Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk.Ali Mohamed Shein Azungumza na Uongozi wa Wizara ya Kazi Uwezeshaji wa Wazee Wanawake na Watoto Zanzibar.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein (katikati) akizungumza na Uongozi wa Wizara ya Kazi,Uwesheji,Wazee,Wanawake na Watoto   katika mkutano wa utekelezaji wa malengo ya mpango kazi kwa kipindi cha Julai  2018-Juni 2019 na mpango kazi wa mwaka 2019-2020 katika ukumbi wa Ikulu Mjini Zanzibar leo,[Picha na Ikulu.] 23/08/2019.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameeleza haja kwa uongozi wa Wizara ya Kazi, Uwezeshajai Wazee, Wanawake na Watoto kuandaa utaratibu maalum wa kuangalia afya za wafanyakazi kabla na baada ya kuajiriwa kazini.

Hayo aliyasema leo, Ikulu mjini Zanzibar alipokutana na uongozi wa Wizara ya Kazi, Uwezeshajai Wazee, Wanawake na Watoto wakati ilipowasilisha utekelezaji wa Mpango Kazi wa Julai  2018 hadi Juni 2019 sambamba na Mpango Kazi wa Utekelezaji kwa mwaka 2019/2020.

Alieleza kuwa utaratibu huo utaweza kurahisisha na kutambua afya za wafanyakazi kwani tayari Serikali inao utaratibu mzuri wa kuwashughulikia wafanyakazi wakati wanapopata ajali wakiwa kazini lakini haipendezi kuona afya za wafanyakazi hazitambuliwi wakati wapo kazi.

Hivyo,  Rais Dk. Shein alisisitiza haja kwa Wizara hiyo kukaa pamoja na kushirikiana na Wizara ya Afya katika kuandaa uataratibu huo maalum utakaowasaidia wafanyakazi kutambua afya zao wakati wote wakaiwa kazini.

Aidha, Rais Dk. Shein ameiagiza Wizara hiyo kufikiria namna ya kuongeza mtaji wa Mfuko wa Uwezeshaji wa Wananchi Kiuchumi ili mfuko huo uweze kukidhi mahitaji ya wananchi ambao idadi yao imekuwa ikiongezeka siku hadi siku.

Amesema kuwa katika kipindi cha miaka minane iliyopita Serikali imechukua juhudi kubwa za kuwawezesha wananchi kupitia mfuko huo ambapo matunda yake yamekuwa yanaonekana wazi wazi.

Pamoja na hayo, Rais Dk. Shein alieleza haja kwa Wizara hiyo kuandaa utaratibu utakaoweza kusaidia kubainisha na kutambua hali ya changamoto ya udhalilishaji wa wanawake na watoto ambayo imekuwa tatizo katika jamii hivi sasa.


Ameeleza matumaini yake makubwa kwa Wizara  hiyo na kusisitiza jinsi anavyofarajika na utendaji kazi kwa uongozi na wafanya kazi wote wa Wizara hiyo na kuwasisitiza kuendeleza umoja na mshikamano wao ili waweze kupata mafanikio zaidi.

Pamoja na hayo, Rais Dk. Shein alisisitiza haja kwa waajiri wa sekta binafsi kufuata sheria, taratibu na kanuni za uajiri katika kuhakikisha  wanarekebisha maslahi ya wafanyakazi wao kwani huo ni uamuzi wa Serikali.

Rais Dk. Shein alitumia fursa hiyo kuupongeza uongozi  wa Wizara hiyo kwa kuwasilisha vyema Mpango Kazi wao huo na kupelekea mjadala huo kuwa mzuri.

Alieleza kuvutiwa kwake na tafiti nne zilizofanywa na Wizara hiyo  ukiwemo utafiti wa kuwatambua na kuwawezesha Vijana Nguvu Kazi Zanzibar, Utafiti wa Fursa za ajira zilizopo katika sekta ya kilimo, uvuvi na utalaii kwa vijana na utafiti wa Pensheni Jamii.

Nae Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee aliipongeza kazi nzuri ya uwasilishaji iliyofanywa na Wizara hiyo huku akisisitiza haja kwa uongozi na wafanyakazi wa Wizara hiyo kuendeleza mashirikiano.

Mshauri wa Rais wa Zanzibar Pemba Dk. Maua Abeid Daftari alitoa pongezi kwa uongozi wa Wizara hiyo kwa kazi nzuri wanazozifanya huku akisisitiza haja ya kuwa na mashirikiano kati ya Wizara hiyo pamoja na Wizara ya Katiba na Sheria.  

Mapema, Naibu Waziri wa Wizara ya Kazi, Uwezeshajai Wazee, Wanawake na Watoto  Shadia  Mohamed Suleiman   alieleza kuwa  Dira ya Wizara hiyo ni kuwa na jamii ya Wazanzibari yenye ajira za staha, ubunifu na uwezo wa kukabiliana na umasikini inayotokana na fursa sawa kwa watu wa makundi yote.

Naibu Waziri huyo alieleza kuwa Wizara hiyo inaendlea na  kusimmaia utekelezaji wa Sheria na kanuni za kazi, kusimamia upatikanajiwa ajira hasa kwa bijana ndani nan je ya nchi.

Aidha, alieleza kuwa Wizara hiyo inaendelea kusimamia usuluhishi na uamuzi wa migogoro ya kazi sehemu za kazi, kuimarisha usalama na afya kazini, kuongeza na kutanua program za uwezeshaji wananchi kiuchumi, kuimarisha program za maendeleo na hifadhi ya wazee, wanawake na watoto pamoja na kuratibu masuala la jinsia katika Sera, Sheria, Mipango na bajeti za Kitaifa na Kisekta.

Alieleza kuwa kwa mwaka wa fedha wa 2018/2019 Wizara imepata mafanikio kadhaa yakiwemo kukamilisha ujenzi wa ghorofa ya pili ya jengo la Ofisi Kuu ya Wizara Unguja na kupata Ofisi mpya Pemba jambo ambalo limepunguza tatizo la uhaba wa Ofisi kwa Watendji.

Pia, Wizara imefanikiwa kutoa mikopo 553  Unguja na Pemba yenye thamani ya TZS milioni 782 kwa Shehia 223 kwa Unguja na Pemba  pamoja na kufanya  usajili wa vyama vya ushirika 281.

Pamoja na hayo, Naibu Waziri huyo alieleza mafunzo mbalimbali yaliyofanywa na Wizara hiyo pamoja na kushirikiana na Serikali ya India, Shirika la UNDP, FAO na COSTECH kwa ajili ya wajasiriamali pamoja na vijana wa Unguja na Pemba.

Alieleza kuwa Wizara hiyo imeendelea kuratibu, kusimamia na kutekeleza Mpango wa pensheni Jamii kwa wazee wenye umri wa miaka sabini na kuendelea ambapo idadi ya Wazee wanaopokea pensheni jamii imefikia walengwa 27,990 ambapo hadi Juni, 2019 wazee wapya 2,275 wamesajiliwa na wazee 1,911 walifariki kwa mwaka 2018/2019.

Naibu Waziri huyo huyo alieleza kuwa Wizara imeratibu upatikanaji wa ajira 2,759 Unguja na Pemba, ambapo ajira 1,555 ni za ndani na ajira 1,204 ni za nje katika nchi za UAE na Oman, pia, Wizara imefanya ukaguzi wa usalama na afya kazini.

Uongozi wa Wizara hiyo pia, ulimpongeza Rais Dk. Shein kwa kuwapa maelekezo ya kutekeleza kazi zao kwa ufanisi sambamba na anavyotekeleza ipasavyo Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi yenye lengo la kuleta usawa na maendeleo endelevu kwa wananchi wote.

Aidha, uongozi huo walieleza kuwa wengi wa waajiri wa sekta binafsi wametekeleza agizo la wafanyakazi la kuwaongezea mishahara kwani hizo ni haki za wafanyakazi na wamekuwa wakizisimamia kwa nguvu zote.

Pia, walieleza kuwa na mashirikiano makubwa sambamba na kufanya kazi kwa pamoja kati yao na Wizara ya Katiba na Sheria.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.