Habari za Punde

Waziri Aboud Atembelea Eneo Mbadala la Kuzikia Watu Katika Kijiji cha Kama Wilaya ya Magharibi A Unguja


 Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Mohamed Aboud Mohamed Kati kati pamoja na Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi yake Nd. Abdulla Hassan Mitawi kulia yake na Mkurugenzi Mkuu wa Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar Nd. Makame Khatib wakilikagua eneo hilo. Baadhi ya Makaburi ya Watu waliokufa kutokana na Maafa ya kuzama kwa Meli za M.V Spice Islander na M.V Skagit yaliyopo katika Kijiji cha Kama Wilaya ya Magharibi “A”.
Mkurugenzi Mkuu wa Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar Nd. Makame Khatibu Makame akifafanua jambo wakati wa ziara ya Waziri Aboud kulikagua eneo la Makaburi la Kama.Picha na – OMPR – ZNZ.
Na.Othman Khamis OMPR.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Mohamed Aboud Mohamed amefanya ziara ya kulikagua eneo mbadala la kuzikia Watu liliyopo katika Kijiji cha Kama Wilaya ya Magharibi “A”.
Eneo hilo la Makaburi ya Watu waliofariki kutokana na Maafa ya kuzama kwa Meli ya M.V. Spice Islander mnamo Tarehe 10 Septemba Mwaka 2011 na M.V Skagit Mnamo Tarehe 18 Julai Mwaka 2012 limetengwa maalum kufuatia lile lililozoeleka la Mwanakwerekwe kujaa Makaburi.
Mh. Mohamed Aboud Mohamed akiambatana na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Nd. Abdullah Hassan Mitawi alisema Uongozi wa Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar unapaswa kusimamia usafishaji wa eneo hilo pamoja na kukamilisha kazi zilizobakia.
Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar tayari imeshatoa maelekezo ya kutumiwa eneo hilo la kama kwa vile Mwanakwerekwe hivi sasa kumekuwa na msongamano mkubwa wa Makaburi hali inayoweza kusababisha baadae kuharibika kwa yale yaliyopo.
Waziri Aboud hata hivyo alifahamisha kwamba bado upo umuhimu wa mahitaji ya kuongezwa kwa ukubwa zaidi wa eneo la kuzikia ili liweze kukidhi mahitaji kwa kipindi kirefu kama ilivyokuwa Mwanakwerekwe.
Mapema Mkurugenzi Mkuu wa Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar Nd. Makame Khatibu Makame alisema eneo hilo tayari limeshatumika kuzikiwa Watu 80 waliokufa kutokana na Maafa ya kuzama kwa Meli za M.V Spice Islander na M.V Skagit.
Ndugu Makame alisema uzikwaji wa Watu hao ambao wapo waliotambuliwa na jamaa zao na kutoa idhini pamoja na wale wasiotambulika umefanywa kwa kuzingatia tofauti ya Imani za Dini zao.
Mkurugenzi Mkuu huyo wa Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar alifahamisha kwamba katika kukamilisha vyema eneo hilo yapo mambo ya muhimu yanayostahiki kujengwa kama Msikiti na sehemu ya kuoshea Maiti.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.