Habari za Punde

Serikali Imejiandaa Vyema Kunufaika na Ujio wa Mashindano ya AFCON
Naibu Waziri Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe.Juliana Shonza akijibu swali la Mbunge wa Konde Mhe.Khatib Haji (CUF) kuhusu mgao wa fedha za FIFA zinazopelekwa TFF na utaratibu unaotumiwa na TFF kuwapatia fedha hizo Chama cha Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFA) leo Bungeni jijini Dodoma.

Na Anitha Jonas - WHUSM. -Dodoma.

Serikali kwa kushirikiana na taasisi zote muhimu imejiandaa kupokea wageni wote watakao shiriki mashindano ya AFCON yanayotarajia kufanyika nchini hivi karibuni .


Kauli hiyo imetolewa leo bungeni jijini Dodoma na Waziri Mkuu Mheshimiwa Kassim Majaliwa alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Kilolo Venance Mwamoto (CCM) wakati wa maswali ya papo kwa papo ya wabunge.


"Serikali inatambua maandalizi yanayofanyika na Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo  kwa kushirikiana na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) pamoja na wadau mbalimbali  na tunatambua kuwa tutapokea wageni wengi akiwemo Rais wa Shirikisho la Mpira Duniani (FIFA)",alisema Mhe.Waziri Mkuu Majaliwa.


Aidha,Mheshimiwa Waziri Mkuu aliendelea kusema kuwa kupitia mashindano hayo serikali imehamasisha Mikoa ya jirani kujipanga kunufaika na mashindano hayo na jumla ya viwanja vitatu vitatumika  na  nijukumu la watanzania wote kushirikiana ili kuhakikisha tunanufaika kwa ujio huu mkubwa.


Pamoja na hayo Mheshimiwa Majaliwa aliendelea kuwasisitiza TFF kuimarisha maandalizi ya timu hiyo itayoshiriki ili taifa liweze kuibuka kidedea,vilevile aliwasihi watanzania wote   kuonyesha uzalendo kwa timu yao ili kuweza kuwatia moyo kwa kuwa na  imani kuwa timu hiyo itaweza kushinda.


Nae Naibu Waziri Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe.Juliana Shonza ametoa majibu ya swali la Mbunge wa Konde Mhe.Khatibu Haji (CUF) lilihoji kuhusu mgao wa fedha zinazotolewa na FIFA kwa TFF kuwa ni kiasi gani zimekwisha pelekwa kwa Chama cha Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFA) kwa kusema kuwa kuwa kufuatia changamoto TFF kutokukidhi vigezo vya utawala bora na uwazi katika matumizi ya fedha kwa zaidi ya miaka mitatu wamekuwa hawapati mgao na FIFA ila kwa kuanzia mapema mwaka huu wanatarajia kuanza kupata mgao huo baada ya kutatua changamoto hizo.


Halikadhalika katika swali la nyongeza Mhe.Naibu Waziri Shonza alijibu kuwa si kweli kuwa ZFA haijawahi kupatiwa msaada wa TFF kwani wameshawahi kupatiwa msaada wa miradi moja wapo ni ujenzi wa ukarabati wa uwanja wa Gombani Pemba na kufafanua kuwa ZFA ni sehemu ya TFF hivyo fedha zinazoletwa na FIFA kwa TFF hugawiwa  kwa mashirikisho yote na ZFA hawaletewi fungu lao peke yao kwani ZFA siyo mwanachama FIFA wala CAF. 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.