Habari za Punde

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe.Riziki Pembe Juma Amewata Wazazi na Wananchi Kutambua Dhana ya Elimu Bure Kwa Wote.

Akizungumza na wazazi na walezi wa wanafunzi wa Wilaya ya Mkoani katika ukumbi wa Skuli ya Sekondari Muhammed Juma Pindua baada ya kusikiliza maoni yao juu ya namna ya kuleta maendeleo katika Elimu nchini, Mhe Riziki amesema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imeweka dhana hiyo kwa lengo la kuwasaidia watoto walio hali ya chini kuweza kujisomea.
Amesema Serikali imejidhatiti katika kutoa elimu bure kuanzia Maandalizi, Msingi na Sekondari ambapo itaendelea kununua mahitaji ikiwemo Madaftari ya Wanafunzi na ya Mahudhurio, pamoja na chaki.
Amesema suala la kuchangia dakhalia kwa chakula bado lipo palepale lakini Serikali inaendelea kulifanyia utafiti ili kujua namna ya kulitatua suala hilo.
Aidha Mhe Riziki ametoa agizo kwa kamati ya Skuli ya Muhammad Juma Pindua kukaa kikao cha pamoja kujadili namna ya kupunguza gharama ya kulipia dakhalia hiyo ambapo amewataka kutoza gharama isiyozidi elfu 35/- kutoka elfu 50/- waliyokuwa wanalipia hapo awali kuanzia mwezi ujao.
Hata hivyo Mhe Riziki amewahimiza wazazi kuzidisha mashirikiano kati yao na walimu pamoja na kujenga utamaduni wa kuwafuatilia watoto wao Skuli kwa lengo la kujua maendeleo yao kwani hali hiyo itawasaidia kuongeza ufaulu mzuri kwa watoto wao.
Pia amewataka wazazi kusimamia suala la utoro wa watoto wao ambapo amesema Wizara ya Elimu haitamruhusu mwanafunzi yeyote wa ngazi ya Msingi na Sekondari kufanya mitihani yake endapo hawatakuwa na mahudhurio mazuri darasani.
"Mwanfunzi yeyote hataruhusiwa kufanya mtihani ikiwa atakuwa mtoro darasani na ataendelea kubaki darasa hilo hilo huku wenziwe wanaenda darasa jengine mpaka atakapojirekebisha" amesisitiza Mhe Riziki.
Kuhusu vikalio katika Skuli mbalimbali Mhe Riziki amesema Serikali imejitahidi kuchangisha watu mbalimbali kununua vikalio ambapo tayari vimeshaanza kugawiwa katika Skuli, hivyo amewataka wazazi kushirikiana kuvitunza ili viweze kudumu kwa muda mrefu.
Wakitoa michango yao baadhi ya wazazi wameishauri Wizara ya Elimu kulipatia ufumbuzi tatizo la upungufu wa walimu, kupunguza idadi ya masomo kwa ngazi ya msingi, pamoja na kuwafanyia utafiti baadhi ya walimu kwani wengine hawana uwezo wa kufundisha.
Mhe Riziki baada ya mkutano huo wa wazazi alipata nafasi ha kuangalia maendeleo ya ujenzi wa Skuli ya Sekondari Mtambile, Skuli ya Sekondari Mwambe na Skuli ya Sekondari Pujini

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.