Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein, akihutubia wakati wa kufungua Semina ya Kitaifa Kuhusu Masuala ya Ardhi na Rasilimali Zisizorejesheka Zanzibar, iliofanyika katika Ukumbi wa Sheikh Idrissa Abdulwakil Kikwajuni Zanzibar.kushoto Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja Mhe. Ayoub Mohammed Mahmoud na Waziri wa Ardhi Maji Nyumba na Nishati Zanzibar Mhe. Salama Aboud Talib.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.
Ali Mohamed Shein ameeleza kuwa licha ya
kuwepo Sheria tisa zinazohusiana na matumizi bora na endelevu ya ardhi hapa
Zanzibar lakini bado watu hawaziheshimu na hawazifuati.
Dk. Shein aliyasema
hayo leo katika hotuba yake ya ufunguzi wa Semina ya siku moja ya Kitaifa kuhusu masuala ya Ardhi na Rasilimali
zisizorejesheka iliyofanyika katika ukumbi wa Sheikh Idrissa Abdulwakil,
Kikwajuni Mjini Zanzibar ambayo imewahusisha viongozi mbali mbali wakuu wa
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Katika hotuba yake
hiyo, Rais Dk. Shein alisema kuwa kwa lengo la kuhakikisha ardhi ndogo inatumika
vyema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa nyakati mbali mbali imetunga Sheria
tisa kuhusiana na matumizi bora na endelevu ya ardhi ikiwa ni pamoja na kuwepo
wka rasilimali zisizorejesheka kama vile mchanga, mawe, udongo na rasilimali za
misitu lakini hazifuatwi.
Alizitaja baadhi ya Sheria
hizo ni Sheria ya Matumizi ya Ardhi Namba 12 ya mwaka 1992, Sheria ya
Uhaulishaji wa Ardhi Namba 8 ya mwaka 1994 na Sheria ya Mahakama ya Ardhi Namba
7 ya mwaka 1994 ambayo ndiyo inayohusiana na uanzishwaji wa Mahakama ya Ardhi.
Rais Dk. Shein
aliongeza kuwa katika ziara yake aliyoifanya katika Wilaya zote za Unguja na
Pemba kuanzia tarehe 12 Februari hadi tarehe 25 Februari mwaka 2019 ameweza
kufahamu mengi kuhusiana na kadhia ya kuvunjwa kwa sheria mbali mbali
zinazohusiana na matumizi bora ya ardhi.
Aliongeza kuwa kwa
bahati mbaya wavunjaji wa sheria hizo ni viongozi an watendaji wa Serikali na
matukio mengine yanayofanywa na wananchi wa kawaida.
“Taarifa za Wilaya
zilizowasilishwa kwangu zote zimethibitisha kuendelea kuibuka kwa migogoro mipya
ya ardhi katika Wilaya ambazo inatofautiana kwa idadi na kwa aina yake baina ya
Wilaya na Wilaya....Nna taarifa kwamba ipo migogoro ya uvamizi wa maeneo ya
Serikali, ipo migogoro baina ya wananchi na wawekezaji na mingine
kadhaa”,alisema Dk. Shein.
Aidha, Rais Dk. Shein
alisema kuwa jambo jengine ni kuwepo kwa uharibifu mkubwa wa mazingira katika
maeneo yanayochimbwa mchanga aliyoyatembelea ikiwa ni pamoja na kuwepo kwa
upungufu wa mchanga wenyewe.
Alieleza kuwa katika
maeneo aliyoyatembelea katika ziara yake hiyo yakiwemo aneo la Donge Chechele,
Pangatupu na Kiombamvua kwa Unguja na Finya (Selem) na Shumba Viamboni kwa
uapnde wa Pemba amejionea hali halisi ya rasilimali hiyo ya mcvhanga na
kusisitiza kuwa mchanga ni mali ya Serikali hivyo ni mali ya wananchi wote.
Rais Dk. Shein
alisitiza kuwa rasilimali ya mchanga hapa Unguja imepungua kwa kiasi kikubwa na
haipo isipokuwa kuna maeneo sita yenye rasilimali hiyo lakini ni maeneo ya
kilimo ambayo wananchi wanalima mazao mbali mbali ya chakula hivyo kunatakiwa
maamuzi ya kuendelea na na kilimo au kuchimbwe mchanga ambao utachimbwa kwa
wastani wa mwaka mmoja na nusu tu.
Alisema kuwa kwa
upande wa kisiwa cha Pemba tatizo la uhaba wa rasiliamli ya mchanga halipo kwa
hivi sasa lakini kwa Unguja hasa katika maeneneo yanayochimbwa mchanga ya
Pangatupu na Donge Chechele mchanga haupo.
Alieleza kuwa Sheria
ya Usimamizi wa Mazingira Namba 3 ya
mwaka 2015 pamoja na kanuni zake
inafahamisha kwamba mchimbaji mchanga anatakiwa apate kibali, achimbe
kwa kuzingatia kima maalum na ajaze mkataba wa kurejesha eneo ikiwemo kupanda
miti baada ya kumaliziza shughuli za uchimbaji.
Dk. Shein alieleza
kuwa utekelezaji wa Sheria hiyo umekosa usimamizi mzuri na matokeo yake maeneo mengi yaliokwisha kuchimbwa mchanga yamebaki kuwa
ni jangwa na miti iliyopandwa katika maeneo hayo haikustawi na haikunawiri kama ilivyokusudiwa.
Alieleza kwua takwimu
zinaonesha kwamba zipo gari 750 Unguja na gari 165 Pemba zinazochukua mchanga
ambapo gari hizo ni nyingi mno kwa shughuli hio na kati ya gari hizo zipo zenye
uwezo wa kuchukua hadi tani 30 ambazo nazo kwa kipindi kirefu zimekuwa
zikichangia uharibifu wa miundombinu ya barabara.
Hivyo, Rais Dk. Shein
alisema kuwa ameamua kuitisha Semina hiyo ili kwa pamoja viongozi wakae,
wajadili na hatimae wafuate njia bora zaidi ya kupambana na changamoto zilizopo
kwani wao ni viongozi ambao wananchi wamewapa dhamana ya kuwaongoza wakiamini
kwamba kila wakati watakuwa waadilifu, wabunifu na wenye na wenye kufanya
maamuzi yenye kuzingatia maslahi mapana na nchi.
Pamoja na hayo, Rais
Dk. Shein alisisitiza haja ya kufanywa kwa utafiti kama anavyosisitiza mara kwa
mara katika uongozi wake kwa lengo la kukabiliana na changamoto zilizopo katika
utekelezaji wa mipango ya maendeleo.
Alieleza kuwa kwa kutumia
tafiti ndipo itawezekana kuwepo wka mipango imara ya matumizi ya rasilimali
zilizopo sambamba na kwua na mipango na njia mbadala za kutumia pale
inapolazimika kuafnaya hivyo.
Aliongeza kuwa tafiti
ndizo zinazowezesha kutambua vizuri vyanzo na uhalisia wa migogoro ya ardhi na
mambo yanayosababbisha na hatimae kuwa na njia za kisayansi za kutatua “Na sisi
ni lazima tufanye utafiti kwani tunazotaasisi za tafiti na Kila Wiaza ina Idara
inayohusiana na utafiti”,alisisitiza Dk. Shein.
Pamoja na hayo, Rais Dk.
Shein alieleza kuwa mara kadhaa amekuwa akisisitiza juu ya umuhimu wa kuwa na
mipango madhubuti itakayowezesha kutekeleza mipango ya kuimarisha ufukiaji wa
ardhi (Land Reclamation) na kueleza azma ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
ya kufanya ufukiaji huo katika eneo la Gulioni hadi Mpigaduri.
Alieleza kuwa huo ndio
mwelekeo wa nchi nyingi za visiwa hivi sasa kama ni hatua muhimu ya kuongeza
maeneo ya ardhi waliyonayo na kutolea mfano nchi ya Singapore ambayo imeweza
kuongeza eneo la ardhi yake kwa zaidi ya asilimia 24 ikilinganishwa na ukubwa
wa ardhi hio ilivyokuwa mwaka 1960.
“Vile vile Uholanzi,
Umoja wa Falme za Kiarabu na kadhalika nazo zimeongeza eneo la nchi zao kwa
kuifukia bahari”,aliongeza Dk. Shein.
Sambamba na hayo, Dk.
Shein alieleza kuwa mradi mkubwa wa Mtoni Marine uliofanywa na mzalendo Sheikh
Said Salim Bakhressa umedhihirisha kwamba inawezekana kuongeza ukubwa wa eneo
la ardhi iliyopo na ikatumika vizuri katika miradi ya uwekezaji na shughuli
nyengine za kiuchumi na kijamii.
Pia, Rais Dk. Shein
ameeleza jinsi anavyosisitiza ujenzi wa majengo ya ghorofa kwa lengo la kuihami
ardhi ndogo iliyopo.
“Sisi ni viongozi
lazima tuamini kwamba mamo haya yote tunaweza kuyafanya sisi wenyewe hapa
Zanzibar.......kwa hivyo, nyinyi ni wataalamu na viongozi naamini kwamba katika
semina hii, suala la matumizi bora ya ardhi na rasilimali zetu mtalitazama kwa
upana zaidi na kwa kuzingatia maendeleo ya sayansi na teknolojia hivi sasa, ili
nasio nasi tuweze wkenda kwa kasi zaidi”,alisisitiza Rais Dk. Shein.
Mapema Waziri wa
Ardhi, Nyumba, Maji na Nishati Salama Aboud Talib akimkaribisha Rais Dk. Shein
alieleza alieleza kuwa Semina hiyo itasaidia kwa kiasi kikubwa kujua hali
halisi iliyopo juu ya suala zima la ardhi na mali zisizorejesheka hapa Zanzibar.
Katika Semina hiyo
Mada mbali mbali zitatolewa ikiwemo
Sheria Zinazosimamia Matumizi ya Ardhi Zanzibar, Haliya Maendeleo ya Rasilimali
za Misitu na Changamoto zake, Hali Halisi ya Maliasili Zisizorejesheka
Zanzibar, Hali ya Mchanga Zanzibar na Muelekeo wake na hatimae Majumuisho na
Maazimio ya Semina hiyo.
Rajab Mkasaba, Ikulu
Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment