Habari za Punde

Shirika la Kimataifa la Nguvu za Atomiki Duniani (IAEA) kushiriiana na Zanzibar katika sekta ya maendeleo
Na Ramadhani Ali – Maelezo Zanzibar.
Mkurugenzi wa Shirika la Kimataifa la Nguvu za Atomiki Duniani (IAEA) Kanda ya  Afrika Profesa Shaukat Abdulrazak amesema Shirika hilo litaongeza ushirikiano na Zanzibar ili kuona linatoa mchango mkubwa zaidi katika kukuza maendeleo ya sekta mbali mbali.
Profesa Shaukat alieleza hayo alipofanya mazungumzo na uongozi wa Wizara ya Afya Zanzibar ulioongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Bi. Asha Ali Abdalla ofisini kwake Mnazimmoja.
Alisema lengo kuu la kufika Zanzibar kwa ziara ya kutwa moja ni kukutana na watendaji wa sekta mbali mbali ili kuwaeleza juu ya nafasi kubwa iliyopo ya kuongeza ushirikiano kwa ajili ya maendeleo ya Zanzibar.
Alisema ushirikiano baina ya Shirika la IAEA na Tanzania ulianza tokea mwaka 1976 na linatoa ufadhili  katika miradi mbalimbali inayohusisha sekta za Afya, Kilimo, Maji, Mifugo, Rasilimaliwatu, Nishati na  Viwanda.
Kwa upande wa Zanzibar Profesa Shaukat alisema Shirika hilo limesaidia katika kupambana na changamoto ya kuteketeza magonjwa yote yanayoambukizwa na Mbung’o na hivi sasa magonjwa hayo sio tatizo kubwa.
Alisema pamoja na kufadhili sekta mbali mbali, Shirika hilo limeweka kipaumbele katika kuwajengea uwezo watendaji kwa kuwapa mafunzo ili kupata uelewa mpana zaidi katika kutekeleza majukumu yao.
Aliweka wazi kuwa Shirika la IAEA limeandaa mpango wa kuimarisha vitengo vinavyoshughulikia maradhi ya Saratani katika Hospitali zinazoshughulikia maradhi hayo baada ya kuonekana yanaongeza kwa kasi katika nchi nyingi zinazoendelea.
Alisema kwa mujibu wa idadi ya Watanzania kunahitajika kuwa na mashine 55 zinazotoa huduma ya mionzi kwa wagonjwa wa Saratani hata hivyo utafiti waliofanya wamegundua zipo mashine tano tu katika Hospitali tatu zinazotoa matibabu hayo ikiwemo Ocean Road na Bugando.
Alisema kuwa mradi wa nguvu za Atomiki Duniani katika Kanda ya Afrika unahusisha nchi 45 ambapo unajikita katika uhusiano wa ushirikiano katika nyanja tofauti.
Mkurugenzi Mkuu Wizara ya Afya Zanzibar Dk. Jamala Adam Taib aliueleza ujumbe huo kuwa Serikali itajenga Hospitali kubwa katika eneo la Binguni na Kitengo maalum cha maradhi ya Saratani kimepewa kipaumbele.
Alilishauri Shirika la IAEA kutoa msukumo zaidi suala la rasilimaliwatu na mafunzo kwa watendaji wa Kitengo cha Saratani ili baada ya kukamilika Hospitali ya Binguni kuwe na nguvukazi ya kutosha.
Akizungumza katika kikao hicho Daktari wa huduma za Saratani Hospitali kuu ya Mnazimmoja Dk. Abdulrahaman Said alisema Kitengo kinachoshughulikia maradhi hayo hivi sasa kina madaktari wawili na wengine watatu wapo masomoni na miaka michache ijayo kitaimarika kufikia madaktari watano.
Alisema hivi sasa Kitengo Saratani kinatoa huduma ya dawa na upasuaji tu kwa vile hawana mashine ya mionzi kwa wagonjwa wa maradhi hayo na hulazimika kwapeleka Hospitali ya Ocean Road Dar es salaam.
Katibu Mkuu Wizara ya Afya Bi. Asha Ali Abdalla alimshukuru Profesa Shaukat Abdulrazak kufika Zanzibar akiambatana na Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania Profesa Lazaro Busagala na kueleza matarajio yake kuwa ziara hiyo italeta manufaa makubwa kwa Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.