Habari za Punde

BAKWATA Waishukuru Serikali ya Mkoa Kufanikisha Kupata Hati za Viwanja Vyao.

Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (kushoto) akimkabidhi hati za viwanja viwili vya Baraza Kuu la Waislamu Tanzania vilivyopo Manispaa ya Sumbawanga Shekhe wa Mkoa Shekh Rashid Akilimali wakati wa hafla fupi ya Makabidiano hayo.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (waliokaa katikati) pamoja na Katibu Tawala Mkoa wa Rukwa Bernard Makali (wa pili Kutoka kulia) na Shekhe wa Mkoa Shekh Rashid Akilimali (wa pili toka Kushoto) Kamati ya Ulinzi na Usalam ya mkoa pamoja na viongozi wengine wa Wilaya na Halmashauri. 
   
Shekhe wa Mkoa wa Rukwa Shekhe Rashid Akilimali amepongeza juhudi za serikali ya mkoa wa Rukwa chini ya mkuu wa mkoa huo Mh. Joachim Wangabo kwa kuweza kufanikisha kupatiwa viwanja viwili vyenye jumla ya ekari 18 vilivyopo katika Manispaa ya Sumbawanga baada ya kupita miaka 13 ya mgogoro baina ya Taasisi hiyo na uongozi wa serikali ya mkoa.
Amesema kuwa Serikali hii ya awamu ya tano ndio inayotakiwa kwani inawajali wanyonge na kuwapa haki wale wanaostahiki kupewa haki hiyo na kuongeza kuwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli kweli anajua kuwateua watu wake na hakukosea kumteua Mh. Wangabo kuuongoza mkoa wa Rukwa
“Kwahiyo mheshimiwa nikushukuru kwa niaba ya waislamu wa mkoa wa Sumbawanga, hili linatoka Moyoni kwangu rasmi, miaka 13 leo tunakabidhiwa hati hizi, imetugonga mioyo, imeleta farka ya jamii, unapomchangisha sadaka mtu halafu isionekane imefanya kazi fulani anabaki anajenga hoja ambayo haipo, wewe ni mfano wa kuigwa kwa wakuu wa mikoa wengine kwa jambo hili, lakini nitakuwa mnyimi wa fadhila kutokumshukuru Mkurugenzi wa Manispaa, kijana Madhubuti kabisa huyu, amejitoa muhanga akasema ardhi hii ipo na mtapata lakini kwa usimamizia wako,” Alisisitiza
Aidha, Shekhe Akilimali alitumia nafasi hiyo kuiomba radhi serikali ya mkoa kwa niaba ya waislam wa mkoa huo katika eneo ambalo uongozi wa taasisi uliwakwaza katika kufuatilia hati hizo na kuonekana ni tatizo katika ofisi za serikali.
Kwa upande wake Mh. Wangabo alisema kuwa ni dhamana ya viongozi katika maeneo mbalimbali ya kiutawala kuhakikisha kuwa hakuna migogoro baina ya serikali na wananchi wanaoongozwa na kuongeza kuwa viongozi kwa namna yoyote ile ni lazima wawe tayari kuitatua migogoro hiyo kwasababu madhara yake ni makubwa na isiposhughulikiwa kwa wakati itapelekea kukosekana kwa utulivu na amani na hatimae maendeleo yanadumaa.
“Tnapotatua migogoro ya namna hii tunawezesha serikali kupita hatua za kimaendeleo pamoja na wananchi kwa ujumla wanapiga hatua za kimaendeleo, mgogoro huu wa viwanja umekuwepo tangu miaka hiyo ya 2006, miaka mingi sana lakini sasa leo tumekata mizizi ya fitina, tunaamini kabisa kwamba kuanzia sasa hivi tutakwenda kwa amani na utulivu na madhehebu ya dini zote sit u waislamu hata wakristo ambapo nao kulikuwa na mgogoro mzito tangu 1985 ambapo nao tumekwishautatua,” Alieleza.
Halikadhalika, Mh. Wangabo alimuagiza Mkurugenzi wa Manispaa ya Sumbawanga kufanya haraka katika kuwafikisha viongozi hao wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA)katika maeneo hayo ambayo wamepatiwa hati ili waweze kutambua mipaka yao huku kukiwa na muwakilishi kutoka ofisi ya Mkuu wa mkoa pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga.
Awali akitoa taarifa ya mgogoro huo Katibu wa BAKWATA Mkoa wa Rukwa Ust. Mohamed Adam alisema kuwa kuna wakuu wa mikoa kadhaa ambao wamepita katika mkoa huo lakini hawakuweza kujaaliwa kuumaliza mgogoro huo ambao umemalizika leo tarehe 30.8.2019 na kusisitiza kuwa jambo hilo litabaki kuwa historia kwa waislamu wa Mkoa wa Rukwa.
“Sisi Waislamu wa Mkoa huu kwa jambo hili ulilolifanya tutaendelea kukumbuka katika maisha yetu yote na Mwenyezi Mungu akujaalie sana Mheshimiwa mkuu wa mkoa kwa alama hii uliyoiweka katika mji wetu,” Alisema.
Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mhe. Joachim Wangabo kwa niaba ya Serikali amekabidhi hati za Viwanja viwili vyenye namba 50074 na 50075 kwa Shekhe wa Mkoa Shekhe Rashid Akilimali kwa niaba ya Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA).
MAelezo ya Picha 
IMG_3159 - Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (kushoto) akimkabidhi hati za viwanja viwili vya Baraza Kuu la Waislamu Tanzania vilivyopo Manispaa ya Sumbawanga Shekhe wa Mkoa Shekh Rashid Akilimali wakati wa hafla fupi ya Makabidiano hayo.
SSW_1616 - Picha ya pamoja ya Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (waliokaa katikati) pamoja na Katibu Tawala Mkoa wa Rukwa Bernard Makali (wa pili Kutoka kulia) na Shekhe wa Mkoa Shekh Rashid Akilimali (wa pili toka Kushoto) Kamati ya Ulinzi na Usalam ya mkoa pamoja na viongozi wengine wa Wilaya na Halmashauri. 
   
IMETOLEWA NA 
OFISI YA MKUU WA MKOA WA RUKWA 
E-mail:       ras@rukwa.go.tz
                   ras.rukwa@tamisemi.go.tz
                   rukwareview@gmail.com
Website:    www.rukwa.go.tz
Twitter:      @Rukwakwetu
Simu Na:     025-/2802138/2802144
Fax Na.        (025) 2802217

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.