Habari za Punde

Uwekaji wa Jiwe la Msingi la Barabara ya Kilomita 31 Kutoka Bububu Hadi Mkokotoni Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Kushoto akipongezwa na Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya China Civic Engeering Construction Company {CCECC} inayojenga Bara bara ya Bububu hadi Mkokotoni  Bwana Zhag Junle mara baada ya kuweka Jiwe la Msingi la Ujenzi wa Bra bara hiyo.
Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya {CCECC}  Bwana Zhag Junle akitoa salamu na kuahidi Kampuni yake kujenga Bara bara ya Bububu hadi Mkokotoni katika kiwango sahihi.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akihutubia Wananchi kwenye hafla ya uwekaji wa Jiwe la Msingi la Ujenzi wa Bara bara ya Bububu hadi Mkokotoni.
Timu ya Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji Zanzibar ikifuatilia matukio mbali mbali yaliyokuwa yakitokea wakati wa hafla ya uwekaji wa Jiwe la Msingi la Ujenzi wa Bara bara ya Bububu hadi Mkokotoni.
Baadhi ya Wananchi walioalikwa kushuhudia hafla ya uwekaji wa Jiwe la Msingi la Ujenzi wa Bara bara ya Bububu kupitia Mahonda, Kinyasini Mkwajuni hadi Mkokotoni.
Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya {CCECC}  Bwana Zhag Junle Kushoto akiteta na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Balozi Seif  kwenye hafla ya uwekaji wa Jiwe la Msingi la Ujenzi wa Bara bara ya Bububu hadi Mkokotoni.
Kikundi cha Utamaduni cya Kijiji cha Nungwi cha Mchikitu kikitoa burdani kwenye hafla ya uwekaji wa Jiwe la Msingi la Ujenzi wa Bara bara ya Bububu hadi Mkokotoni.
Picha na – OMPR – ZNZ.
Na.Othman Khamis OMPR.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amewaasa Wananchi wanaoishi katika maeneo yanayopendekezwa na Serikali kupitishwa Miradi ya Kiuchumi na kijamii kuacha ulalamishi wakati wanapolipwa fidia ya Nyumba au Vipando vyao kwa ajili ya kupisha Miradi hiyo.
Alisema tabia ya baadhi ya Watu kukata sehemu ya Majengo yao hasa katika upishaji wa Ujenzi wa Bara bara na kuendelea kuishi kwenye nyumba hizo wakati tayari wameshalipwa fidia baada ya kukamilisha Tathmini ya Mali zao haistahiki kabisa kwa vile inakwenda kinyume na hali halisi.
Balozi Seif Ali Iddi alitoa nasaha hizo baada ya kuweka  Jiwe la Msingi la Ujenzi wa Bara bara ya Kilomita 31 iliyoanzia Bububu kupitia Mahonda, Kinyasini, Mwajuni hadi Mkokotoni ikiwa ni miongoni mwa Shamra shamra za kusherehekea Maadhimisho ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar kutimia Miak 55.
Balozi Seif  alisema Wananchi lazima waelewe kwamba Serikali itakapohitaji kutanua Bara bara wakati  wowote kulingana na mahitaji ya mabadiliko ya matumizi si vyema ikajichomoza lawama kwa vile wahusika wanakuwa tayari wameshalipwa fidia stahiki.
Alisema hifadhi iliyowekwa  ya utanuzi wa Bara bara kwa mujibu wa Sheria  lazima Wananchi waiheshimu na kujiepusha nayo ili kutoa nafasi kwa Serikali kuendelea kuyasimamia Maendeleo yao ya kila siku ikiwemo Sekta ya Mawasiliano.
Alieleza kwamba Bara  bara ya Mkoa wa Kaskazini Unguja ina Historia  ndefu katika kutoa huduma za Mawasiliano iliyoanza mara baada ya Vita Vikuu vya pili vya Dunia kwa sasa ikiwa ni muhimili mkuu wa Mawasiliano katika Sekta ya Utalii.
Balozi Seif alifahamisha kwamba kukamilika kwa ujenzi wa Bara bara hiyo ya Kilomita 31 kutaleta mabadiliko makubwa ya maendeleo kwa vile harakati za Kiuchumi Kwa Wananchi watakaotumia usafiri kwa eneo hilo zitaongezeka mara dufu.
Hata hivyo Balozi Seif  aliwaomba Wananchi ambao hadi sasa bado maeneo yao hayajafikiwa na Miradi ya Ujenzi wa Bara bara waendelee kuwa wastahamilivu  huku Serikali  Kuu ikiendelea kutafuta njia mbadala za kutanzua changamoto zinazowakabili Wananchi.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwaonya baadhi ya Madereva Nchini kuacha tabia ya kuzifanya Bara bara kuwa makaburi ya Wananchi wanaotembea  kwa miguu na baskeli.
Alisema mara nyingi ajali hutokea  kutokana na uzembe wa baadhi ya Madereva  kwa kutozingatia Sheria, Kanuni na Taratibu  sahihi zilizowekwa za  matumizi ya Bara bara.
Balozi Seif aliwahakikishia Wananchi kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kutekeleza majukumu yake iliyojipangia licha ya baadhi ya kejeli zinazoendelea kutolewa na Watu wasioelewa wanataka nini.
“ Wenzetu hawa inapaswa watafutiwe  dawa kwa vile  inaonekana baadhi yao  wamevaa Miwani za mbao zinayoshindwa kuona upande wa Pili”. Alisema Balozi Seif.
Alisema wapo baadhi ya Watu wana kasoro ya kutoona  Maendeleo makubwa yanayofanywa na kutekelezwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya Mwaka 2015 – 2020 inayosimamiwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohamed Shein.
Mapema Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji Zanzibar Nd. Mustafa Aboud Jumbe  alisema Ujenzi wa Bara bara ya Bububu hadi Mkokotoni kupitia Kinyasini na Mkwajuni ni miongoni mwa Miradi ya Ujenzi wa Bara  Bara mbali mbali Nchini iliyoanza rasmi Mwezi Juni Mwaka 2018.
Nd. Mustafa alisema zipo Bara bara nyengine katika mpango huo Unguja na Pemba ambazo zinasimamiwa na Serikali katika juhudi zake za kuwajengea mazingira bora ya Mawasiliano Wananchi wake.
Alisema Bara bara ya Bububu hadi Mkokotoni iliyoanza kujengwa mara baada ya Vita vya Pili vya Dunia kwa ujenzi wa kifusi, Mawe na Lami baridi ilijengwa tena upya mnamo Mwaka 1995  kwa Msaada wa Shiriika la Misaada ya Maendeleo la Denmack {Danida}.
Nd. Mustafa alieleza kwamba ongezeko kubwa  la mahitaji zaidi  ya Mawasiliano limeifanya Serikali kuijenga upya Bara bara hiyo kwa Mkopo wa Benki ya Maendeleo ya Afrika {ADB} chini ya Ujenzi wa Kampuni ya Kimataifa ya China Civil Engeering Construction Company {CCECC} ya Jamuhuri ya Watu wa China.
Alisema Bara bara hiyo itakayokuwa na upana wa Mita 6 itajengewa mabega na kuifanya kuwa na upana wa Mita 10.5 ambapo lengo la baadae ni kufikia Mita 15 ikiwa na Madaraja Sita na Makalvati 26.
Pamoja na Mambo mengine Nd. Mustafa alisema ujenzi wa bara  bara hiyo utaambatana na neema itakayowafikia moja kwa moja Wananchi itayolenga ujenzi wa Kituo kikubwa cha Abiria eneo la Mkokotoni, kusaidia nguvu katika Ujenzi wa Gati ya Mkokotoni,  msaada kwa Kituo cha Afya pamoja na Vikalio kwa Skuli ya Chaani.
Akitoa salamu katika hafla hiyo Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya China Civic Engeering Construction Company {CCECC} Bwana Zhag Junle aliwahakikishia Wananchi wa Zanzibar  pamoja na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwamba Wahandisi wake watakamilisha Ujenzi wa bara bara hiyo kwa wakati na kiwango kinachokubalika Kimataifa.
Bwana Zhang aliishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar  kwa kuwaamini kuwapa dhamana ya Ujenzi wa Bara bara hiyo ambayo wanaithamini jambo ambalo watalazimika kutumia utaalamu na ujuzi wao katika kufanikisha kazi hiyo muhimu.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.