Habari za Punde

Masheha watakiwa kuwahamsisha wananchi kushiriki katika zoezi la usafi wa mazingira yao

Wilaya ya Magharibi B.               
Makamo Mwenyekiti wa Kamati ya huduma za Jamii katika Baraza la Manispaa Wilaya ya Magharibi B Thuwaiba Jeni Pandu amewaomba Masheha kuwahamasisha Wananchi kushiriki katika zoezi la kusafisha Mazingira ili  kuepukana na maradhi ya Mripuko hasa katika kipindi hiki cha mvua zinazotarajiwa kunyesha hivi karibuni.
Akizungumza na kamati ya Afya kiongozi Shehia ya Pangawe huko Nyarugusu Wilaya ya Magharibi B amesema Masheha wanawajibu wa kuwakumbusha Wananchi kusafisha mazingira katika maeneo yao.
Amesema baadhi ya Masheha wanashindwa kuwajibika ipasavyo katika kuihamasisha jamii kusafisha mazingira jambo ambalo linasababisha baadhi ya Wananchi kujenga imani ya kuwa jukumu la kusafisha mazingira ni la Serikali na Taasisi zinazohusiana na usafi wa mazingira pekee.
Mh.Thuwaiba ambae pia ni Diwani wa kuteuliwa Wilaya ya Magharibi B amesema tayari bararza la Manispaa katika WIlaya hiyo imeanza mchakato wa kuanzisha Sheria ndogondogo zitakazowaza kuwatia hatiani wanaochafua Mazingira kwa makusudi ili iwe fundisho kwao na wengine wenye nia ya kutenda vitendo kama hivyo.
Amefahamisha kuwa Masheha watakuwa na wajibu mkubwa wa kuzisimamia sheria hizo wakati zitakapokamilika ili kuhakikisha wananchi wanazifuata kwa kusafisha mitaro ya maji machafu kuondosha vichaka na Vidimbi vinavyotuama maji na kusasabisha maradhi ikiwemo ya Malaria.
Kwa upande wake Sheha wa Shehia ya Pangawe Abdallah Juma Mtumweni amesema wameweka mikakati ya kupita zoni hadi zoni kutoa elimu ya kusafisha Mazingira lakini baadhi ya Wananchi wamekuwa wagumu kuifuata elimu hiyo jambo ambalo linaweze kuwavunja moyo na kuwakatisha tamaa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.