Habari za Punde

Wananchi wa Jimbo la Pangawe Zanzibar Wilaya ya Magharibi B Unguja Wapata Elimu ya Ugatuzi

Na.Takdir Suweid -Maelezo Zanzibar.
Wakaazi wa Jimbo la Pangawe Khamis Juma Maalim ametaka Wakaazi wa Jimbo hilo kutumia fursa zilizomo katika Mfumo wa Madaraka Mikoani (Ugatuzi) ili kurahisisha kuleta maendeleo katika maeneo yao kinyume na hapo zamani kuchaguliwa na Viongozi.
Ameyasema hayo wakati alipokuwa akizungumza katika kikao maalum cha kutoa elimu ya Ugatuzi wa Madaraka na umuhimu wake,kikao ambacho kimefanyika katika kiwanja cha Mpira Nyarugusu Wilaya ya Magharibi B.
Amesema baadhi ya Wakaazi wa Jimbo hilo wanakabiliwa na tatizo la kutoifahamu dhana ya ugatuzi na umuhimu wake hivyo Viongozi wa Jimbo wameamua kupeleka Wataalamu wa fani hiyo ili Wananchi hao wapate uelewa.
Mh.Khamis ambae pia ni Waziri wa Katiba na Sheria amesema hapo awali kulikuwa na Matatizo ya wananchi kutokushirikishwa ipasavyo katika kutatua matatizo ya Msingi yanayowakabili lakini dhana hiyo wataweza kujuwa wajibu wao na kushiriki kutatua matatizo katika sekta ya Elimu ya Msingi,Afya ya Msingi na Kilimo.
Amefahamisha kuwa iwapo Wananchi hawatoshiriki katika Ugatuzi wa Madaraka kupitia Mabaraza ya Wadi na Mashauriano lengo la Serikali kuleta maendeleo kwa haraka halitoweza kufikiwa hivyo amewaomba wananchi kushirikiana katika kuitekeleza dhana hiyo.
Kwa upande wake Diwani wa Wadi ya Pangawe Ameir Pandu Mgana amesema wameamua kutoa elimu hiyo ili Wananchi waweze kujuwa dhana ya Ugatuzi na Umuhimu wake na kuweza kushiriki kutatua matatizo yao kwa haraka kupitia Mabaraza ya Wadi na Mashauriano katika Shehia.
Nao baadhi ya Wakaazi wa Jimbo la Pangawe Wameupongeza uongozi wa Wadi na Jimbo kwa kuanda utaratibu wa kupatiwa elimu hiyo kwani itaweza kuwasaidia katika kujuwa umuhimu na mchango wao katika kuleta maendeleo kupitia Manispaa,Halmashauri na Mabaraza ya Miji.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.