Habari za Punde

Tani 15 za mchanga zakamatwa Wete

Na  Masanja     Mabula      Pemba

ZAIDI  ya tani 15 za mchanga uliokuwa katika maandalizi ya kusafirishwa kutoka bonde la Gawani shehia ya Jadida wilaya ya Wete umekamatwa  kufuatia doria zinazofanywa na maafisa wa Wizara ya Kilimo Pemba kwa kushirikiana na serikali ya wilaya.

Akizungumza katika eneo hilo, Mkuu wa Wilaya ya Wete Abeid Juma Ali amesema serikali haitasita kuchukua hatua za kinidhamu kwa mwananchi ambaye atakamatwa akichimba mchanga maeneo yasiyoruhusiwa.

Amesema vitendo vya uchimbaji wa mchanga umewekewa utaratibu maalumu ili kuhakikisha rasilimali hiyo inaendelea kutumika kwa manufaa ya umma.

“Hatuwezi kufumbia macho vitendo hivi, tutahakikisha mhusika akipatikana anachukuliwa hatua za kisheria”alisema.

Afisa mdhamini wizara ya Kilimo, Maliasili, mifugo na Uvuvi Pemba Sihaba Haji Vuai amesema mchanga huo utataifishwa na kuahidi kuendelea kuwatafuta waliohusika na uchimbaji wa mchanga katika eneo hilo.

Amesema licha ya wahusika kutofahamika, lakini Wizara italazimika kuutafisha mchanga huo wakati wanaendela kuwatafuta waliohusika na uharibifu huo.

“Kuanzia leo mchanga huu unakuwa ni mali ya serikali, na wizara kwa kushirikiana na wananchi ili kuhakiksha waliohusika wanapatikana na wanafikishwa mahakamani”alisisitiza.

 Kaimu sheha wa shehia ya Jadida Massoud Msellem Shineni ameitaka jamii kutoa ushirikiano ili wahalifu wanaohujumu rasilimali za nchi waweze kupatikana na kuchukuliwa hatua.

 Tukio hilo limekuja ikiwa ni siku chache baada ya serikali kutangaza maeneo mawili PEMBA katika wilaya ya Micheweni ambayo yatatumika kuchimba mchanga, moja litatumiwa kwa ajili ya ujenzi wa miradi ya serikali na moja kwa ajili ya miradi ya wananchi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.