JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
OFISI
YA WAZIRI MKUU
Simu: +255-26-232-2484/232-4560 Mlimwa Kusini,
11 Barabara ya Edward Sokoine,
Nukushi: +255-26-232-1955, S. L. P. 980,
2 Februari, 2019
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
WAZIRI MKUU AFUNGUA WIKI YA SHERIA
*Asema Serikali ni mdau muhimu wa Mahakama
WAZIRI Mkuu, Kassim
Majaliwa amesema Serikali imeendelea kushirikiana na Mhimili wa Mahakama katika
kuhakikisha huduma bora za utoaji haki zinawafikia wananchi kwenye maeneo
wanayoishi kwa wakati.
“Serikali ya Awamu ya
Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli ni mdau muhimu wa Mahakama na
inafuatilia kwa karibu changamoto zote zinazoikabili pamoja na wadau wengine
katika mfumo wa utoaji haki.”
Ameyasema hayo leo (Jumamosi, Februari 2, 2019) wakati akifungua wiki ya Sheria Tanzania katika viwanja wa
Nyerere Square jijini Dodoma. Ametoa wito kwa wananchi watembelee mabanda ya
maonesho hayo.
Amesema kupitia wiki
ya sheria wanachi watapata elimu kuhusu masuala ya sheria pamoja na kushuhudia
na kunufaika na maboresho yanayofanywa na Mahakama kwa kushirikiana na wadau
mbalimbali katika utoaji haki.
Waziri Mkuu amesema
jambo hilo ni jema kwani masuala ya kisheria si mepesi kujulikana kwa kila mwananchi
na kwa sababu hiyo, wananchi wengi wamekuwa na uelewa mdogo wa masuala hayo ya
kisheria.
Amesema wananchi
wengi hawajui taratibu na mienendo ya kimahakama na wakati mwingine wanakosa au
kupoteza haki zao kwa kigezo cha kutofuata taratibu ili kupata haki zao hizo.
“Nitoe rai kwa
wananchi watumiae ipasavyo fursa hii ya Wiki ya Sheria inayoambatana na
maonesho kwa lengo la kupata elimu na huduma mbalimbali hususan za kisheria.”
Akizungumzia kuhusu dhamira ya
Mahakama kutumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika kuleta
mabadiliko kwenye utoaji haki, amesema ni hatua nzuri na itasaidia kuboresha
utoaji wa haki kwa wakati.
Hata hivyo, Waziri Mkuu amewasihi
katika matumizi hayo ya mifumo ya TEHAMA wasikatishwe tamaa na changamoto
zitakazojitokeza kwani mara nyingi kitu kipya chochote hakikosi changamoto za
hapa na pale.
“Binafsi naunga mkono uamuzi wa dhati
wa Mhimili wa Mahakama kutumia TEHAMA katika usajili wa mashauri. Uamuzi huo
unakwenda sanjari na azma ya Serikali ya kuhakikisha TEHAMA inatumika vema
kwenye taasisi za umma kwa lengo la kutoa huduma bora na kwa wakati.”
Kadhalika, Waziri Mkuu amesema matumizi
bora ya TEHAMA yataipunguzia Serikali na mihimili mingine ya dola gharama za
uendeshaji hususan katika utoaji huduma kwa wnanchi.
Amesema lengo la Serikali ni kuona
kuwa huduma bora zinawafikia wananchi kwa urahisi na vilevile, zinapatikana
wakati wote. “Nitoe wito kwa wadau muhimu wakiwemo Mawakili wa Serikali na
Mawakili wa Kujitegemea, nao kutumia mifumo ya TEHAMA katika kusajili mashauri
na wala wasiwe wao wa kwanza katika kulaumu na kubeza.”
Amesema Mawakili wote wa Serikali na
Kujitegemea, wanapaswa kuwa sehemu ya kutatua changamoto zitakazoibuka katika
matumizi ya mifumo hiyo ya TEHAMA kwa kuwasilisha mapendekezo kuhusu namna bora
ya kuiboresha.
Ameongeza matumizi ya TEHAMA siyo tu
yatawawezesha kutoa huduma kwa wakati, lakini yataweka uwazi ambao
utawapunguzia malalamiko mengi kuhusu watumishi wenu na utoaji haki.
Waziri Mkuu amewataka watumie vema
Wiki ya Sheria kwa ajili ya kutoa elimu ya kutosha kwa wananchi kuhusu
mapinduzi ya matumizi ya TEHAMA yanayoendelea Mahakamani.
Kwa
upande wake,
Jaji Mkuu Profesa Ibrahimu Juma amesema kwa kipindi cha wiki nzima, maonesho ya
Wiki ya Sheria yatafanyika jijini Dodoma pamoja na kwenye Mahaka zote nchini,
kuanzia ngazi ya wilaya.
Pia, Jaji Mkuu ametumia fursa hiyo
kuwakumbusha viongozi wa vijiji, kata, wilaya, mkoa, idara na wizara, wabunge,
majaji, mahakimu na watumishi wa umma wahudhurie maonesho hayo ya Wiki ya
Sheria.
Ametolea mfano banda la maonyesho la
Ofisi ya Mwanasheria Mkuu litawakumbusha kuwa mamlaka yao mihimili mitatu ya
dola yanatokana na nguvu ya sheria, nguvu ambayo haimuonei mwananchi yeyote.
Jaji Mkuu amesema watu watakaoshiriki
katika maonesho hayo kwa kutembelea mabanda watumie nafasi hiyo kujifunza na
kutathmini umuhimu na hadhi ya mfumo wa kimahakama katika kustawisha maisha yao
pamoja na kuwasaidia kupata haki kwa mujibu wa sheria.
Kabla ya kufungua maadhimisho hayo
ambayo kwa mara ya kwanza yamefanyika nje ya jiji la Dar es Salaam, Waziri Mkuu
alishiriki matembezi ya kilomita tano pamoja na Jaji Mkuu na viongozi wengine
yaliyoanzia Mahakama Kuu Dodoma hadi viwanja vya Nyerere Square na kisha
alitembelea mabanda.
IMETOLEWA
NA:
OFISI
YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
41193 – Dodoma,
JUMAMOSI, FEBRUARI 2, 2019.
No comments:
Post a Comment