RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi Alhaj Dk.Ali Mohamed Shein amewataka wananchi kuendelea kuvumiliana,kuheshimiana
na kusaidiana bila ya kujali rangi, kabila wala dini kwa lengo la kudumisha
amani na utulivu uliopo ili kuitekeleza saumu kwa usalama.
Alhaj Dk. Shein aliyasema
hayo katika risala maalum aliyoitoa kwa wananchi kupitia vyombo vya habari
katika kuukaribisha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani katika mwaka huu wa 1440 Hijria
sawa na mwaka 2019 Miladia.
Katika risala yake hiyo,
Alhaj Dk. Shein alisema kuwa kila mmoja ana wajibu wa kuzingatia sheria na kujiepusha na vitendo vyote vinavyoweza
kusababisha kuvunjika kwa amani.
Alhaj Dk. Shein
alisisitiza kuwa zipo baadhi ya nchi ambazo wananchi wake wanaikosa neema hiyo
ya amani kwa nyakati mbali mbali na wanalazimika wafunge wakiwa katika mtihani
wa migogoro ya wenyewe kwa wenyewe isiyokwisha.
“Tunamshukuru Mwenyezi
Mungu kwa kutuwezesha kuukaribisha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani wakati nchi yetu
ikiwa katika hali ya amani na utulivu…….hizi ni miongoni mwa neema nyingine
ambazo Subhana wa Taala ametushushia”,aliongeza Dk. Shein.
Aidha, Dk. Shein alisema
kuwa hizo ni tunu ambazo wananchi wanapaswa kuzitunza kwa sababu mahali
panapokosa amani na utulivu nafsi za watu wake huwa muda wote katika wahka na
taharuki, mambo ambayo yanaondoa unyenyekevu na taqwa katika utekelezaji wa
ibada.
Alieleza kuwa utulivu wa
nafsi unahitajika katika kufanya ibada kwa umakini na pia, unahitajika katika
kutekeleza shughuli nyengine za maendeleo na zile za kujitafutia riziki za kila
siku.
Aliongeza kuwa kwa
mnasaba huo hali ya amani na utulivu ni msingi muhimu unaolazimika kuenziwa na
kuendelezwa kwa nguvu zote.
Pamoja na hayo, Alhaj
Dk. Shein aliwasisitiza waumini wa dini ya Kiislamu kuendeleza wajibu wao kwa
kujiandaa na kutia nia ya kuukabili Mwezi Mtukufu wa Ramadhani kwa kuongeza
jitihada katika uchamungu ili kuweza kunufaika na fadhila za mwezi huo.
“Ni dhahiri kwamba sisi
waja ni watendaji makosa, na baadhi ya wakati huwa tunatenda kwa kujua na mara
nyengine bila ya kujua. Hivyo, jitihada zatu za kufanya ibada kwa wingi katika
mwezi huu zitatupelekea kusamehewa makosa yetu”,alisisitiza Alhaj Dk. Shein.
“Namuomba Mwenyezi Mungu
atuwezeshe kuufunga Mwezi Mtukufu wa Ramadhani kwa salama na atuwezeshe kupata
fadhila za mwezi huu…….Mwenyezi Mungu atupe wasaa wa kuapa riziki za halali na
atufanyia wepesi kwa kila zito ambalo lina heri kwetu”.
“Tunamuomba Mola wetu
atuwezeshe kufanya ibada kwa wingi ili iwe sababu ya kutughufiria makosa yetu
kadhalika kwa barabaka za Mwezi huu Mtukufu wa Ramadhani, tunamuomba awape
maghufira ndugu zetu na wazee wetu waliokwishatangulia mbele ya hahi”, Alhaj
Dk. Shein alimalizia risala yake hiyo.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment