Habari za Punde

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Katiba Sheria Utumishi wa Umma na Utawala Bora Zanzibar Mhe Haroun Azungumza na Waziri wa Muungano wa Ofisi ya Waziri Mkuu India

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Katiba Sheria Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe Haroun Ali Suleiman, akizungumza na mwenyeji wake Waziri wa Muungano Ofisi ya Waziri Mkuu anaeshughulikia masuala ya Utumishi wa Umma nchini  India  Dr Jitendra Signh, alipofika ofisini kwake kwa mazungumzo akiwa katika ziara yake nchini india.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Katiba Sheria Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mh Haroun Ali Suleiman  akiwa katika picha ya pamoja na mwenyeji wake Waziri wa Muungano Ofisi ya Waziri Mkuu anaeshughulikia masuala ya Utumishi wa Umma nchini  India  Dr Jitendra Signh

Na.Mwandishi Wetu. 
WAZIRI wa Nchi (OR), Katiba, Sheria, Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Haroun Ali Suleiman, leo amefanya mazungumzo na Waziri wa Muungano Ofisi ya Waziri Mkuu wa serikali ya India anayeshughulikia masuala ya utumishi wa Umma Dk. Jitendra Singh.

Mazungumzo hayo yamefanyika nyumbani kwa mwenyeji wake, Dk. Singh, jijini New Delhi nchini India, yakilenga kukuza mashirikiano kati ya Zanzibar na India.

Mhe. Haroun amemueleza Dk. Singh kuwa, Zanzibar inaridhika na kuimarika kwa mashirikiano ya muda mrefu kati yake na India yaliyojikita katika nyanja tafauti za kimaendeleo.

Aidha alieleza umuhimu wa mashirikiano katika masuala ya utumishi wa umma, ambapo pamoja na mambo mengine, alipendekeza kuwepo programu za ushirikiano katika mafunzo juu ya jambo hilo.

Mhe. Haroun pia, alipendekeza wizara zao ziangalie uwezekano wa wataalamu wa India kuja Zanzibar kusaidia kufundisha masomo katika ngazi ya digrii ya kwanza katika Chuo cha Utumishi wa Umma (IPA).

Aidha alishauri watendaji wa IPA kuanzisha utamaduni wa kufanya ziara za kimafunzo katika chuo cha utumishi wa umma cha India, ambazo pia alisema zitasaidia kubadilishana uzoefu na mbinu za ufundishaji.

Kwa upande wake, Dk. Singh amemshukuru Mhe Haroun kwa kumtembelea na kupata fursa ya kubadilishana mawazo, hali aliyosema ni muhimu katika kuimarisha ushirikiaano uliopo kati nchi hizo mbili.

Alieleza kuwa, India sasa ina chuo kikubwa kinachotoa mafunzo kwa watumishi wa umma, na kwamba kimekuwa kikipokea watumishi kutoka nchi mbalimbali kwa ajili ya kujifunza chuoni hapo.

Dk. Singh alisema wako tayari kushirikiana na Zanzibar katika sekta ya utumishi wa umma na kushauri kutayarishwe mapendekezo yatakayoonesha aina ya masomo yanayohitajika kwa ajili ya watumishi wa Zanzibar, pamoja na walimu wa fani na ngazi gani watakaoweza kuja Zanzibar kufundisha katika chuo cha IPA.

Halikadhalika, amesisitiza kuwa ni muhimu kwa watendaji wa wizara hizo mbili kuwasiliana ili kufanikisha mapendekezo hayo.

Katika ziara hiyo, Waziri Haroun amefuatana na  George Kazi, ambaye ni Naibu Katibu Mkuu wa wizara yake, akiwa amealikwa kuwa mgeni wa heshima katika mkutano mkuu wa majaji wakuu wa dunia.

Mkutano huo umepangwa kuanza tarehe 16 hadi 20 Novemba katika mji wa Lucknow jimbo la Uttar Pradesh, India.

1 comment:

  1. Naomba kufanyike marekebisho kwenye Headline Ni Waziri wa Muungano wa Ofisi ya Waziri Mkuu India na sio Waziri Mkuu .ahsante

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.