Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza ,la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein, Awatumia Salamu za Pongezi Rais wa Rwanda. Mhe.Paul Kagame na Rais wa Burundi Mhe. Pierre Mkurunziza Kwa Kutimiza Miaka 57 ya Uhuru.


RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amewatumia salamu za pongezi Rais wa Rwanda Paul Kagame na Rais wa Burundi Pierre Nkurunziza kwa kutimiza miaka 57 ya Uhuru wa Mataifa hayo.

Katika salamu ambazo Rais Dk. Shein amemtumia Rais wa Rwanda Paul Kagame zilieleza kuwa kwa niaba ya wananchi wa Zanzibar wanaungana pamoja na ndugu zao wa Rawanda katika kusherehekea siku hii muhimu katika historia ya Taifa hilo.

Salamu hizo zilipompongeza Rais Kagame kwa jitihada kubwa alizozichukua katika kukuza na kuimarisha uchumi wa nchi hiyo sambamba na kuimarika kwa mshikamano wa wananchi wa Taifa hilo.

Aidha, salamu hizo, zilieleza kuwa tukio hilo kubwa, linatoa nafasi ya kuendeleza uhusiano na ushirikiano mkubwa kati ya pande mbili hizo pamoja na wananchi wake hatua ambayo itaimarisha zaidi uhusiano katika nyanja za Kitaifa na Kimataifa yakiwemo mashirikiano katika Jumuiya yao ya nchi za Afrika Mashariki (EAC).

Sambamba na hayo, Dk. Shein alimtakia kiongozi huyo pamoja na familia yake na wananchi wote wa Rwanda, afya njema na kuwatakia sherehe njema zenye amani na utulivu wananchi wa nchi hiyo.

Wakati huo huo, Rais Dk. Shein pia, alitumia salamu hizo za pongezi Rais wa Burundi Pierre Nkurunziza kwa kutimiza miaka 57 ya Uhuru wa Taifa hilo na kueleza kuwa wananchi wa Zanzibar kwa niaba yake wanaungana na ndugu zao wa Burundi katika kusherehekea uhuru wa Taifa hilo.

Salamu hizo zilieleza historia na uhusiano sambamba na mashirikiano yaliopo kati ya Zanzibar, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Burundi na kueleza jinsi inavyojivunia mafanikio yaliopatikana nchini Burundi tokea kupatikana kwa uhuru wake.
Aidha, salamu hizo zilieleza kuwa hatua hiyo ni bahati kubwa inayoashiria mashirikiano na mahusiano mema ya kidugu kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki (EAC).

Katika salamu hizo, Rais Dk. Shein pia, alimtakia kiongozi huyo pamoja na familia yake na wananchi wote wa Burundi, afya njema na kuwatakia wananchi wa hiyo kusherehekea kwa  amani na utulivu siku hii adhimu na ya kihistoria ya nchi hiyo.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.