Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein, akizungumza na Waziri wa Kilimo na Masuala ya Ardhi wa Jamuhuri ya Kiarabu ya Watu wa Misri.Dkt. Ezzaldin O. Abusteit, alipofika Ikulu Zanzibar na Ujumbe wake, kwa mazungumzo na kufanya Ziara Maalum Zanzibar.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.
Ali Mohamed Shein ameipongeza azma ya
Jamhuri ya Kiarabu ya Misri ya kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika
kuimarisha sekta ya kilimo hapa nchini.
Hayo aliyasema leo
Ikulu mjini Zanzibar wakati alipofanya mazungumzo na Waziri wa Kilimo na
Masuala ya Ardhi wa Jamhuri ya Kiarabu ya Misri Dk. Ezzaldin Abusteit ambapo
katika mazungumzo hayo Waziri huyo pia, aliahidi kushirikiana na Zanzibar
katika kuliimarisha na kuliendeleza shamba la pamoja na Kilimo la JKU- Bambi, liliopo
Mkoa wa Kusini Unguja.
Katika maelezo yake
Rais Dk. Shein alieleza kuwa Misri imekuwa mshirika mkubwa wa Zanzibar katika kuunga
mkono juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar za kuimarisha sekta za
maendeleo ikiwemo kilimo ambayo ni sekta muhimu katika maisha ya Wazanzibari.
Rais Dk. Shein
alieleza kuwa azma ya Serikali ya Misri ya kuendeleza mashirikiano katika
uendelezaji wa mradi wa Shamba la pamoja la JKU-Bambi ambalo ni ushirikiano
kati ya nchi hiyo na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar umeweza kuleta tija na
maendeleo makubwa katika sekta ya kilimo.
Alieleza kuwa miongoni
mwa mafanikio yaliopatikana ni pamoja na kuwepo kwa wataalamu na utaalamu
unaotokana na msaada wa Misri ambapo juhudi hizo zimeweza kusaidia kwa
kiasikikubwa katika kuendeleza sekta ya kilimo nchini hasa katika mradi huo.
Hivyo, katika maelezo
yake Rais Dk. Shein alisisitiza haja ya kuendeleza ushirikiano huo sambamba na kuzidisha
mikakati kwa kuendeleza tafiti za pamoja katika sekta hiyo kwa lengo la
kuzidisha uzalishaji, mbegu, aina za udongo na tafiti nyenginezo kwenye vianzio
vya kilimo.
Aidha, Rais Dk. Shein
alimueleza kiongozi huyo mikakati iliyowekwa na Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar katika kuimarisha sekta ya kilimo hasa katika kuliendeleza na
kuliimarisha Shamba hilo sambamba na Serikali ilivyojipanga katika masuala ya
utafiti wa kilimo ikiwa ni pamoja na kuipa kipaumbele taasisi ya utafiti pamoja
na Chuo cha Kilimo kiliopo Kizimbani.
Alieleza kuwa kwa
upande wa chuo hicho cha Kilimo, tayari kimeshaungwanishwa na Chuo Kikuu cha
Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) kwa lengo la kupata mafanikio zaidi katika
utoaji wa taaluma ndani ya sekta ya kilimo.
Rais Dk. Shein alisema
kuwa tayari mwanzo mzuri umeanza kuonekana katika mashirikiano ya uendelezaji wa sekta hiyo ya
kilimo kati ya Misri na Zanzibar na kusisitiza haja ya kuuendeleza ushirikiano
huo ili uzidi kuleta mafanikio kwa pande zote mbili.
Sambamba na hayo, Rais
Dk. Shein alitilia mkazo suala la mafunzo kwa wataalamu wa kilimo wa Zanzibar
na kueleza haja ya kuendelezwa utamaduni uliokuwepo hapo siku za nyuma ambapo
watalamu walio wengi walipata mafunzo nchini humo katika Chuo Kikuu cha
Al-Azhar.
Katika maelezo hayo,
Rais Dk. Shein pia, alipongeza uhusiano na ushirikiano wa muda mrefu uliopo
kati ya Misri na Zanzibar na kusisitiza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
itaendelea kushirikiana na Serikali ya Misri pamoja na Kiongozi wake mkuu Rais
Abdel Fattah El-Sisi na wananchi wote wa Taifa hilo.
Nae Waziri wa Kilimo
na Masuala ya Ardhi wa Jamhuri ya Kiarabu ya Misri Dk. Ezzaldin Abusteit
alimueleza Rais Dk. Shein azma ya Serikali ya Jamhuri ya Kiarabu ya Misri
ilivyokusudia kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha sekta ya kilimo hapa
nchini.
Katika maelezo yake
kiongozi huyo wa Serikali ya Misri aliyefika Ikulu mjini Zanzibar akifuatana na
ujumbe wake kutoka serikali hiyo pamoja na Balozi wa nchi hiyo anaefanyia kazi
zake katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Gaber Mohamed ambapo Waziri
Abusteit alizipongeza juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar za kuimarisha
sekta ya kilimo.
Katika maelezo yake
Waziri huyo wa Kilimo wa Misri alimueleza Rais Dk. Shein kuwa Misri inathamini
uhusiano na ushirikiano wa kihistoria uliopo kati ya pande mbili na kueleza
kuwa Serikali ya nchi yake utauendeleza na kuuimarisha ili uzidi kuleta tija na
manufaa makubwa.
Waziri Abusteit
alitumia fursa hiyo kumpa Rais Dk. Shein salamu kutoka kwa Rais wa Jamuri ya
Kiarabu ya Misri Abdel Fattah El-Sisi ambazo salamu hizo pia, zilisisitiza
kuimarisha uhusiano na mshirikiano katika ya Zanzibar na Misri huku zikieleza
kutambua juhudi zinazochukuliwa na Serikali anayoiongoza Dk. Shein katika
kuimarisha sekta ya kilimo.
Aidha, Waziri huyo
alimueleza Rais Dk. Shein kuwa kutokana na Wizara yake kubeba mambo muhimu
yakiwemo kilimo, uvuvi na mengineyo ambayo yanashabihiana na Wizara ya Kilimo,
Maliasili, Mifugo na Uvuvi ya Zanzibar itajenga ukaribu mkubwa zaidi katika
kushirikiana.
Aliongeza kuwa Misri
itahakikisha inashirikiana na Zanzibar katika kuleta Mapinduzi ya Kilimo kwa
kuweka kipaumbele suala la mafunzo kwa wataalamu, teknolojia ya kisasa katika
kilimo pamoja na vifaa vya kilimo ili kuendana na kilimo cha kisasa na chenye
tija.
Pia, Waziri huyo wa
Kilimo wa Misri alimuhakikishia Rais Dk. Shein kuwa Misri iko tayari katika
kuyaunga mkono malengo ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iliyoyaweka katika kuendeleza
na kuimaisha sekta ya kilimo kwa ajili ya maendeleo ya Zanzibar na watu wake.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment