Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Balozi Seif Ali Iddi Azungumza na Spika wa Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki Mhe. Martin Karoli.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif  Ali Iddi Kulia akizungumza na Spika wa Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki Mh. Martin Ngagoga katika Ofisi ya Spika wa Baraza la Wawakilishi Chukwani Zanzibar. 
Spika wa Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki Mh. Martin Ngagoga Kushoto akisisitiza jambo wakati wa mazungumzo yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif  Ali Iddi.
Balozi Seif  katu kati akiwa katika picha ya pamoja na Spika wa Bunge la Afrika ya Mashariki Mh. Martin Ngago aliyekaa Kulia yake pamoja na Ujumbe wake mara baada ya mazungumzo yao.Kushoto ya Balozi Seif ni Mh. Marya Ussi Yahya, Mh. Makame Hasnuu na wa kwanza kushoto ni Mh. Fanai Nkuhi.

Na.Othman.Khamis OMPR.
Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki ni Taasisi pekee inayotafakari kwa kina na kuchukuwa hatua muwafaka kwa mujibu wa matakwa ya Nchi  sita Wananchama wa Jumuiya hiyo katika utekelezaji wa majukumu yake iliyojipangia.
Spika wa Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki Mheshimiwa Martin Karoli Ngoga alitoa kauli hiyo wakati wa mazungumzo yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi katika Ofisi ya Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar iliyopo Chukwani nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.
Mheshimiwa Martin Karoli Ngoga ambae amefika Zanzibar na Ujumbe wake kuomba ruksa ya kufanya Vikao vya Bunge Lao Visiwani Zanzibar Mwezi Febuari Mwaka 2019 alisema zipo changamoto katika uwajibikaji wa Bunge hilo, lakini endapo zikitafutiwa ufumbuzi muwafaka zinaweza kuleta faida kubwa kwa Wanachama.
Alisema Wajumbe wa Bunge hilo kutoka Nchi mbali mbali za Jumuiya hiyo wamekua wakishiriki vyema katika Vikao vya Maamuzi yenye kuleta ustawi na muelekeo unaozingatia hatma njema ya Wananchi wake.
Spika huyo wa Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki aliupongeza Uongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na ule wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ushirikiano mkubwa unaowapa Watumishi hao wa Bunge la Afrika Mashariki kitendo ambacho huleta faraja kwa Uongozi mzima wa Bunge hilo.
Naye Mbunge wa Bunge hilo la Jumuiya ya Afrika Mashariki kutoka Zanzibar Mh. Makame Hasnuu aliyeambatana na Spika huyo alisema wakati umefika kwa Mamlaka ya Afrika ya Mashariki kubadilisha mfumo wa bunge hilo ili liendeshwe kwa Lugha ya Kizalendo ya Kiswahili.
Mh. Hasnuu alisema juhudi zinaendelea kufanywa hivi sasa za kushawishi kufanywa kwa marekebisho ya Mkataba kwa lengo la kuchukuwa hatua za Kisekta ili kuliona Bunge hilo la Nne tokea kuasisiwa kwake linafanikiwa vyema.
Naye kwa upande wake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Bunge hilo likiwa na sauti moja maendeleo ya haraka ya Kisiasa na Ustawi wa Kijamii yatakwenda haraka.
Balozi Seif alisema ni vyema kwa Watumishi  hao kuendeleza Umoja wao licha ya tofauti za Kiuchumi na Kisiasa yanayoyakabili baadhi ya Mataifa Wanachama wa Jumuiya hiyo ya Afrika Mashariki.
Alisema Viongozi Waasisi wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki walikuwa na msimamo Mmoja uliopelekea kusimamishwa kwa Jumuiya hiyo licha ya kupata msuko suko mwishoni mwa Miaka ya Sabini.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alimueleza Spika huyo wa Bunge la Afrika Mashariki kwamba Zanzibar inafuatilia muenendo mzima wa Bunge hilo na kuridhika na uwajibikaji wake.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.