Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein, Ahutubia Baraza la Eid Fitry Zanzibar

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein, akihufubia Baraza la Eid Fitry katika ukumbi wa Sheikh Idrissa Abdulwakil Kikwajuni Zanzibar leo, baada ya kumalizika kwa Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.


RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Ali Mohamed Shein amewanasihi wananchi kutii sheria za nchi ili wageni wanaoitembelea Zanzibar nao waweze kuiga mfano wao na hatimae waendelee kuishi kwa hali ya salama na amani. 


Alhaj Dk. Shein aliyasema hayo leo katika hotuba yake aliyoitoa katika Baraza la Idd El Fitri kwenye ukumbi wa Sheikh Idrissa Abdulwakil, Kikwajuni mjini Zanzibar hafla ambayo imehudhuriwa na viongozi mbali mbali wa vyama vya siasa na Serikali akiwemo Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd, Mabalozi Wadogo waliopo Zanzibar na wananchi. 

Katika hafla hiyo, ambapo Mama Mwanamwema Shein nae alihudhuria, Dk. Shein alieleza kuwa kuwepo kwa amani na utulivu nchini kumzidisha kupiga hatua za ufanisi za utekelezaji wa mipango mikuu ya maendeleo ambayo ni MKUZA III, Dira ya Maenedeleo ya 2020, Mpango wa Dunia wa Maendeleo Endelevu na Ilani ya Uchaguzi Mkuu ya CCM ya mwaka 2015-2020.

Rais Dk. Shein alisema kuwa nchi inayothamini na kufuata misingi ya utawala bora watu wake huwa na uvumilivu maalum wa kuishi pamoja katika jamii yenye watu wenye imani tafauti za kidini na kiutamaduni.

Aliongeza kuwa watu wa Zanzibar na Watanzania kwa ujumla wamekuwa ni kigezo kizuri miongoni mwa nchi kadhaa duniani katika kuuendeleza ustaarabu huo wa uvumilivu tangu hapo kale na dahari.

 “Kwa hakika uvumilivu ni miongoni mwa sababu zinazotuepusha na migogoro ya wenyewe kwa wenyewe nchini. Tumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupa tunu hii, tutahakikisha kwamba tunailinda amani na usalama nchini mwetu kwa kila hali”alisema Alhaj Dk. Shein.

Aidha, alisisitiza kuwa wananchi wa Zanzibar wanawajibu wa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuwajaalia kuwa na uchumi unaokuwa mwaka hadi mwaka ambapo katika mwaka wa fedha 2018 uchumi ulikuwa kwa asilimia 7.1 kutoka 7.0 na mfumko wa bei uliendelea kushuka kutoka kasi ya asilimia 5.6 mwaka 2017 hadi kufikia asilimia 3.9 mwaka 2018.

Alieleza kuwa katika kuimariska kwa uchumi makusanyo ya mapato yameongezeka na kufikia TZS bilioni 6668.70 mwaka 2017/2018 kutoka TZS bilioni 181.48 mwaka 2010/2011 ambayo ni sawa na ongezeko la mara 3.7.

Dk. Shein alisema kuwa pato la mtu binafsi ambalo lilikuwa TZS 942,000 mwaka 2010, limeongezeka na kufikia TZS 2,323,00O mwaka 2018 ikiwa ni sawa na ongezeko la asilimia 146.7.

Hivyo, alisema kuwa makusanyo na utekelezaji wa mipango ya maendeleo inaleta matarajio ya kukua kwa uchumi kufikia asilimia 7.8 katika mwaka wa fedha wa 2019/2020 na hapana shaka kwamba Zanzibar itafikia nchi yenye uchumi wa kati ifikapo mwaka 2020 kama ilivyolengwa katika Dira ya Maendeleo ya Zanzibar ya 2020.

Pamoja na hayo, Alhaj Dk. Shein alieleza kuwa Serikali haina uwezo wa kumpa kila mtu mmoja pesa za matumizi katika kuendeleshea maisha yake ila humlipa kupitia huduma mbali mbali zinazotoa kwa wananchi.

Kwa hivyo, kila kiongozi kwa nafasi aliyo nayo itamlazimu asimamie suala la ulipaji kodi pamoja na utoaji wa risiti na kuwataka wananchi kuendelea kushajiishana juu ya utoaji na uchukuaji wa risiti ili kuhakikisha kwamba kila senti inayolipaswa kukusanywa na Serikali inakusanywa.

Alitoa wito kwa wafanyabiashara watambue umuhimu wa kutoa risiti zilizohalali katika biashara zao na kulipa kodi kwa mujibu wa sheria kwani ni dhahiri kuwa sehemu kubwa ya mapato ya nchi yanatokana na kodi.

Dk. Shein alisema kuwa Serikali imeridhika na kiwango cha uwajibikaji kilichooneshwa na Wizara zote na Taasisi zake katika kutumia fedha zilizoidhinishwa na Wizara zote na Taasisi zake katika kutumia fedha zilizoidhinishwa na Baraza la Wawakilishi kwa mujibu wa sheria na taratibu za matumizi zilizopo.

Kwa mnasaba huo, Rais Dk. Shein ametoa pongezi kwa Mawaziri, Manaibu Mawaziri, Watendaji na Watumishi wote wa Serikali na Taasisi zake kwa mafanikio hayo na ufanisi unaoendelea kupatikana katika kukuza uchumi, kuimarisha huduma za wananchi na kuwapatia huduma mbali mbali kwa ufanisi.

Alhaj Dk. Shein aliwaeleza wananchi kuwa mafanikio yameanza kupatikana katika kuimarisha huduma za sekta zilizogatuliwa katika kuwatumikia wananchi na changamoto zinazojitokeza katika kipindi hichi cha mpito zikiwemo uhaba wa baadhi ya wataalamu, ufinyu wa nafasi za ofisi za kufanyia kazi, nyenzo za kufanyia kazi na mambo mengineyo zisiwe sababu ya kuona mfumo wa ugatuzi haufai.

Alisema kuwa Serikali inaendelea na jitihada zake za kuifanyia kazi changamoto inayoendelea kuwakabili wananchi ya uharibifu wa miundombinu ya barabara pamoja na madaraja katika mzimu wa mvua.

Dk. Shein alitoa pongezi kwa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji kwa kutekeleza agizo alilowapa la kulitafutia ufumbuzi wa kudumu tatizo la maji la Kibonde Mzungu kwa kujenga daraja la kisasa na kuiagiza kuendelea na kazi ya kuiunganisha barabara ya Fuoni kutoka kwenye kituo cha Polisi hadi Kibonde Mzungu huku akitoa pole kwa wananchi wote waliopata athari kutokana na mvua za masika.

Alisema kuwa katika jitihada za kuimarisha miundombinu ya barabara, Serikali imenunua mtambo wa lami wa kisasa pamoja na kuagiza zana na vifaa vya kisasa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa barabara pamoja na ukarabati wa baadhi ya barabara za Unguja na Pemba vyote vikiwa na thamani ya TZS Bilioni 14.8.

Sambamba na hayo, alitoa shukurani kwa uongozi na wafanyakazi wa Wizara ya Ardhi, Nyumba, Maji na Nishati na Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA) kwa kuwapatia huduma ya maji wananchi ambao huduma hiyo hawaipati vyema katika maeneo yao.

Alitoa shukurani kwa vyombo vya Ulinzi na Usalama kwa ajili ya kusimamia ulinzi wa nchi katika maeneo yote, kusimamia hali ya usalama wa wananchi na kukabiliana na madereza wanaovunja sheria za usalama barabarani.

Alhaj Dk. Shein aliwaombea kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu kuwapa afya njema, Waislamu wanaokwenda kutekeleza Ibada ya Hijja huko Saudi Arabia mwaka huu ili waweze kuitekeleza vyema ibada hiyo.

Alisisitiza kuwa ili ufanisi upatikane katika maendeleo ya jamii ni vyema wananchi wakaendelea na mwenendo mzuri wa kutafuta radhi za Allah hata katika miezi mingine baada ya kumaliza kwa mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

Aliwasihi Mashekhe na Walimu waendelee kutoa mawaidha juu ya umuhimu wa kuyaheshimu maamrisho ya Mwenyezi Mungu kwa kufuata mwenendo wa maadili mema na kubainisha madhara ya kuhalifu maarisho ya Mola.

Akitoa tafsiri na maelezo mafupi ya Aya za Qur-an tukufu Surat Muuminuna kuanzia Aya ya 1 hadi ya 11, Sheikh Abdallah Hamid Suleiman kutoka Chuo Cha Kiislamu alisisitiza haja ya umoja na mshikamano kwa waumini wa dini ya Kiislamu na wananchi wote sambamba na kukemea vitendo viovu na kufanya mambo mema na kuyafuata maarisho ya Mwenyezi Mungu.

Mapema, Rais Dk. Shein aliungana na wananchi pamoja na viongozi mbali mbali wa Dini na Serikali katika sala ya  Idd El Fitri iliyosaliwa katika viwanja vya Maisara, mjini Zanzibar ambapo katika hotuba ya sala hiyo waislamu walisisitizwa kuimarisha umoja na kuendeleza amani iliyopo sambamba na kufuata mafunzo ya mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Baada ya hapo Rais Dk. Shein alifika Ikulu mjini Zanzibar na kupata fursa ya kusalimiana na viongozi wa Dini ya Kiislamu na baadae aliwapa wananchi waliofika katika viwanja vya Ikulu mjini Zanzibar skukuu yao ya Idd El Fitri kama ilivyo kawaida yake kwa miaka yote kila ifikapo siku hii.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822  

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.