Habari za Punde

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe.Riziki Pembe Juma Akizungumza na Wanafunzi wa Kidatu cha Sita Wanaofanya Mitihani Yao Leo Tanzania Nzima.


Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe. Riziki Pembe Juma akizungumza na Wanafunzi wa Kidatu cha Sita Unguja katika ukumbi wa Skuli ya Sekondari ya Lumumba alipozungumza nao wakati wa matayarisho na kujiandaa kwa mitihani yao ya Taifa ya Kidatu cha Sita inayoaza leo Tanzania Nzima.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Ali Mohamed Shein anawatakia kheri na mafanikio mema  Wanafunzi wote wa Zanzibar na Tanzania Bara wanaotarajiwa kufanya mitihani yao ya kidatu cha sita inayotarajiwa kufanyika Jumatatu ijayo.

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe Riziki Pembe Juma ametoa salamu hizo kwa niaba yake wakati alipozungumza na wanafunzi wa kidatu cha sita wa Skuli ya Sekondari Lumumba Mjini Unguja.

Mhe Riziki amewataka wanafunzi kuhakikisha wanafanya mitihani yao kwa bidii ili kuhakikisha alama ZERO zinatoweka katika matokeo yao.

Amesema kufanya hivyo kutaweza kutimiza ndoto za Wizara ya Elimu katika kuongeza upasishaji na kupata wataalamu waliobora hapa nchini.

Aidha amewataka wanafunzi hao kuwa watulivu wakati wanapofanya mitihani na kujiepusha na udanganyifu ambao utawapelekea kuharibu muelekeo mzima wa maisha yao.

Pia amewataka Wanafunzi kufahamu kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kupitia Rais Dk Ali Mohamed Shein amejitahidi kutafuta nafasi za masomo nje ya nchi kwa lengo la kuwasaidia wanafunzi kujiendeleza na elimu ya juu nje ya nchi kwa lengo la kupata wataalamu zaidi, hivyo amewataka kujitahidi ili kuipata fursa hiyo.

Nae Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe Simai Mohammed Said amewataka wanafunzi hao kutokuwa na hofu wakati wa mitihani yao na kutafakari kwa kina suali kabla ya kujibu pamoja  na kuwataka kumtanguliza mbele Mola wao ili kuwasaidia katika mitihani yao.

Kwa upande wake Mwalim Mkuu wa Skuli ya Sekondari Lumumba Mwalim Mussa Hassan Mussa amesema wamefarajika kuona baadhi ya viongozi na wadau mbalimbali wa Elimu  wamejitolea kuwasaidia futari wanafunzi hao ili waweze kufanya mitihani yao vizuri ambapo amewashukuru na kuwaombea baraka zaidi kwa Allah.

Nao wanafunzi hao wamemuahidi Waziri wa Elimu kuwa watafanya vizuri  Mitihani yao na kuhakikisha nafasi za masomo za nje ya nchi wanazipata ili lengo la Serikali la kupata wataalamu liweze kufikiwa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.