Habari za Punde

Watu Wenye Ulemavu Wapewa Elimu ya Sera ya Huduma Ndogo za Fedha

Mchumi Mkuu kutoka Wizara ya Fedha na Mipango, Dionisia Mjema, akiwasilisha mada kwa watu wenye ulemavu wa kusikia (viziwi) ambapo alitoa wito kwa walemavu wote nchini kushiriki katika shughuli mbalimbali za kuwawezesha kiuchumi, wakati wa Semina ya Elimu ya Sera ya Taifa ya Huduma Ndogo za Fedha kwa makundi maalum iliyoandaliwa na wizara hiyo, mkoani Mwanza.
Baadhi ya washiriki wa Semina ya Elimu ya Sera ya Taifa ya Huduma Ndogo za Fedha kwa makundi maalum wakifuatilia kwa makini mafunzo hayo yaliyoandaliwa na Wizara ya Fedha na Mipango , Jijini Mwanza.
Mmoja wa washiriki akielezea changamoto za watu wenye ulemavu wa kusikia (viziwi) kwa kutumia lugha ya alama, likiwemo suala la mawasiliano,  katika Semina ya Elimu ya Sera ya Taifa ya Huduma Ndogo za Fedha kwa makundi maalum iliyoandaliwa na Wizara ya Fedha na Mipango, mkoani Mwanza.
Mchumi Mkuu kutoka Wizara ya Fedha na Mipango, Dionisia Mjema (Watatu kushoto), akiwa katika picha ya pamoja na Maafisa waandamizi wa wizara hiyo pamoja na  Washiriki wa Semina ya Elimu ya Sera ya Taifa ya Huduma Ndogo za Fedha kwa makundi maalum iliyoandaliwa na Wizara hiyo,  mkoani Mwanza.

(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Fedha na Mipango)

Na Farida Ramadhani, WFM, Mwanza
Wizara ya Fedha na Mipango imeanza kutoa elimu ya Sera ya Taifa ya Huduma Ndogo za Fedha kwa watu wenye ulemavu wa kusikia (Viziwi) kwa lengo la kuwajengea uwezo na kushirikishwa katika Huduma Jumuishi za Fedha.

Akizungumza katika mafunzo hayo, Mchumi Mkuu kutoka Wizara ya Fedha na Mipango, Dionisia Mjema, ameeleza kuwa mafunzo hayo yameanza mkoani Mwanza na yanatarajia kuwafikia makundi maalumu yote na wananchi wa hali ya chini ili  kuwawezesha kutumia fursa zilizopo kwa ajili ya kuinua maisha yao na kuchangia katika uchumi wa nchi.

“Miongoni mwa malengo ya Sera ya Taifa ya Huduma Ndogo za Fedha ni kuangalia makundi maalum kwa kujua changamoto zao na kuona namna ya kuzitatua na namna  makundi hayo yanaweza kujiunga kwenye vikundi (solidarity groups) kwa ajili ya kupatiwa mikopo ili kujishughulisha katika shughuli za kiuchumi”, alisema Bi. Dionisia.

Mjema alisema Sera hiyo inalenga kuongeza utoaji wa huduma bora na jumuishi za kifedha kwa wananchi wa kipato cha chini na makundi maalum  ili  kuongeza  ukuaji wa uchumi na kupunguza umaskini.

Alisema Serikali inatambua umuhimu wa Huduma Ndogo za Fedha katika kukuza uchumi wa nchi na kuwa, ili kuboresha usimamizi na udhibiti wa Sera hiyo, imetunga Sheria ya  Huduma Ndogo za Fedha  mwaka 2018 ambayo inatoa mwongozo na kusimamia utekelezaji wa Sera pamoja na kuwalinda watumiaji wa huduma za fedha nchini.  

Mjema alitoa wito kwa watu wenye ulemavu kushiriki shughuli za maendeleo kwa kuwa fursa zipo nyingi na wana nafasi kubwa katika jamii.

Naye Katibu Mtendaji wa Taasisi ya Maendeleo ya Viziwi nchini (TAMAVITA), Kelvin Nyema, ameipongeza Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango kwa kuandaa mafuzo hayo, kwa kuwa anaamini mafunzo hayo yataongeza uelewa kwa wenye ulemavu wa kusikia ambao wengi walikuwa hawana uelewa wa masuala mbalimbali ya kifedha.

Nyema alisema changamoto kubwa inayowakabili ni mawasiliano ambayo inasababisha wasishirikishwe katika shughuli mbalimbali za maendeleo na za kijamii.

“Mawasiliano ni changamoto kubwa kwetu viziwi, ni kikwazo hata katika kushiriki kwenye shughuli mbalimbali za maendeleo, ukizingatia lazima tuwe na wakalimani”, alisema.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Viziwi mkoani Mwanza (CHAVITA) Jones George, ameiomba Serikali kuweka mazingira wezeshi kwa wenye ulemavu wa kusikia (viziwi) kupata mikopo ili waweze kujikwamua kiuchumi.

Alisema hali ya watu wenye ulemavu wa kusikia ni ngumu, hawana elimu yoyote ya masuala ya fedha na hawajui waanzie wapi huku akibainisha kuwa kuna wakati wanaogopa kukopa kwa dhana kuwa wakikopa watafungwa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.