Mtendaji Mkuu Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS),
Mhandisi Patrick Mfugale akisaini Mkataba wa ujenzi wa Daraja la Kigongo-Busisi
mkoani Mwanza na Mwakilishi kutoka kampuni ya
ujenzi ya China Civil Engeering Construction
Coorporation,
Zhang Jang, katika hafla iliyofanyika Makao makuu ya Mamlaka ya Bandari
Tanzania TPA, Jijini Dar es Salaam, wanaoshuhudia ni Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi
na Mawasiliano Mhandisi Isack Kamwelwe
na Waziri wa TAMISEMI, Selemani Jaffo.
Mtendaji Mkuu Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS),
Mhandisi Patrick Mfugale na Mwakilishi kutoka kampuni ya ujenzi ya China Civil Engeering Construction
Coorporation,
Zhang Jang, wakionesha nakala za mkataba wa ujenzi wa Daraja la Kigongo- Busisi
mara baada ya kusainiwa, ujenzi wake utagharimu TZS. Bilioni 592.
(Picha Idara ya Habari-MAELEZO).
Na.Mwandishi Wetu –MAELEZO.
Hatimaye historia imeandikwa
nchini Tanzania kwa kusainiwa kwa mkataba wa ujenzi wa daraja la Kigongo Busisi
katika Ziwa Victoria mkoani Mwanza lenye urefu wa kilometa 3.2, ambao
utagharimu jumla ya fedha za kitanzania Bilioni 592.
Akizungumza Jijini Dar es Salaam
katika hafla ya utiaji saini mkataba wa ujenzi wa daraja hilo, Waziri wa Ujenzi
Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Isaac Kamwelwe, amesema mradi huo utatekelezwa
kwa fedha za walipa kodi wa Tanzania bila kutegemea fedha za wafadhili.
Waziri Kamwelwe alisema mradi wa
Kigongo Busisi kama ilivyo miradi mingine ya kimkakati ulipigwa vita sana na
baadhi ya watanzania na hata wahisani, amesema hata baadhi ya wanasiasa waliupinga
wakidai ni mradi mkubwa sana kwa taifa na hauna tija kwa wakazi wa maeneo hayo
na nchi kwa ujumla.
“Serikali hii ikiamua jambo
inalivalia njuga na inahakikisha linakamilika kwelikweli , huu ni mkonga wetu watanzania
na haijawahi hata siku moja mkonga ukamshinda tembo hivyo tunafanya na
tutafanikiwa kwa sababu tunatumia fedha zetu wenyewe ili hao waliotukatisha
tamaa washangae ” Alisema Waziri Kamwelwe.
Amesemakuwa ni wakati sasa kwa
watanzania kutembea kifua mbele kwani sasa kodi zao zinatumika ipasavyo katika
kuwaletea maendeleo, ndio maana mradi huo mkubwa unaanza kutekelezwa, sambamba
na miradi mingine kama ya umeme wa mto Rufiji pamoja na kuendelea kununua ndege
mpya ili kuimarisha shirika la ndege.
Amesema wahisani wengi walikuwa
na masharti kwamba wakikuletea fedha wanakuletea na mkandarasi wao, hivyo
amesema kwa Tanzania ya sasa haitakubalika kwani kuna mgawanyo wa majukumu na
wataalam wa mikataba, kuna wataalam wa manunuzi na hata washauri katika miradi
mbalimbali hivyo serikali iko makini sana hasa katika masuala ya mikataba ili
wasiingie mikataba ambayo itakuja kuwa kifungo kwa watanzania.
Waziri Kamwelwe amesema wakati wa
ujenzi wa daraja kutakuwa na ajira za kudumu zaidi ya elfu moja na ajira zisizo
za kudumu zaidi ya elfu kumi, kwakua fedha ni za watanzania ni wajibu wa
serikali kuhakikisha fedha zinawanufaisha watanzania.
Hafla ya utiaji saini mkataba wa
Ujenzi wa Daraja la Kigongo Busisi ulihudhuriwa pia na Waziri wa nchi
Ofisi ya Rais TAMISEMI Suleiman Jaffo , wakuu wa mikoa ya Mwanza na
Geita, wabunge kutoka katika mikoa hiyo pamoja na baadhi ya wajumbe wa kamati
ya Kudumu ya Bunge ya miundombinu.
Ujenzi wa daraja hilo
unatekelezwa na kampuni ya China Civil Engineering Construction Cooperation kwa kushirikiana na kampuni ya
China Railway 15 Bureau Group , na linatarajiwa kuwa na urefu wa kilometa 3.2
pamoja na barabara zenye urefu wa kilometa 1.66. mkoa wa Mwanza.
Utiaji saini huo ulifanywa na
Mhandisi Patrick Mfugale Mtendaji Mkuu wa Tanroads kwa niaba ya Serikali ya
Tanzania na Bw.Zhan Jang kwa niaba ya makampuni ya China Civil Engineering Cooperation na China
Railway 15 Bureau Group.
No comments:
Post a Comment