Na Khadija Khamis –Maelezo Zanzibar 10/07/2019.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kamisheni ya kukabiliana na maafa Zanzibar Ndg.Makame Khatib Makame amesema elimu ya majanga ya maafa ni muhimu kupewa watoto na walezi ili kuweza kujikinga pindipo yakitokea .
Akifungua mafunzo ya siku moja ya kutoa elimu kwa walezi na watoto wa Kituo cha kulelea Watoto Yatima Mazizini ili kujua jinsi ya kukabiliana na maafa ikiwemo mtetemeko wa ardhi ,moto ,mafuriko pamoja na kimbunga .
Alisema kuwa watoto, wazee, walemavu na mama wajawazito ni waathirika wakubwa hivyo wakipata elimu itawasaidia kujiokoa na majanga na kusaidiana na wengine.
Alifahamisha kuwa suala la maafa linamgusa kila mtu hivyo iko haja ya kuwafikishia taaluma watoto waliomo katika vituo mbali mbali ili kuweza kujikinga kwani maafa huwa hayachagui umri wala jinsia .
“Suala la maafa linamgusa kila mtu wala halichagui muda na hutokea wakati wowote lazima tuwe na tahadhari .“alisema MkurungenzI Makame .
Nae Mkurugenzi wa Wanawake na Watoto ambae pia ni Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Wazee na Ustawi wa Jamii Nasima Haji Chum alisema mafunzo yatasaidia kuwapa uwezo walezi na watoto kupambana ili kupunguza athari .
Alisema maisha ya binaadamu yamezungukwa na mambo mengi ikiwemo majanga ya maafa ya kimaumbile na maafa ambayo yanayosababishwa na binaadamu hivyo ni muhimu kujua jinsi ya kuweza kujiokoa hasa kwa wale makundi maalum .
Ofisa Mratibu wa kutoa Elimu kutoka Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa Aziza Ali Rajabu alisema elimu watakayopata walezi na watoto wa vituoni itasaidia kuokoa na kupunguza athari za majanga ya maafa katika sehemu mbali mbali .
Aliwataka walezi na watoto wenye umri mkubwa ambao tayari wanajitambua kuwa na tahadhari kwa wenzao wadogo ili kuwaepusha na kuchezea vitu hatarishi kama umeme na kuwasha vibiriti karibu na majiko ya gesi .
Nae Mdhamini wa Kituo cha Kulelea watoto Yatima Mazizini Chum Ali Abeid alisema wamefurahishwa na kupata fursa ya mafunzo hayo watayafanyia kazi na kuwa na tahadhari kubwa kwa watoto wao.
Aidha alisema elimu hii itawajengea uwezo wa kujua jinsi gani wataweza kumuokoa mtoto pindipo ataanguka na kuzimia na kuwadhibiti pindi maafa yakitokea ili kuokoa maisha yao.
Nao watoto waliopata mafunzo hayo wamesema wamefurahishwa na taaluma hiyo na kuahidi kuyafanyia kazi na kuyafikisha kwa wenzao ,
Mafunzo hayo ya siku moja yalijumuisha vituo vya kulelea watoto yatima ikiwemo kijiji cha kulelea watoto yatima SOS pamoja na mazizini .
No comments:
Post a Comment