Habari za Punde

Naibu Waziri wa Maliasi na Utalii Mhe. Constantine Kanyasu Awaonya Wananchi Wanaotoa Vitisho Kwa Askari Wanyamapori wa Vijiji

Naibu Waziri wa  Maliasili na  Utalii, Mhe. Constantine Kanyasu, akizungumza  na wahitimu wakati  akifunga mafunzo ya Askari  20 wa  Wanyamapori wa Vijiji  wa kutoka mikoa ya Ruvuma, Mbeya na Singida waliohitimu mafunzo hayo  katika Chuo cha Mafunzo ya Uhifadhi wa Maliasili kwa Jamii cha Likuyu Sekamaganga kilichopo katika wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma 
Naibu Waziri wa  Maliasili na  Utalii, Mhe. Constantine Kanyasu akizungmza na  Mkuu wa  Chuo cha Mafunzo ya Uhifadhi wa Maliasili kwa Jamii cha Likuyu Sekamaganga, Jane Nyau huku  akiangalia mnara mpya uliowekwa na TTCL kwa ajili ya huduma za mtandao katika chuo hicho mara baada ya kuwasili kwa ajili ya kufunga mafunzo ya askari 20 wa wanyamapori wa vijiji katika wilya ya Namtumbo mkoani Ruvuma. Katikati ni Mkuu wa wilaya ya Namtumbo, Sophia Mfaume pamoja na viongozi wengine 
Naibu Waziri wa  Maliasili na  Utalii, Mhe. Constantine Kanyasu akikagua paredi  kwa Askari  20 wa  Wanyamapori wa Vijiji  wa kutoka mikoa ya Ruvuma, Mbeya na Singida wakati akifunga  mafunzo kwa  wahitimu wa mafunzo hayo  katika Chuo cha Mafunzo ya Uhifadhi wa Maliasili kwa Jamii cha Likuyu Sekamaganga kilichopo katika wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma Ruvuma
Baadhi ya Askari wa wanyamapori wa Jamii wakiwa wanamsikiliza  Naibu Waziri wa  Maliasili na  Utalii, Mhe. Constantine Kanyasu wakati akizungumza nao katika mahafali ya kufuzu mafunzo yao katika Chuo cha Mafunzo ya Uhifadhi wa Maliasili cha Likuyu Sekamaganga,

Mkuu wa chuo Chuo cha Mafunzo ya Uhifadhi wa Maliasili cha Likuyu Sekamaganga akizungumza wakati wa mahafali ya kufuzu kwa Askari wanyamapori wa Jamii mkoani Ruvuma.
 (Picha na Lusungu Helela - WMU)

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.Constantine Kanyasu amewataka Wananchi waache tabia ya kuwatishia maisha  Askari wanyamapori wa vijiji  (VGS) wakati wanapowakataza wananchi hao kuendesha shughuli za kibinadamu katika maeneo ya mtawanyiko na mapito ya wanyamapori (shoroba)

Kufuatia hali hiyo, Mhe.Kanyasu amemtaka Mkuu wa wilaya ya Namtumbo,  Mhe. Sophia Mfaume afanye uchunguzi kwa kutumia vyombo vyake vya usalama ili kuwabaini Wananchi hao wanaowatishia Askari  wanapotekeleza majukumu yao  na watakaobainika hatua kali za kisheria zichukuliwe dhidi yao.


Mhe. Kanyasu, ameyasema hayo wakati alipokuwa akifunga mafunzo ya Askari  20 wa  Wanyamapori wa Vijiji  wa kutoka mikoa ya Ruvuma, Mbeya na Singida waliohitimu mafunzo hayo  katika Chuo cha Mafunzo ya Uhifadhi wa Maliasili kwa Jamii cha Likuyu Sekamaganga kilichopo katika wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma

“leo mmehitimu na tumewaapisha, mmekuwa askari kweli  lakini tambueni kuwa kazi za kiuchumi zinapelekea uharibifu mkubwa sana wa mapito ya wanyama, nendeni mkawaelimishe wananchi wasiendelee kuharibu kwa ustawi wa hifadhi zetu"

Amefafanua kuwa  maeneo ya mtawanyiko na shoroba lazima zilindwe ili kuruhusu wanyamapori waendelee  kuzaliana  na pia kwenda  kupata virutubisho maalum ambayo havipo mbugani.

''Tunazihitaji hizi shoroba, tulikuwa tumejisahau shoroba nyingi zimekuwa mashamba na makazi na wanyama wamekuwa hawana sehemu ya kupita'' amesema Kanyasu

Amesema shoroba na maeneo ya mtawanyiko zisipokuwepo utalii na Hifadhi vitatoweka.

"Lazima tufike mahali tuamue eneo hili ni kwa ajili ya kilimo na eneo hili kwa ajili ya makazi, haiwezekani maeneo yote tukaanzisha kilimo na makazi ilhali wanyamapori hawana mipaka" Alisisitiza Kanyasu .

Amesema uwepo wa shoroba na maeneo ya mtawanyiko husaidia  kupata kizazi imara cha wanyamapori kwani wakifungiwa sehemu moja huzaliana ndugu na kukosa ubora,ikiwamo kuwa rahisi kushambuliwa na magonjwa.

Katika hatua nyingine, Mhe.Kanyasu amewataka askari hao kufanya kazi kwa uaminifu kwa kujiepusha kuungana na mtandao wa majangili.


Kwa upande wake, Mkuu wa wilaya ya Namtumbo, Mhe. Sophia Mfaume amewahakikishia askari hao kuwa wafanye kazi kwa kufuta sheria na wale watakaowakwamisha  katika kutekeleza majukumu yao hatasita kuwachukulia sheria.

Aidha, Amewataka Wananchi wafuate sheria kwa kuheshimu maeneo ya mtawanyiko na shoroba ili Hifadhi ziendelee kuwepo

Kwa upande wake, Mhitimu wa mafunzo hayo Musa Alfred Wakati akisoma risala, Amemueleza Naibu Waziri kuwa mafunzo waliyopewa yatakuwa chachu katika shughuli za uhifadhi nchini.

Naye Mbunge wa viti maalum wa mkoa wa Ruvuma, Jaqueline Msongozi amewataka askari hao wa vijiji watekeleze majukumu yao bila kutishwa na mtu yeyote kwa vile maliasili hizo ni za watanzania wote na wao wanazilinda kwa niaba ya Watanzania.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.