Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein, akizungumza na mgeni wake Mwenyekiti wa Kampuni ya Touchroad Group ya China Ndg,He. Liehui, alipofika Ikulu Zanzibar kwa mazungumzo na Rais wa Zanzibar, kushoto Mwenyekiti wa Bodi ya Utalii Tanzania Mhe. Jaji Thomas Mihayo.Mazungumzo hayo yamefanyika leo 8-3-2019.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameikaribisha Kampuni Touchroad Group kutoka
nchini China kuja kuekeza Zanzibar huku
akiipongeza kwa azma yake ya kuitangaza Zanzibar kiutalii.
Dk. Shein ameikaribisha
Kampuni ya Touchroad Group wakati alipofanya mazungumzo na Mwenyekiti wa
Kampuni hiyo He Liehui yenye Makao Makuu yake mjini Shanghai, nchini China.
Katika mazungumzo hayo,
Dk. Shein aliikaribisha Kampuni hiyo na kumueleza Mwenyekiti wake He Liehui kuwa
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iko tayari kutoa ushirikiano wake mkubwa na
kuweka mazingira mazuri katika kuhakikisha azma ya Kampuni hiyo inafikiwa.
Dk. Shein alieleza kuwa Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar imekuwa na mashirikiano ya muda mrefu na Kampuni
kutoka nchini humo hiyo ni kutokana na uhusiano na ushirikiano wa kihistoria
uliopo kati ya Zanzibar na China.
Alisema kuwa China
imeweza kuiunga mkono Zanzibar na kutoa ushirikiano wake mkubwa katika
kuendeleza na kuimarisha sekta mbali mbali za maendeleo zikiwemo afya, elimu,
kilimo, viwanda, habari, miundombinu na sekta nyenginezo tokea kuasisiwa kwa
Mapinduzi matukufu ya Januari 12, 1964 ambapo ni miaka 55 hivi sasa.
Aidha, Dk. Shein alimuueleza
Mwenyekiti huyo kuwa aliweza kujionea mweyewe hatua iliyofikiwa na Kampuni hiyo
katika shughuli zake za uwekezaji inazozifanya nchini Djibout wakati wa ziara
yake mnamo mwezi Mei mwaka 2017.
Katika ziara hiyo ambapo
Rais Dk. Shein alitembelea maeneo mbali mbali nchini humo yakiwemo yale ambayo
yameekezwa na Kampuni hiyo ikiwemo Bandari ya kisasa ya Djibout na eneo la
Maeneo huru ya Kiuchumi.
Pamoja na hayo, Rais Dk.
Shein alieleza kuwa azma ya Kampuni hiyo ya kuitangaza Zanzibar kiutalii
itasaidia kwa kiasi kikubwa katika jitihada za Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar inazozichukua katika kuitangaza sekta hiyo Kitaifa na Kimataifa.
Aliongeza kuwa
ushirikiano utakaoimarishwa kati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Kampuni
hiyo utasaidia kwa kiasi kikubwa katika kuwaletea maendeleo wananchi wa
Zanzibar hasa ikizingatiwa kuwa uwezo wa Kampuni hiyo ni mkubwa sambamba na
uzoefu ulionao ndani na nje ya Bara la Afrika.
Dk. Shein alitumia fursa
hiyo kuipongeza Kampuni hiyo kwa kuonesha nia ya kutangaza fursa za utalii
zilizopo nchini.
Nae Mwenyekiti wa
Kampuni ya Touchroad Group ya nchini China He Liehui, alipongeza mapokezi
aliyoyapata pamoja na mazungumzo na majadiliano mazuri ya ushirikiano
aliyoyafanywa kati ya Kampuni hiyo na uongozi wa Wizara ya Biashara, Viwanda
pamoja uongozi wa Mamlaka ya Vitega Uchumi Zanzibar.
Aidha, Mwenyekiti huyo
wa Kampuni ya Touchroad alimuhakikishia Rais Dk. Shein kuwa kuna kundi kubwa la
watalii wapatao 10,000 watakaokuja Tanzania mwaka huu wa 2019 ambao wataletwa
na Kampuni hiyo na kusisitiza kuwa atahakikisha wanaitemebela Zanzibar.
Alieleza kuwa kundi hilo
kubwa la watalii kutoka nchini China linalotarajiwa kuwasili kwa awamu katika
mwaka huu mbali ya kuwashirikisha watalii pia watakuwemo wafanyabiashara pamoja
na wawekezaji ambao watafika na Zanziar.
Mwenyekiti huyo
alimuahidi Rais Dk. Shein kuwa kundi la mwanzo la watalii hao linatarajiwa
kuwasili mwezi Mei mwaka huu ambalo litajumuisha watalii wasiopungua 300 ambao
nao wataitemebelea Zanzibar.
Alieleza kuwa Kampuni
yake ina azma ya kuitangaza Zanzibar na kutoa fursa mpya ya kuvitangaza vivutio
viliyopo ili Zanzibar iendelee kuwa kivutio kikubwa cha watalii kutoka nchini
China.
Alisisitiza kuwa Kampuni
hiyo iko tayari kuanzisha usafiri wa moja kwa moja kati ya Zanzibar na China
kwa lengo la kuwaleta watalii kuja kuitembelea Zanzibar na kuagalia vivutio
vilivyopo.
Mwenyekiti huo
alimueleza Rais Dk. Shein jinsi Kampuni yake ilivyopata mafanikio na kuwa
Kampuni iliyoekeza kwa kiasi kikubwa ambayo imeweza kushirikiana na nchi zipatazo
25 za Bara la Afrika zikiwemo Djibout, Afrika Kusini, Nigeria, Zimbabwe,
Botswana na nyengienzo pamoja na kuwa na ofisi katika nchi nane za Afrika.
Mapema Mwenyekiti wa
Bodi ya Utalii Tanzania Jaji Thomas Mihayo alimueleza Rais Dk. Shein kuwa ziara
ya Mwenyekiti huyo wa Kampuni ya Touchroad Group ni sehemu ya utekelezaji wa Makubaliano
yalioingiwa kati ya Tanzania na Kampuni hiyo ya kutangaza vivutio vya utalii
vya Tanzania katika soko la China.
Rajab Mkasaba, Ikulu
Zanzibar
Postal Address:
2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment