Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein azungumza na Balozi wa Jamuhuri ya Rwanda Nchini Tanzania Mhe.Eugine Kayihura alipofika Ikulu Zanzibar kuja kumuaga baada ya kumaliza muda wake wa kazi Nchini Tanzania.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.
Ali Mohamed Shein ameeleza kuwa lugha ya Kiswahili itakuwa ni kiunganishi
kizuri katika kukuza ushirikiano na uhusiano kati ya Rwanda na Zanzibar.
Rais Dk. Shein
aliyasema hayo leo Ikulu mjini Zanzibar wakati alipokutana na kufanya
mazungumzo na Balozi wa Rwanda nchini Tanzania Eugine Kayine Kayihura ambaye alifika
Ikulu kwa ajili ya kuaga.
Katika maelezo yake, Rais
Dk. Shein alimueleza Balozi Kayihura kuwa azma ya Rwanda na Zanzibar
kushirikiana katika sekta ya elimu hasa katika mafunzo ya lugha ya Kiswahili
itajenga uhusiano mwema kati ya pande mbili hizo.
Rais Dk. Shein
alieleza kuwa hatua hiyo itakuwa na mafanikio makubwa hasa ikizingatiwa kuwa
hivi sasa lugha ya Kiswahili tayari imeteuliwa kutumika rasmi katika Jumuiya ya
Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).
Aidha, Rais Dk. Shein
alieleza kufurahishwa kwake na uhusiano mzuri uliopo kati ya Rwanda na Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania ikiwemo Zanzibar jambo ambalo amesisitiza kuwa ni vyema
likaendelezwa kwa nguvu zote.
“Mahusiano na
mashirikiano yetu ni lazima yaendelezwe kwani sote ni ndugu na haya ndio
yanayotupa nguvu na ari ya kuyaimarisha na kuyaendeleza maendeleo yetu
tulioyapata sambamba na kufikia malengo tuliyoyakusudia”,alisema Dk. Shein.
Pamoja na hayo, Rais
Dk. Shein alimueleza Balozi huyo mafanikio yaliopatika Zanzibar kutokana na
sekta ya utalii ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa idadi kubwa ya watalii ndani
ya miaka hii tisa ya uongozi wake.
Alimueleza Balozi huyo
kuwa idadi ya watalii wanaokuja kuitembelea Zanzibar imeongezeka kwa kiasi
kikubwa ikifananishwa na ile ya mwaka 2010 ambapo kwa hivi sasa watalii
wanakadiriwa kufikia laki sita wametembelea Zanzibar.
Hivyo, alieleza kuwa kuwepo
kwa mashirikiano kati ya Rwanda na Zanzibar katika sekta hiyo kutakuwa na manufaa
kwa pande zote mbili.
Katika kuhakikisha
sekta ya utalii inaimarika zaidi, Dk. Shein alimueleza Balozi huyo mikakati
iliyowekwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kuendeleza ujenzi wa jengo
jipya la abiria katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume.
Alisisitiza kuwa hatua
hiyo ya kuendeleza ujenzi huo ambao ulisita kwa muda itazidisha na kuongeza idadi
ya watalii watakaoingia Zanzibar na kupelekea sekta hiyo izidi kuimarika na
kuongeza pato la Taifa sambamba na fedha za kigeni.
Sambamba na hayo, Rais
Dk. Shein alimuhakikishia Balozi Kayihura kuwa Serikali ya Zanzibar chini ya
uongozi wake itashirikiana nae vyema Balozi mpya wa Rwanda atakayekuja kuchukua
nafasi yake.
Nae Balozi Eugine Kayihura alisema kuwa Rwanda inajivunia
uhusiano na ushirikiano mzuri uliopo kati yake na Zanzibar na kusisitiza kuwa
miongoni mwa mahusiano hayo ni kushirikiana katika sekta ya elimu hasa katika
kujifunza lugha ya Kiswahili ambayo Zanzibar ndio kitovu cha lugha hiyo.
Kutokana na hali hiyo,
itakuwa ni jambo la busara kwa Rwanda kuleta vijana wake kwa lengo la kujifunza
Kishwahili sambamba na kubadilishana uzoefu kati ya vijana hao na wenzao wa
Zanzibar hatua ambayo itakuza na kuimarisha uhusiano na ushirikiano.
Aidha, alisema kuwa
Rwanda ina mambo mengi ya kujifunza na kupanua wigo kutoka Zanzibar kutokana na
mafanikio makubwa yaliopatikana katika sekta ya utalii ambapo, watalii wengi
wanaotembelea Rwanda pia, hufika na Zanzibar.
Sambamba na hayo,
Balozi huyo alieleza kufurahishwa kwake na mafanio iliyoyapata Zanzibar hasa
katika kuimarisha sekta ya Utalii na kupongeza juhudi zinazochukuliwa na
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya uongozi wa Dk. Shein katika
kufanikisha sekta hiyo.
Balozi Kayihura ambaye
alimueleza Rais Dk. Shein kuwa anatarajia kituo chake kipya cha kazi kitakuwa
ni Afrika ya Kusini alimuhakikishia Rais kuwa Rwanda kupitia Balozi wake mpya
atakayechukua nafasi yake ataendelea kushirikiana na Zanzibar.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment