Habari za Punde

Wizara ya elimu kuendelea kutekeleza mpango wa elimu kwa ufanisi

Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe Simai Mohamed Said amesema Wizara itaendelea kutekeleza mpango wa Elimu kwa ufanisi ili kutimiza malengo yaliowekwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar chini ya uongozi wa Dk. Ali Mohamed Shein yaweze kufanikiwa.
Akifungua mkutano wa uzinduzi wa miradi ya Elimu itakayoendeshwa kwa mashirikiano na UNESCO katika ukumbi wa Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serika Mazizini, amesema mpango huo utasaidia kukuza kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi na kupata wataalamu waliobora hapa nchini.
Mhe Simai amewataka wadau wote wa Elimu wasichoke kuiunga mkono Wizara hio ili kuleta ufanisi katika uendeshaji wa miradi hiyo ili malengo yaliyowekwa yaweze kufikiwa.
Aidha amelipongeza Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshuhulikia  Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) kwa maamuzi ya busara kwa kuunga mkono utekelezaji wa shuhuli mbalimbali za kielimu Tanzania ikiwemo Zanzibar.
Amesema UNESCO imeandaa miradi mitatu tofauti ambayo yote inapitia Wizara ya Elimu ni "0 3 ambayo inaeleza our Right, our lives and our future", BEAR(Better Education for Africa Rise) na mradi wa tatu ni 'Empowering Girls  and Young Women's Through Education'.
Amefahamisha kuwa miradi hiyo itapelekea vijana, wanawake na watoto wa kike kujitambua na kuandaa watoto wenye kudumisha mila, silka na tamaduni zao ili kuweza kupunguza maambukizi ya HIV.
Nae Naibu Katibu Mkuu utawala mwalim Abdullah Mzee Abdullah amesema mmongonyoko wa maadili ndio chanzo cha ongezeko la ukimwi hivyo UNESCO kuanzisha miradi hiyo itapelekea kulinda utamaduni  kwa ajili ya kizazi chenye maadili mema.
Pia amewaomba washiriki wa mkutano huo kushirikiana pamoja  na kupeana miongozo itakayoweza kufikia malengo yaliokusudiwa katika miradi hiyo na kuondoa migongano ambayo itaweza kuwaharibia malengo yao.
Nae Mwakilishi wa UNESCO Bwana Mathias Herman amesema Shirika lao litaendelea kushirikiana na Serikali  ya Mapinduzi Zanzibar katika kusaidia sekta ya Elimu nchini na kuona watoto wanapatiwa Elimu bora.
Nao washiriki wa mkutano huo wamesema ili kufikia malengo ni lazima kila Skuli iwe na mshauri nasaha  ili kuleta ufanisi wa miradi hiyo.
Mkutano huo wa siku mbili umewashirikisha wakurugenzi mbalimbali wa Wizara ya Elimu, viongozi wa dini na Mashirika ya maendeleo na asasi za kiraia wa shughuli mbalimbali za kielimu hapa Tanzania ikiwemo Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.