WANANCHI wanaoishi katika maeneo yenye shida ya
maji Zanzibar wamempongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein kwa kutekelezwa vyema agizo alilolitoa kwa
taasisi husika la kupatiwa maji safi na salama katika kipindi hichi cha mwezi
wa Ramadhani.
Katika maelezo yao
wananchi hao walitoa pongezi zao hizo kwa nyakati tofauti kufuatia agizo
alilolitoa Rais Dk. Shein katika risala yake ya kuukaribisha mwezi mtukufu wa
Ramadhani mwaka huu la kupatiwa huduma hiyo muhimu.
Katika risala hiyo Rais
Dk. Shein aliiagiza Wizara ya Ardhi, Nyumba, Maji na Nishati na uongozi wa
Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA) kuhakikisha kuwa ule utaratibu wa kila mwaka wa
kusambaza maji unatekelezwa katika maeneo yenye shida ya maji.
Mbali ya maeneo hayo
pia, Rais Dk. Shein alitoa agizo hilo la kupelekwa huduma hiyo kwa maeneo ambayo
bado huduma za maji safi na salama hazijafika kwa wananchi katika sehemu mbali
mbali za Unguja na Pemba.
Wananchi katika maeneo
hayo walieleza jinsi wanavyopata huduma hiyo vizuri katika kipindi hichi cha
mwezi wa Ramadhani na kueleza jinsi wanavyofarajika kutokana na zoezi hilo
linavyofanywa na Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA) linavyokwenda vizuri.
Wananchi wa maeneo mbali
mbali katika kisiwa cha Unguja na Pemba wameeleza kufarajika kwao na juhudi za
makusudi zinazochukuliwa na Mamlaka ya
Maji (ZAWA) katika kuhakikisha wanapata maji safi na salama katika kipindi
hichi cha mwezi wa Ramadhani.
Wakizungumza kwa nyakati
tofauti na maeneo tofauti hasa katika mji wa Zanzibar wananchi hao walitoa
shukurani na pongezi kwa Rais Dk. Shein kwa agizo lake hilo ambalo walisema
kuwa limesaidia katika kuhakikisha wanapata huduma hiyo muhimu.
Walieleza kuwa huduma
hiyo ni muhimu katika maisha yao hasa katika kipindi hichi cha mwezi wa
Ramadhani ambao mahitaji huwa yanazidi kwa kiasi kikubwa hivyo waliupongeza utamaduni
huo aliouweka Rais Dk. Shein wa kuikumbusha Wizara na Mamlaka yake ya Maji
(ZAWA) kila mwaka inapowadia Ramadhani kuwasogezea karibu zaidi huduma hiyo
wananchi.
“Kuna kila sababu za
kuipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya uongozi wa Rais Dk. Ali
Mohamed Shein kwa agizo lake alilolitoa kwenye taarifa yake ya kuukaribisha
mwezi wa Ramadhani na sisi wananchi tulio na shida ya maji tuletewe maji,
tunampongeza jinsi anavyotujali”, alisema Bi Fatma Khamis mkaazi wa Uroa.
Hivi karibuni, Waziri wa Wizara Ardhi, Nyumba,
Maji na Nishati Salama Aboud Talib akisoma muhtasari wa taarifa ya utekelezaji
wa Mpango Kazi wa Wizara hiyo kwa kipindi cha Julai 2018 hadi Machi 2019
alieleza kuwa Wizara hiyo kupitia Mamlaka ya Maji (ZAWA) imeendelea kusimamia
shughuli za program za uhuishaji na upanuzi wa shughuli za maji mijini na
usambazaji wa maji vijijini.
Aliongeza kuwa katika utekelezaji wa Programu hiyo
Mamlaka ya Maji kupitia mradi wa ADF-12 imeendelea na kazi ya ujenzi wa Tangi
la Saateni katika sehemu ya nne ya nguzo na kufikia asilimia 50 ya ujenzi na
kwa upande wa Tangi la Kilimani Mnara wa Mbao lipo hatua ya jamvi la juu ambapo
ujenzi wake umefikia asilimia 65.
Aidha, alieleza kuwa Mradi huo umefanikiwa kulaza
mabomba kwa masafa ya kilomita 60 katika maeneo ya Bumbwisudi, Kizimbani,
Kianga, Welezo, Mikunguni, Mwembemakumbi, Makadara, Mwembeladu, Rahaleo,
Miembeni na Mkunazini.
Nao uongozi wa Mamlaka
ya Maji Zanzibar (ZAWA), ulieleza juhudi
unazoendelea kuzichukua katika kuwapelekea maji safi na salama wananchi wa
maeneo mbali mbali yakiwemo Uroa, Ndijani, Fukuchani, Michamvi, Jitimai ya
zamani, Kwarara na maeneo mengine kwa upande wa Unguja.
Na kwa upande wa Pemba
ulieleza kuwa miongoni mwa maeneo yanayopelekwa huduma hiyo ni pamoja na Kaskazini
Pemba huko Kwale, Mnyati Gombani ya Kale, Fenewani Shehia ya Kwale Kusini,
Kilimahodi, Kilimani, Mitamani Shehia ya Mfikiwa Mkoa wa Kusuni Pemba na maeneo
mengineyo.
Nao wafanyakazi wa
Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA) walieleza jinsi wanavyopata mashirikiano kutoka
kwa wananchi na kuwapongeza wananchi hao kwa kutekeleza agizo la Rais Dk. Shein
la kuwataka wananchi kwa upande wao kutoa mashirikiano kwa Mamlaka hiyo katika
zoezi hilo.
Katika hotuba zake
anazozitoa Rais Dk. Shein amekuwa akisisitiza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar inaendelea kutekeleza miradi kadhaa ya maji safi na salama kwa lengo
la kuongeza kiwango cha upatikanaji wa maji katika maeneo mbali mbali ya Unguja
na Pemba.
Uwamuzi wa Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar wa kuimarisha huduma za maji safi na salama ni wa busara
na wa msingi katika kuondosha kero zinazowakabili wananchi unaokwenda sambamba
na Malengo ya mwaka 2020 na Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini
nchini (MKUZAIII) pamoja na utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2015-2020
katika kuimarisha huduma za maji safi na salama Zanzibar.
Rajab Mkasaba, Ikulu
Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment