Na.Mwandishi Wetu.
Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu wa Uchumi Zanzibar
(ZAECA), imefanikiwa kukamata fedha mabunda zaidi ya 30 ya fedha za kigeni zinazosadikiwa
kuwa ni feki.
Akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa ZAECA, Mkuu
wa kitengo cha uchunguzi na operesheni, Makame Khamis Hassan, alisema fedha
hizo zinazodaiwa kumilikiwa na Ndg.Khatibu Amini Makame (Nondo), wamefanikiwa
kuzikamata baada ya kupata taarifa kutoka kwa wasamaria wema kutoa taarifa hiyo.
Mkuu huyo alisema tukio hilo limetokea katika maeneo ya baa
ya sai iliyopo maeneo ya Kibonde mzungu wilaya ya Magharibi B Unguja.
Hili ni tukio la pili kukamata fedha kama hizo ambazo ni
kosa kwa mujibu wa kifungu cha sheria 51, kinaeleza kwamba mtu yeyote atakae jihusisha
au kujiingiza moja kwa moja katika vitendo vya kughushi bidhaa fedha au
utambulisho wa bidhaa au huduma kwa manufaa ya kipato au faida kwa manufaa ya
kibiashara ametenda kosa la kuhujumu uchumi chini ya sheria namba moja ya mwaka
2012, ya ZAECA.
Mkuu huyo alisema baada ya kupata taarifa hiyo walifanikiwa
kuweka mtego na hatimae kufanikiwa kumkamata mtu huyo.
Alifahamisha kwamba mzigo huo na mtuhumiwa wanaendelea
kumshikilia ili kuendelea na upelelezi ili kuweza kukamilisha tuhuma hizo.
Alibainisha kwamba kukamilika kwa hatua hiyo mtuhumiwa huyo atafikishwa
katika vyombo vya sheria ili kuendelea na hatua nyengine za kisheria.
Aidha alitumia fursa hiyo kuitaka jamii kuacha kujihusisha
na matukio kama hayo ambayo yanapelekea kuhujumu uchumi wa nchi, ameitaja jamii wakibaini vitende hivyo kutoa taarifa ZAECA ili kuwafichua wale wote wanaojihusisha na vitendo hivyo
kwa namna moja ama nyengine.
Sambamba na hayo Mkuu huyo alisema kutokea kwa matukio kama
hayo yanasababisha kwa kiasi kikubwa serikali kukosa uwezo wa kutekeleza huduma
mbalimbali za kijamii, hivyo ushirikiano wao ndio chachu ya kutokomeza vitendo
hivyo.
No comments:
Post a Comment