Habari za Punde

Balozi Seif akutana na Ujumbe wa Mamlaka ya Nyaraka na Makumbusho ya Kitaifa wa Oman

 Mwenyekiti wa Mamlaka ya Nyaraka na Makumbusho ya Kitaifa wa Oman Dr. Hamad Mohamed  Al – Dhawyany akielezea faraja yake kutokana na uhusiano wa muda mrefu uliopo kati ya Oman na Zanzibar  wakati wa mazungumzo yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi.
 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na Ujumbe wa Mamlaka ya Nyaraka na Makumbusho ya Kitaifa wa Oman ukiongozwa na Mwenyekiti wake Dr. Hamad Mohamed  Al – Dhawyany.
 Waziri wa Habari, Utalii na Mambo ya Kale Zanzibar Mheshimikwa Mahmoud Thabit Kombo akitoa taarifa ya maendeleo ya ujenzi wa Jumba la Ajabu Forodhani linalojengwa kwa Ufadhili wa Serikali ya Oman.
 Baadhi ya Viongozi wa Ujumbe wa Mamlaka ya Nyaraka na Makumbusho ya Kitaifa wa Oman ukiendelea na mazungumzo yake na Ujumbe wa Zanzibar ulioongozwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif.
 Balozi Seif akimkabidhi zawadi ya Mlango wa Zanzibar Mwenyekiti wa Mamlaka ya Nyaraka na Makumbusho ya Kitaifa wa Oman Dr. Hamad Mohamed  Al – Dhawyany mara baada ya kumaliza mazungumzo yao.
 Balozi Seif  aliyekaa kati kati kwenye viti akiwa katika picha ya pamoja na Ujumbe wa Mamlaka ya Nyaraka na Makumbusho ya Kitaifa wa Oman pamoja na uke wa Wizara ya Habari, Utalii na Mambo ya Kale Zanzibar.

Picha zote na OMPR

Na Othman Khamis OMPR

Uhusiano wa karibu baina ya Wizara ya Habari, Utalii na Mambo ya Kale Zanzibar na Mamlaka ya Nyaraka na Kumbukumbu za Taifa ya Oman unaendelea kukua kila wakati kufuatia ukaribu uliopo wa Viongozi wa Kitaifa wa Oman na Zanzibar.
Mwenyekiti wa Mamlaka ya Nyaraka na Makumbusho ya Kitaifa wa Oman Dr. Hamad Mohamed  Al – Dhawyany alitoa kauli hiyo akiuongoza Ujumbe wa Viongozi 12 wa Taasisi hiyo wakati wa mazungumzo yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Vuga Mjini Zanzibar.
Dr. Hamad Mohamed  Al – Dhawyany alisema Historia ya kidamu muda mrefu iliyopo kati ya Wananchi wa Zanzibar na Oman inazidi kuongeza ushawishi wa ushirikiano katika nyanja tofauti zinazozidi kuongezeka siku hadi siku.
Alisema uimarishaji wa Jumba la Ajabu Forodhani, Makumbusho ya Kifalme Mizingani pamoja na Magofu ya Kihistoria yaliyopo Mtoni chini ya ufadhili wa Oman utakapokamilika utatoa fursa kwa Wageni na Watalii kutembelea kitendo ambacho mbali ya kuimarisha Historia hiyo muhimu lakini pia kitaongeza mapato ya Taifa.
Dr. Hamad Mohamed  Al – Dhawyany alisema wakati matengenezo ya Jumba la Ajabu Forodhani yakiendelea pamoja na muelekeo wa kulifanyia Matengenezo Jumba la Kifalme Mizingani ukikamilika, Magofu ya Kihistoria yaliyopo Mtoni Ujenzi wake unaweza kuanza wakati wowote kuanzia sasa kwa vite taratibu zote zimeshakamilika.
Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Zanzibar inathamini sana ushirikiano wake na Oman kutokana na Historia ya Wananchi wake walioingiliana kidamu.
Balozi Seif aliendelea kuipongeza Serikali ya Oman Chini ya Kiongozi wake mahiri Mfalme Qaboos Bin Said kwa jitihada inazochukuwa za kuiunga mkono Zanzibar katika harakati zake za kujiletea Maendeleo yaliyolenga kustawisha Maisha ya Wananchi wake.
Alisema Ujio wa Meli ya Kifalme ya Oman katika Visiwa vya Zanzibar Miaka Miwili iliyopita mbali ya Wananchi wa Zanzibar  kufurahia ujio huo lakini pia imeleta baraka kubwa kutokana na mambo makubwa yaliyozaliwa kutokana na ziara ya Meli hiyo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alifahamisha kwamba Matengenezo ya Jumba la Ajabu Forodhani, Jumba ya Kifalme Mizingani pamoja na Magofu ya Kihistoria ya Mtoni ni miongoni mwa mambo yaliyozaliwa kutokana na ziara ya Meli hiyo.
Balozi Seif alieleza kwamba majengo hayo yana heshima kubwa Duniani kutokana na Historia yake inayothaminiwa pia na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni {UNESCO}  na kupelekea Mji Mkongwe za Zanzibar uliobeba Majengo hayo kuingizwa katika urithi wa Kimataifa.
Mapema Waziri wa Habari, Utalii na Mambo ya Kale Zanzibar Mheshimiwa Mahmoud Thabit Kombo alisema hii ni mara ya Pili kwa Ujumbe wa Mamlaka hiyo kutembelea Zanzibar kufuatilia Maendeleo ya Mikataba mbali mbali iliyotiwa saini kati ya Serikali za Oman na Zanzibar.
Mh. Mahmoud alisema yapo mafanikio makubwa ya utekelezaji wa Miradi ya pamoja ya pande hizo mbili akitaja kuwa ni pamoja na Matangenezo ya Beit Al Ajaib Forodhani, Jumba la Kifalme Mizingani pamoja na Majengo ya Kihistoria ya Mtoni.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.