Habari za Punde

Uzinduzi wa Mtambo wa Sola Magereza Kuu Arusha Yapatiwa Nishati ya Umeme wa Jua.

Mkuu wa Mkoa wa Arusha akiteta Jambo katika uzinduzi wa Mtambo wa sola uliofungwa na kampuni ya Mobisol katika   Magereza kuu ya Arusha.

Na. Ahmed Mahmoud Arusha.
Magereza kuu ya Arusha  imepatiwa msaada wa nishati ya umeme jua iliyotolewa na kampuni ya sola ya Mobisol ili kuhakikisha upatikanaji  wa nishati ya uhakika katika magereza hiyo na kuondokana na changamoto ya kukatika kwa umeme Mara kwa Mara.

Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mrisho Gambo akizindua mitambo ya umeme jua katika magereza hiyo alisema kuwa mitambo hiyo itasaidia kuimarisha usalama  kwa wafungwa na askari magereza kwani eneo hilo linahitaji nishati ya uhakika.

Gambo alisema kuwa kampuni hiyo imefanya ubunifu mkubwa wa kuikumbuka magereza taasisi ambayo ilikua ikisahaulika na wadau wa maendeleo.

Mmoja wa Waasisi wa Kampuni ya Mobisol  Livinus Manyanga alisema kuwa msaada huo ni kutambua changamoto ya nishati iliyopo ila kwa sasa mitambo waliyoiweka itasaidia kuongeza ufanisi wa uendeshaji wa shughuli za magereza.

"Mitambo hii imegharimu kiasi cha shilingi milioni 16 na tutaihudumia kwa kipindi cha zaidi ya miaka mitatu ili kusaidia Wafungwa na Mahabusu wapate mwanga wa uhakika" Alisema Manyanga

Mkuu wa Gereza la Arusha Anderson Kamtyaro wameishukuru kampuni ya Mobisol kwa msaada huo ambao itasaidia  kuwezesha magereza na wafungwa kufanya kazi katika mazingira bora ya kazi.

Anderson aliwataka Wadau wengine kuiga mfano wa kampuni ya Mobisol kwa kujitoa kutatua changamoto zilizoko kwenye taasisi za serikali.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.