Habari za Punde

Udhibiti Mapato Nidhamu Kwa Watumishi Vimepaisha Uchumin -Mhe.Majaliwa.


Waziri Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Kassim Majaliwa amesema hatua ya kudhibiti upotevu wa mapato na matumizi ya fedha za Serikali, uboreshwaji wa mazingira ya biashara na uwekezaji pamoja na kusimamia uwajibikaji kwa watumishi wa umma kumesababisha kukua kwa uchumi.

Amesema Tanzania ni nchi yenye amani na utulivu na Serikali imeendelea kuongeza nguvu katika kudumisha amani na utulivu kwenye maeneo yote nchini, hali inayotoa fursa kwa wananchi wake kuendeleza shughuli zao za maendeleo. 

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumatatu, Julai 8, 2019) wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu wa Misri, Dkt. Mostafa Madbouly akiwa katika siku yake ya kwanza ya ziara yake ya kikazi nchini Misri.

Hivyo, amemuhakikishia Waziri Mkuu wa Misri kwamba Serikali ya Tanzanzia na wananchi wake wapo tayari kuendelea kushirikiana na Serikali ya nchi hiyo na wananchi wake katika kuchochea ukuaji wa uchumi wa nchi hizo mbili.

Amesema nchi za Tanzania na Misri zinahitaji kutumia nafasi ya ushirikiano wa kibiashara na uwekezaji katika ukuzaji wa uchumi, hivyo Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwakaribisha wawekezaji na wafanyabiashara kutoka Misri waje kuwekeza nchini.

Amesema Serikali ya Tanzania imefanikiwa kiuchumi na kwa sasa ni nchi pili ambayo uchumi wake unakua kwa kasi barani Afrika, ikitanguliwa na nchi ya Ivory Coast. Uchumi wa Tanzania ulitarajiwa kukua kwa asilimia 7.2 mwaka jana kutoka asilimia saba.

“Hali ya uchumi wa Tanzania inaendelea vizuri, tumeendelea kushuhudia kushuka kwa mfumuko wa bei ambapo kwa sasa tumefikia asilimia 3.2, kiwango hiki ni matokeo ya kukuza sekta za madini, ujenzi, mawasiliano, utalii pamoja na kushuka kwa bidhaa za chakula na mafuta. Tunatarajia kiwango hiki kitashuka zaidi kwa sababu ya uwekezaji.”

Waziri Mkuu amesema Serikali ya Awamu ya Tano tangu ilipoingia madarakani mwaka 2015, kipaumbele chake kilikuwa ni kukuza kiwango cha uchumi kutoka cha chini kwenda cha kati ifikapo mwaka 2025 kupitia sekta ya viwanda.

 IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATATU, JULAI 8, 2019.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.