Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein, akizungumza na Rais wa Shirikisho la Michezo ya Jumuiya ya Madola Bi. Dame Louis Martin, alipofika Ikulu Zanzibar kwa mazungumzo leo.
Na. Abdi Shamna Ikulu. Zanzibar.
RAIS wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, amelipongeza
Shirikisho la Michezo la Jumuiya ya Madola (IOC), kwa kuunga mkono juhudi za
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha michezo mbali mbali nchini.
Dk. Shein ametowa pongezi hizo wakati
alipokutana na Rais wa IOC Dame Louse Martin aliefika Ikulu na ujumbe wake kwa
ajili ya mazungumzo.
Rais huyo wa IOC yupo
Zanzibar kwa ajili ya kuhudhuria mkutano
maalum wa Shirikisho la Michezo
Jumuiya ya Madola (IOC), Kanda ya Afrika ulioanza jana katika hoteli Verde Mtoni
mjini hapa.
Mkutano huo wa siku
tatu unawashirikisha wajumbe kutoka nchi
19 za Afrika, ambapo pamoja na mambo mengine unatathmini maendeleo ya michezo
katika kanda hiyo, ushindani wa kimichezo katika michuano ya Jumuiya ya Madola
pamoja na ushiriki wa Kanda hiyo katika michuano ijayo ya Jumuiya ya Madola itakayofanyika
Birmigham nchini Uingereza, mwaka 2022.
Dk. Shein alisema kwa
miaka kadhaa sasa IOC imekuwa ikiunga mkono kikamilifu juhudi za Serikali katika kuendeleza michezo
mbalimbali nchini kupitia nyanja za kiufundi, mafunzo na rasilimali fedha.
Alisema hatua hiyo
imeiwezesha Zanzibar kupata mafanikio makubwa ya michezo na hivyo kuleta
ushindani mkubwa katika ukanda wa Afrika Mashariki na duniani kwa ujumla.
Alisema Zanzibar ina
historia kubwa ya mafanikio kupitia sekta ya michezo, akitolea mfano wa
ushindani mkubwa uliokuwa ukionyeshwa na wanamichezo wake katika michuano mbali
mbali, ikiwemo ile ya Gossage, iliyokuwa ikizikutanisha nchi za Afrika
Mashariki.
Aidha, aliliomba
Shirikisho hilo kuendelea kuisaidia Zanzibar harakati zake za kuinua michezo,
pamoja na kukiendeleza kizazi kipya
kiliopo ambacho kimebarikiwa kuwa na vijana wengi wenye vipaji.
Nae, Rais wa IOC, Dame
Louse Martin alimhakikishia Dk. Shein azma ya Shirikisho hilo kuendelea kuiunga
mkono Zanzibar katika kuimarisha michezo mbali mbali kupitia nyanja tofauti.
Alisema ameridhishwa sana
na juhudi zinazochukuliwa na viongozi wa
michezo nchini katika kuhakikisha Zanzibar inapiga hatua kubwa za maendeleo
kimichezo na kutajika duniani kote.
Katika ujumbe wake, Rais
huyo wa IOC alifuatana na Makamu wa Rais wa IOC Kanda ya Afrika Miriam Moyo ,
Rais wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC) Gulam Abdalla Rashid pamoja na Katibu
Mkuu wa TOC Filbert Bayi.
.
Abdi Shamna, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777476982. Fax: 024
2231822
E-mail: abdya062@gmail.com
No comments:
Post a Comment