu wakiwa wamemaliza muda wao wa utumishi wakiwa na afya njema yenye furaha ingawa ni masikitiko kwa kutokuwa nao kwani tayari walikuwa ni familia moja hivyo wamewaomba wastaafu hao kutokana na uzowefu wao wa kazi  kutowaacha mkono bali wawe tayari kutumia busara zao hekima na ujuzi pale watakapohitajika .

Aidha wameahidi kwa Mhe Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr Ali Mohamed Shein ambae ndio  Kiongozi mkuu wa Ofisi ya Rais Katiba Sheria Utumishi wa Umma na Utawala Bora kuendelea kufanya kazi kwa taratibu zote na sio kwa mazowea kwani wanaongozwa na Mkataba wa Utoaji Huduma kwa Umma

Wafanyakazi hao waliostaafu wamefanya kazi katika kada tofauti na taasisi mbalimbali  na hatimae kumalizia Ofisi ya Rais Katiba Sheria Utumishi wa Umma na Utawala Bora jumla yao ni saba ambapo wametunukiwa vyeti, fedha taslim na zawadi nao ni  Bw Omar Khamis Shaaban, Bi Asha Ali Omar, Bw Silima Khamis Daima, Bw Ali Shaaban Masoud Bw Joseph Antony Mussa, Bw Rashid Amour Alley na Bw Mohamed Khamis.


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.