Habari za Punde

WAFANYAKAZI WA WIZARA YA AFYA WAFANYIWA VIPIMO VYA AFYA ZAO

Naibu Waziri wa Afya Zanzibar Harusi Said Suleiman akifanyiwa kipimo cha sukari mwilini na Muuguzi Mere Hamad Jadi katika zoezi maalum la kuwapima wafanyakazi wa Wizara ya Afya lililofanyika Wizanani kwao Mnazi mmoja Mjini Unguja.
Jopo la madaktari wakichina na madaktari wazalendo wakiendesha zoezi la kuwafanyia uchunguzi wa afya Wafanyakazi wa Wizara ya Afya Zanzibar lililofanyika katika Wizara hiyo Mnazimmoja Mjini Unguja.
 Dk. Lee Hua Chao akimfanyi uchunguzi wa sikio Bi. Sabrina Abdalla Muhamed, mmoja ya wafanyakazi wa Wizara ya Afya Zanzibar walipofika kufanyiwa uchunguzi wa afya zao Wizarani hapo. 
Naibu Waziri wa Afya Zanzibar Harusi Said Suleiman (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na madaktari wa kichina nje ya Wizara hiyo baada ya kuzindua zoezi la kupima afya kwa Wafanyakazi wa Wizara yake.
Picha na Makame Mshenga
Na Ramadhani Ali Maelezo.
Wizara ya Afya Zanzibar kwa kushirikiana na Kitengo chake cha Maradhi yasiyoambukiza wamefanya zoezi la kupima afya za Wafanyakazi wa Wizara hiyo lilioendeshwa na madaktari wa kichina na madaktari wazalendo wanaofanyakazi Hospitali kuu ya Mnazimmoja.
Akitoa nasaha wakati wa kuanzisha zoezi hilo, Naibu Waziri wa Afya Zanzibar Harusi Said Suleiman alisema lengo la kufanya uchunguzi wa afya za wafanyakazi wa Wizara hiyo ni kuwawezesha kujua afya zao na ni moja ya njia ya kuhamasisha jamii kuona umuhimu wa kupima afya zao mara kwa mara kila inavyowezekana.
Alisema Wizara kwa kushirikiana na Kitengo cha maradhi yasiyoambukiza inampango wa kutoa huduma za aina hiyo katika taasisi nyengine kwa malengo ya kuhamasisha uchunguzi wa afya mapema kabla ya kusubiri kuugua.
Aliongeza kuwa Wizara imeamua kutoa huduma hiyo kwa wafanyakazi wake baada ya kugundulika kuongezeka kwa kasi maradhi yasiyoambukiza Zanzibar na duniani kwa jumla.
Alisema kati ya wafanyakazi 1,940 waliopimwa afya zao mwaka 2016 asilimia 6.0 waligunduliwa wakiwa na kisukari na Shinikizo la damu imefikia asilimia 33 kiwango ambacho ni kikubwa kwa mujibu wa idadi ya wananchi wa Zanzibar.
Aliwataka wafanyakazi wa Afya kujitokeza kwa wingi kupima afya zao kila fursa inapotokea kwani mfanyakazi akiwa na afya bora utendaji wake wa kazi wa kutoa huduma kwa wananchi utaimarika.
Naibu Waziri wa Afya alikumbusha kuwa mwishoni mwa mwezi Disemba madaktari wa china wakishirikiana na madaktari wazalendo walimaliza zoezi la uchunguzi wa Saratani ya mlango wa kizazi kwa awamu ya kwanza na zoezi kama hilo litaendelea tena katika mwezi wa Juni na Septemba mwaka huu.
Amewaomba wananchi wajitokeze kwa wingi muda huo utakapofika ili waweze kutambua afya zao mapema huku wakijua kwamba kinga ni bora kuliko kutibu.
Naibu Waziri wa Afya Harusi Said Suleiman aliwapongeza madaktari wa china kwa upendo na msaada mkubwa wanaotoa kwa wananchi wa Zanzibar hasa katika hospitali ya Mnazimmoja na Abdalla Mzee Mkoani na hivi sasa wameanzisha utaratibu wa kutoa huduma za uchunguzi na matibabu katika maeneo ya vijijini kila baada ya miezi mitatu hadi sita.
Kiongozi wa madaktari wa China wanaofanyakazi Hospitali ya Mnazimmoja Dk. Zhang Zhen alisema wataendelea kushirikiana na Wizara ya Afya kuhakikisha wanatoa huduma bora zaidi kwa wananchi wa Zanzibar.
Alisema ushirikiano kati ya China na Zanzibar ulianza miaka mingi iliyopita na lengo la nchi zote mbili ni kuona ushirikiano huo unaendelea kuimarika zaidi.
Vipimo vilivyofanyika katika zoezi hilo ni shinikizo la damu, kisukari, matatizo ya macho, masikio, kinywa pamoja na ushauri kwa magonjwa  ya akinamama na maradhi mengine sugu. Wafanyakazi waliogundulika na matatizo watapatiwa matibabu katika Hospitali kuu ya Mnazimmoja.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.