Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe,.Dk. Ali Mohamed Shein, akizungumza na Uongozi wa Wizara ya Biashara na Viwanda Zanzibar, wakati wa mkutano wa Utekelezaji wa Bajeti na Mpango Kazi wa Wizara hiyo kwa mwezi wa Julai 2018 hadi Juni 2019. uliofanyika katika ukumbi wa Ikulu Zanzibar,27-8-2019,
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.
Ali Mohamed Shein ameeleza kuwa nia ya Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar ni kuhakikisha sauti za Wajasiriamali zinasikika na
zinafanyiwa kazi ili kufikia malengo waliyoyakusudia.
Rais Dk. Shein aliyasema, Ikulu mjini Zanzibar
alipokutana na uongozi wa Wizara ya Biashara na Viwanda wakati ilipowasilisha Mpango
Kazi wa Julai 2018 hadi Juni 2019 sambamba na Mpango Kazi wa Utekelezaji kwa
mwaka 2019/2020.
Alieleza kuwa matajiri walio wengi duniani walianza
na ujasiriamali hivyo ni vyema wajasiriamali wakapewa kipaumbele katika
shughuli zao wanazozifanya ili waweze kupata mafanikio na kufikia malengo yao
waliyoyakusudia ikiwa ni pamoja na kuwashirikisha kikamilifu katika maonesho ya
kibiashara ya ndani na nje ya nchi.
Alieleza kuwa mbali ya matajiri hao duniani, hata
hapa Zanzibar matajiri walio wengi wameanza na ujasiriamali hivyo, si jambo la
busara kuwabeza na badala yake ni vyema
wakapema kipaumbele na mashirikiano ya kutosha.
Aidha, Rais Dk. Shein alisisitiza haja ya
kuwasaidia wajasiriamali ili na wao waweze kuwa wafanyabiashara wakubwa na kufikia
malengo waliojiwekea jambo ambalo limeiibua Serikali katika kuhakikisha
inawatekelezea matakwa yao na kuwashirikisha kikamilifu
Pamoja na hayo Rais Dk. Shein alitumia fursa hiyo
kutoa pongezi kwa uongozi wa Wizara ya Biashara na Viwanda kwa kuwasilisha
vyema Mpango Kazi wao na kueleza kuwa utendaji wao pamoja na wafanyakazi wa
Wizara hiyo ndio uliopelekea kupata mafanikio
Hivyo, Rais Dk. Shein aliutaka uongozi huo kuongeza
kasi na kufanya kazi kwa bidii ili mafanikio zaidi yaendelee kupatikana katika
kuimarisha sekta hiyo ambayo ina umhimu katika kuimarisha uchumi na kukzua
sekta za kijamii.
Rais Dk. Shein alipongeza mafanikio makubwa yaliopatikana
katika Wizara hiyo chini ya uongozi wa Waziri wake Balozi Amina Salum Ali
ambaye amefanya juhudi kubwa ya kuiimarisha Wizara hiyo katika uongozi wake kwa
mashirikiano ya pamoja na watendaji wake.
Dk. Shein aliutaka uongozi wa Wizara hiyo
kuendelea kumsaidia Waziri wao huyo kila mmoja kwa wakati wake na nafasi yake
kwa lengo la kuimarisha sekta ya biashara na viwanda kwani azma ya Serikali ni
kuhakikisha Zanzibar inakuwa kwenye ramani ya viwanda.
Alieleza matumaini ya kuimarika kwa zao la mwani
ambapo tayari kuna aina nne za mwani hapa Zanzibar na kueleza kuwa hatua hiyo
itapelekea kupata mafanikio mazuri ya zao hilo ikiwa ni pamoja na mchakato wa
kujenga kiwanda cha mwani huko Chamanangwe Pemba.
Alieleza kuwa Zanzibar ina historia kubwa ya
kulima mazao mbali mbali yakiwemo ya viungo vya chakula kwa muda mrefu, hivyo
ni vyema mazao hayo yakaimarishwa ikiwa ni pamoja na kuwashajiisha wakulima kuyalima
vikiwemo viungo kama pilipili hoho.
Rais Dk. Shein alisisitiza haja ya kulima kwa
wingi kwa viungo vya chakula kwa sababu vimekuwa vikipendwa sana nje ya nchi
hivyo ni vyema kilimo hicho kikaimarishwa.
Aidha, alieleza kufarajika kwake na uongozi wa Wizara
hiyo kwa kutumiwa alama ya ubora ya Taasisi ya Viwango Zanzibar (ZBS) katika
bidhaa mbali mbali zinazozalishwa ndani na nje ya nchi huku akieleza azma ya
Zanzibar kuwa nchi ya viwanda.
Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd alitoa pongezi
kwa uongozi huo na kuzipongeza juhudi za Waziri Balozi Amani Salum Ali za kuhakikisha maendeleo yanapatikana katika sekta ya
viwanda na biashara ikiwa ni pamoja na kuanzishwa kwa Mamlaka inayosimamia Viwanda vidogo vidogo na
Vya Kati (SMIDA).
Nae Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la
Mapinduzi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee aliipongeza kazi nzuri ya uwasilishaji
iliyofanywa na Wizara hiyo huku akisisitiza haja kwa uongozi huo kuendeleza
mashirikiano na uadilifu.
Mshauri wa Rais wa Zanzibar Pemba Dk. Maua Abeid
Daftari kwa upande wake alitoa pongezi kwa Shirika la Biashara la Taifa (ZSTC)
kwa kuendeleza zao la mchaichai kisiwani Pemba kwani wananchi wengi
wamehamasika na kuomba wasaidiwe kuwekewa vinu karibu na sehemu wanazoishi.
Mapema Waziri wa Biashara
na Viwanda Balozi
Amina Salaum Ali akiwasilisha muhtasari wa utekelezaji Mpango Kazi wa Wizara
hiyo alisema katika kipindi cha mwaka 2018/2019 jumla ya tani 218,911 za
chakula muhimu ukiwemo mchele, sukari na unga wa ngano zilikuwepo kwa ajili ya
matumizi ya soko la ndani na kuifanya Zanzibar kuendelea kuwa na chakula cha
kutosha cha aina hizo katika kipindi chote.
Alieleza kuwa sensa ya viwanda iliyofanyika mwaka
2016 ilionesha idadi ya viwanda imeongezeka ambapo sukari imeongezeka kutoka tani 677
iliyozalishwa mwaka 2017 hadi tani 3,339 kwa mwaka 2018 sawa na ongezeko la
asimilia 79.7 na uzalishaji wa unga wa ngano nao uliongezeka kutoka tani 25,196
mwaka 2017 hadi tani 26,963 mwaka 2018.
Balozi Amina alieleza kuwa katika kipindi cha
mwaka 2018/2019, Shirika la Biashara la Taifa limenunua karafuu tani 211.34 kwa
jumla ya TZS Bilioni 2.9 ambapo pia uzalishaji wa mafuta ya mimea ulifikia kilo
40,955.3 kwa jumla ya TZS bilioni 1.5.
Alieleza kuwa Serikali inaendelea kununua karafuu
kulingana na Sera ya Serikali ya kununua kwa bei ya asilimia 80 ya bei ya
kuuzia nje hata hivyo, msimu mdogo wa karafuu kwa mwaka 2018/2019 ulipelekea
kupungua kwa tani za ununuzi wa karafuu.
Kwa bajeti ya mwaka 2019/2020, alisema Wizara
inakusudia kuimarisha maabara za ZBS zilizopo Amani pamoja na kuimarisha
miundombinu, vifaa vya ukaguzi wa magari, kuliendeleza eneo la Nyamanzi
sambamba na kuongeza vifaa kwa ajili ya matamasha.
Alieleza kuwa Wizara hiyo kwa kushirikiana na wataalamu
kutoka Indonesia inatarajia kufanya mafunzo ya ukulima wa mwani ulio na tija na
kuanza maandalizi ya kuanzisha kiwanda cha kusarifu mwani huko Chamanangwe kisiwani
Pemba.
Balozi Amina, alieleza mpango wa Wizara wa
kusimamia program maalum ya wajasiriamali inayopata msaada kutoka mfuko maalum wa
Nchi za Falme za Kiarabu pamoja na mchango wa Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar.
Alisisitiza kuwa ili kurahisisha ufanyaji biashara
hapa Zanzibar, Wizara itaandaa mfumo maalum wa Tehama ambao utatoa taarifa na
huduma muhimu za usajili, uwekezaji na leseni au vibali vinavyotakiwa kwa
wawekezaji na wafanyabiashara.
Pia, uongozi huo ulieleza juhudi inazozichukua kwa
wafugaji wa nyuki kwa kuwapa mafunzo maalum wafugaji hao sambamba na kusimamia vyema ufugaji huo
kwa lengo la kupata asali yenye ubora na viwango vinavyohitajika kitaifa na
kimataifa.
Uongozi huo pia, ulimpongezi Rais Dk. Shein kwa
utaratibu mzuri alioweka wa mikutano hiyo inayojadili Mpango Kazi wa Mawizara
huku wakitumia fursa hiyo kueleza sifa inazozipata Zanzibar kutoka kwa wageni
wanaokuja kuitembelea kutokana na amani, utulivu, upendo pamoja na maendeleo
yaliopo.
Uongozi huo pia, ulizitaja bidhaa
zilizizothibitishwa ubora na kupatiwa alama ya ubora ya (ZBS) kwa mwaka
2018/2019 ni maji ya kunywa ya (Zan Aqua), mchele (Tulip) unaozalishwa nchini
Pakistan, mchele wa (Ikram), unga wa sembe (Mwangaza), Mikate ya slesi, maji ya
kunywa (Pure life) na (Uhai), mafuta ya nazi na mifuko.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment