Habari za Punde

Mwakilishi jimbo la Dimani awataka wazazi kuwasimamia watoto ili waongeze bidii ya kudurusu


Na Takdir Suweid

Mwakilishi wa Jimbo la Dimani Dkt.Mwinyihaji Makame Mwadini amewataka Wazazi kuwalea, kuwafuatilia na kusimamia watoto wao ili kuongeza bidii ya kudurusu masomo na kuepuka kufanya vibaya katika Mitihani yao.
Ametoa wito huo huko Skuli ya Msingi Kombeni wakati alipokuwa akifunguwa kikao cha kutathmini matokeo ya Mitihani ya majaribio ya darasa la sita iliofanyika hivi karibuni.
Amesema Matokeo mbaya yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na Wazazi kushindwa kuwahimiza Watoto wao kushughulikia Masomo yao.
Aidha amefahamisha kuwa ili Wanafunzi wafanye vizuri katika Mitihani yao hakuna budi Wazazi kushirikiana na Waalimu katika kuwajengea mbinu bora za usomeshaji kwa Watoto wao.
Hata hivyo Dkt.Mwinyihaji ameahidi kusimamia kambi ya miezi 4 iliobakia kabla ya Wanafunzi kufanya Mitihani ili iweze kukaa pamoja na kudurusu Masomo yao.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Skuli ya Msingi Kombeni Nassor Amir Nassor amewakumbusha Wazee kuwakataza watoto wao kuacha kutumia muda mwingi kuangalia Tv na kuacha masomo jambo ambalo linaweza kusababisha kufanya vibaya Mitihani yao.
Wakitoa michango katika kikao hicho baadhi ya Wanakamati na Wazee wa Skuli hiyo wamewaomba Waalimu kuwaacha Wanafunzi kuchukuwa Vitabu Majumbani ili wapate kudurusu Masomo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.