Habari za Punde

Jaji Mkuu wa Zanzibar Ahutubia Wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Sheria Zanzibar Kisiwani Pemba Wilaya ya Wete.


Jaji Mkuu wa Zanzibar Mhe Omar Othman Makungu akihutubia wakati wa hafla ya Maadhimisho ya Siku ya Sheria Zanzibar, zilizofanyika katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi Wete Kisiwani Pemba. 


Na.Abdi Shamna -Pemba.
JAJI mkuu wa Zanzibar. Omar Othman Makungu amesema taasisi za umma zinathamni mchango mkubwa wa serikali katika kufanikisha mageuzi ya kutendaji, ili kufanikisha dhana  ya utoaji  bora wa haki katika jamii.

Amesema taasisi hizo, ikiwemo mahakama, Ofisi ya Mwendesha mashtaka, pamoja na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu zinaridhishwa na juhudi zinazochukuliwa na serikali katika kuimarisha miundombinu, upatikanaji wa vifaa pamoja na mafunzo kwa watendaji.

Jaji mkuu amesema hayo leo katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi Wete, wakati akitoa nasaha zake katika kilele cha maadhimisho ya siku ya Sheria Zanzibar.
Maadhimisho ya Siku ya Sheria Zanzibar yanaakisi kuanza kwa mwaka mpya wa sheria hapa Zanzibar.

Alisema kutokana na mchango huo shughuli za Mahakama zimeimarika, hususan baada ya Serikali kuteuwa Majaji, mahakimu na makadhi wapya katika ngazi zote za mahakama Unguja na Pemba.

Alisema kwa nyakati tofauti watendaji wa taasisi hizo wamepata mafunzo ya ndani na nje ya nchi, hivyo kujenga uwezo katika kufanikisha dhana ya serikali ya upatikanaji wa haki bora kwa jamii.

Aidha, aliipongeza Serikali kwa kuimarisha mhimili huo wa Dola (mahakama) kimuundo na kibajeti , sambamba na hatu ya kuanzisha mfuko wa mahakama, ambao utaiwezesha taasisi hiyo kufanyakazi zake kwa ufanisi zaidi.

Jaji Othman aliipongeza serikali kwa kuanzisha mradi wa usalama na kufunga kamera za CCTV, hatua itakayosaidia sana kuimarisha usalama wa mji pamoja na kubaini makosa mbalimbali, yakiwemo ya usalama barabarani, hivyo kuipunguzia kazi mahakama.

Jaji Othaman, alipongeza azma ya serikali ya kuanzisha ujenzi wa jengo jipya la mahakama kuu katika eneo la Tunguu, litakaloambatana na skuli ya mafunzo ya sheria ‘Law school’.

Aidha, Waziri wa Wizara ya Nchi (OR) katiba, Sheria, Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Haroun Ali Suleiman aliwapongeza viongozi wa Serikali wa Mikoa na Wilaya kisiwani Pemba kwa mashirikiano makubwa yaliofanikisha vyema sherehe hizo.

Nae, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Said Hassan Said alisema uimarishaji wa taasisi za umma utarahisisha upatikanaji wa haki katika suala zima la Utawala Bora.

Alisema changamoto iliopo kwa baadhi ya watendaji wa taasisi za umma, inatokana na ukosefu wa utaalamu, weledi na ukiukwaji wa maadili .

Alisema kuna umuhimu wa kuimarisha mfumo ili kuwajengea zaidi uwezo watendaji wa taasisi hizo ili hatimae waweze kufanyakazi zao kwa ufanisi.

Alisema Ofisi ya Mwanasheria Mkuu itashirikiana na taasisi zote za umma pamoja na wadau wa sheria kufanikisha malengo ya kuwepo kwake.

Alisema ni mpango wa Ofisiya Mwanasheria mkuu  kufungua Ofisi kisiwani Pemba katika mwaka huu wa fedha 2019/2020, sambamba na kuendesha program ya ‘outreach’ ili wananchi waweze wafaidika na huduma za kisheria.

Mapema, Mkurugenzi wa Mashtaka Zanzibar (DPP), Ibrahim Mzee alisema utatuzi wa migogogro kupitia mifumo isiyo rasmi, hususan ule wa kujichukulia sheria mikononi ina madhara makubwa kwa jamii.

Alisema suala la upatikanaji wa haki ni kiashiria muhimu katika maendeleo ya watu kiuchumi na kijamii.

Alisema Ofisi ya DPP itaendelea kushirikiana na tasisi nyengine za umma, ili kufanikisha dhana ya upatikanaji wa haki, ili jamii iweze kupata haki kwa usawa.

Aidha, Mwakilishi wa Chama cha Wanasheria Zanzibar Omar Said Shaaban, alisema mjumuiko huo unatowa fursa kwa wadau wa sheria kukumbusha changamoto zinaoikabili sekta hiyo na jamii kwa jumla ili kuzipatia ufumbuzi.

Alisema ipo haja ya kuziimarisha taasisi zote, ikiwemo za binafsi ili kuondokana na changamoto mbali mbali katika suala zima la upatikanaji wa haki.

Aidha alisema wakati umefika kwa Zanzibar kuwa na chama chake ‘ Zanzibar Law Society’ kwa mujibu wa sheria zitakazopitishwa na Baraza la Wawakilishi, ili kuweza kutekeleza wajibu wake kisheria.

Maadhimisho hayo yalioambatana na kauli mbiu “uimarishaji wa Taasisi za Umma ni Ustawi bora wa Upatikanaji wa Haki kwa jamii”, yalihuduriwa na Majaji, Mahakimu, Makadhi, Masheha, Viongozi wa Dini, Viongozi wa Vikosi vya Ulinzi na Usalama pamoja na wadau wengine wa sheria kutoika mikoa ya Unguja na Pemba.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.