Habari za Punde

Wananchi wa Wanufaika na Mpango wa Kaya Maskini TASAF Zanzibar.

Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Nd. Shaaban Seif Mophamed akizungumza na Wananchi wa Matemwe Kijini kwenye Kituo cha Afya cha kijiji hicho alipokuwa katika zaiara ya kutembelea Miradi ya Tasaf iliyobuniwa kwa Kaya Maskini.
Wa kwanza kutoka Kushoto ni Mkurugenzi Uratibu wa shughuli za serikali SMT, SMZ Khalid Bakar Amrani.

Wananchi wanaonufaika na mpango wa  kunusuru kaya maskini (TASAF) wametakiwa kutunza na kuiendeleza miradi waliobuni na kutekelezwa na serikali ili iendelee kuwahudumia na  kuwanufaisha  mara baada ya kumalizika kwa kipindi cha miradi hiyo.
Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa  Pili wa Rais wa Zanzibar Shaaban Seif Mohamed  alieleza  hayo  wakati alipokuwa katika ziara maalum iliojumuisha Wilaya ya Magharibi “A”na Mkoa wa Kaskazini Unguja kwa lengo la  kukagua miradi hiyo  ya  TASAF  awamu  ya tatu na kusikiliza changamoto zinazowakabili wananchi hao ili  kuzipatia ufumbuzi.
Katibu Mkuu Shaabani  alisema, serikali imekuwa mstari wa mbele katika kuwaanzishia wananchi wake miradi mbali mbali lakini hujitokeza changamoto ya kuilinda na kuendeleza miradi hiyo pale serikali inapoiwacha mikononi mwa wananchi pindi miradi inapofikia ukingoni.
Akikagua kituo cha Afya kilichopo Kianga na Nyumba ya Madaktari iliopo Matamwe Kijini ambavyo vyote vimesaidiwa kupitia Mradi wa TASAF Katibu Mkuu amesema wananchi wanapaswa kuiendeleza miradi hiyo kwa niaba ya serikali na wasisite kuwachukulia hatua endapo watawaona watu wasiokuwa waaminifu wakiharibu miradi yao.
 “Baadhi ya watu hawathamini jitihada za serikali  ambazo zinalenga kuwaletea maendeleo wananchi wake, hivyo hufanya hujuma za makusudi nawaombeni msisite kuwachukulia hatua kwa mujibu wa sheria za nchi” Alieleza Katibu Shaaban.
Katika ziara hiyo  ametembelea mradi wa Kilimo katika bonde la kizimbani bonde ambalo Mpango wa kunusuru kaya maskini umeliendeleza  kwa kuligawa kwa kujenga matuta maalum na kuweka miundombinu ya kupitishia maji kwa vile serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inayoongozwa na Dk. Ali Mohamed Shein itaendeleza jitihada hizo.
Akitolea ufafanuzi suala la baadhi ya watu kutoa upinzani kwa kuwabeza na kuwapuza katika shughuli zao za kilimo alisema serikali italipatia ufumbuzi suala hilo kwa kuendelea kuwaelimisha watu hao ili waachane na vitendo visivyofaa ili lengo la serikali la kuwaletea maendeleo wananchi wake liweze kufikiwa.
Wakulima walionufaika na mradi wa kupunguza Kaya Maskini walimueleza Katibu Mkuu kupitia ziara yake hiyo kuwa, wameishukuru serikali ya mapinduzi kutokana na miradi walioanzishwa imewaletea matunda kwa kupata kipato kinachowasaidia katika kutatua matatizo yanayowakabili.
Pamoja na mambo mengine wananchi hao kupitia katibu mkuu huyo wameiomba serikali kuwapatia vifaa vitakavyowasaidia kuendeleza shughuli zao za kilimo ili waweze kuzalisha za kupata kipato cha ziada.
Akiwa katika kijiji cha Kijini Katibu mkuu Shaaban alipokea changamoto inayolalamikiwa na wananchi hao juu ya kukosekana kwa daktari wa kudumu katika spitali yao licha ya kuchukuwa jitihada ya kujenga nyumba maalum ya kulala daktari pamoja na kuweka miundombinu yote ikiwemo umeme, maji safi na salama.
Wamesema kukosekana kwa daktari wa kulala kijijini hapo kumepelekea wananchi wanapatwa na maradhi nyakati za  usiku kupata usumbufu na kupelekea kutafuta huduma masafa marefu.
Nae Mkurugenzi Uratibu wa shughuli za serikali SMT, SMZ Khalid Bakar Amrani amewaeleza wananchi hao kuwa hivi sasa serikali ipo katika mchakato wa kuwapelekea awamu nyengine ya TASAF.  hivyo amewaomba wananchi kujitokeza kwa wingi kupitia kwa masheha katika shehia zao na kutoa taarifa sahihi zitakazoisaidia serikali kupanga mipango yake.
Ziara hiyo ya Katibu mkuu imejumuisha shehia za Kianga, Kizimbani, Donge mbiji, na matemwe kijini ambapo amepata fursa ya kutembelea miradi ya ujenzi wa Vituo vya Afya na Kilimo iliyobuniwa na wanakaya husika.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.