Habari za Punde

Waziri Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Aagiza Apelekewe Taarifa za Utendaji wa DED Lindi.

Waziri Mkuu Mhe.Kassim Majaliwa amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Bw. Shaibu Ndemanga ampelekee taarifa za utendaji kazi wa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya Bw. Waryoba Gunza baada ya kushindwa kutoa maelezo kuhusu utekelezaji wa mradi wa maji kata ya Rutamba.

Ametoa agizo hilo leo (Ijumaa, Agosti 23, 2019) wakati akizungumza na wananchi katika Mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye kijiji cha Rutamba akiwa katika ziara yake ya kikazi ya kukagua shughuli za maendeleo na huduma za jamii mkoani Lindi.

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo baada ya kumtaka Mkurugenzi huyo atoe maelezo ya namna gani walivyojipanga katika kutekeleza mradi wa maji kwenye kata hiyo ambayo wakazi wake wanakabiliwa na tatizo la upatikanaji wa maji na kushindwa kutoa maelezo.

Kwa mujibu wa Mhandisi wa Maji wa Wilaya ya Lindi, Bw………alisema mradi wa kata hiyo unakabiliwa na tatizo la uchakavu wa miundombinu na ukarabati wake unahitaji bajeti sh. milioni 75 ambazo wameziomba kutoka Wizara ya Maji.

Waziri Mkuu amesema miradi yote ambayo gharama zake ziko chini ya sh. milioni 100 inatakiwa itekelezwe kwa kutumia fedha za ndani ya halmashauri husika. “Miundombinu hiyo ilitakiwa iwe imebadilishwa. Mradi wa sh. milioni 75 unaomba fedha wizarani ni uvivu.”
Waziri Mkuu amesema suala la huduma ya maji limewekewa msisitizo na Rais Dkt. John Magufuli kwa kuanzisha kampeni ya kumtua mama ndoo kichwani, inayolenga kuwawezesha wananchi kupata maji safi na salama karibu na makazi yao.
Waziri Mkuu aliwaambia wananchi kuwa Serikali ya Awamu ya Tano ina mikakati mizuri inayolenga kuondoa tatizo la maji kote nchini ili kusaidia wananchi hao hasa wanawake kutumia muda mwingi kufanya kazi za maendeleo kuliko kutafuta maji.
Hata, hivyo Waziri Mkuu amewahakikisha wananchi hao kwamba licha ya kuagiza mradi huo wa ukarabati wa miundombinu ya kusambazia maji ufanyike kwa haraka, pia Serikali inatekeleza mradi mwingine wa maji wa Milola ambao ukikamilika maji yatafikishwa hadi Rutamba.
Wakati huo huo,Waziri Mkuu amewaagiza Wakuu wa Wilaya nchini wahakikishe wanawasimia vizuri watumishi wa umma na kuwachukulia hatua wote watakaobainika kushindwa kutekeleza majikumu yao ipasavyo.
“Rais Dkt. John Pombe Magufuli ana nia njema ya kuwapa huduma safi wananchi wote hadi wanyonge na ameelekeza wahudumiwe vizuri bila ya ubaguzi. Wananchi kama kuna mtumishi asiyewahudumia vizuri msisite kumtaja kwa sababu Serikali hii haitomvumia.”
Waziri Mkuu asema ni lazima kila mtumishi wa umma anayelipwa mshahara kwa kutumia kodi za wananchi ahakikishe anatekeleza ipasavyo majukumu yake kwani asipofanya hivyo hatokuwa na nafasi ya kuendelea na kufanya kazi ndani ya Serikali.
“Watumishi fanyeni kazi kwa bidii na msitarajie kuundiwa tume pale mnapofanya vibaya, ukiharibu kazi tunakushughulikia hapo hapo na huu ndio msimamo wa Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli.”

Waziri Mkuu amesema kuwa watumishi wanatakiwa wafanye kazi kwa kuzingatia sheria na kanuni za kazi na pia watambue dhamana kubwa waliyonayo, ambayo ni kuwahudumia wananchi wote bila ya ubaguzi wa aina yoyote.

Amesema watumshi wa umma hawapaswi kukaa maofisini bali wanatakiwa wapange siku nne katika juma kwa ajili ya kwenda kutembelea wananchi hususani waishio maeneo ya vijijini kwa ajili ya kuwasikiliza kero zao na kuzipatia ufumbuzi.

Waziri Mkuu amesema Serikali imedhamiria kuboresha huduma za jamii ambazo zilikuwa zikiwakwaza wananchi zikiwemo za miundombinu ya barabara, tatizo la maji, elimu na afya, lengo likiwa ni kuwawezesha Watanzania wote waishi vizuri.
Awali, akizungumza kwaniaba ya wabunge wa mkoa wa Lindi, Mbunge wa Viti Maalumu, Riziki Lulida alisema wakazi wa kata ya Rutamba wanakabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji licha ya kuwepo kwa vyanzo, hivyo aliiomba Serikali iwasaidie.
Hata hivyo alilalamikia kuwepo kwa uharibifu mkubwa wa mazingira katika maeneo hayo ikiwemo uvamizi katika vyanzo vya maji pamoja na ukataji hovyo wa misitu unaohatarisha kuibuka kwa jangwa, ambapo Waziri Mkuu ameagiza viongozi wa wilaya hiyo kuzishughulikia suala hilo.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,         
IJUMAA, AGOSTI 23, 2019.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.