Na. Raya Hamad – WKS
Mkurugenzi Utumishi na Uendeshaji Ndg Juma Ali Simai amewataka maafisa utumishi
na wakuu wa vitengo kuendana na kasi ya mabadiliko kwa kufuata sheria kanuni na
miongozo ya kazi kwa mujibu wa utumishi wa Umma ili kila mtumishi atekeleze
majukumu yake ya kazi kwa ufanisi.
Mkurugenzi Juma ameyasema hayo alipokuwa akiyafungua mafunzo
ya tathmini ya upimaji wa mfanyakazi kwa Wakuu wa Divisheni na pamoja na wakuu wa vitengo kwa Taasisi zilizo
chini ya Wizara ya Katiba na Sheria kwenye ukumbi wa mkutano wa Wizara ya
Katiba na Sheria Mazizini.
Ndugu Juma amewataka Wakuu
wa Divisheni na pamoja na wakuu wa
vitengo hao kufuata taratibu na kuwa
waadilifu katika kuwafanyia tathmini
wafanyakazi ili kuepuka upendeleo au kumuonea mfanyakazi jambo ambalo
litampelekea kukosa haki yake ya msingi.
Aidha Mkurugenzi Juma amesema lengo la mafunzo hayo ni kuimarisha
Ufanisi wa utekelezaji wa majukumu, kuimarisha utoaji wa huduma bora kwa kufuata
utaratibu utakaotumika katika Upimaji Utendaji Kazi kwa Watumishi wa Umma na
kuondokana na mfumo wa mazoea ili kuongeza ari ya kiutendaji.
Pia amesisitiza kuwa kila mtumishi anaepatiwa majukumu yake
ayatekeze kwa kivitendo ili kufikia dira dhamira na malengo ya Serikali ya
Mapinduzi Zanzibar kuwa na watumishi wenye sifa “niwaombe sana mzingatie sheria
na kanuni tujitahidi kutenda haki kwa wafanyakazi wote kama anajitahidi na
kujituma ipasavyo na mkajiridhisha form ijazwe vizuri na kama maadili na
nidhamu mbaya basi kusiwe na upendeleo”alisisitiza.
Nae muwezeshaji wa mafunzo hayo ndugu Maulid Shaib Ahmada
amewataka wakuu wa vitengo kuzingatia mfumo wa Utumishi wa Umma
uliowazi na kuwapatia watendaji
waliochini yao majukumu yao ya kazi kwa maandishi ili nao waweze kujitathmini
badala ya kufanyakazi kwa mazowea.
Maulid amesema mafunzo yanayotolewa juu ya uanzishwaji
wa Upimaji Utendaji Kazi yanalenga kuwa na taswira moja ya muundo wa kiutumishi
na kupata uwelewa wa pamoja ili kurahisisha utekelezaji bora wa majukumu yao
kupitia mfumo huo.
Kuhusu Upandishwaji
vyeo katika Utumishi Serikalini Muwezeshaji huyo amesisitiza kuwa utazingatia
vigezo maalum ikiwemo misingi yahaki,
usawa, uwajibikaji, utendaji mzuri wa kazi, uzoefu na muda wa utangulizi wa
kuingia kazini kwa Watumishi wote.
“Kumpandisha Cheo Mtumishi ni sehemu moja wapo ya kumpa
motisha kutokana na utendaji wake, kujenga weledi na kuimarisha usimamizi
katika Utumishi wa Umma na kwa maana hio upandishwaji vyeo utazingatia kuwepo
bajeti iliyoidhinishwa kwa mwaka wa fedha husika, utendaji mzuri, uwajibikaji,
heshima, ubunifu, nidhamu, mashirikiano mazuri kati ya Mtumishi na Mtumishi
pamoja na Viongozi, sifa za kielimu, uzoefu na maarifa ya kazi aliyonayo katika
Daraja alilonalo.”
Aidha amesema taratibu za kumpandisha cheo mtumishi ni lazima
apimwe utendaji wake wa kazi kwa kujaza fomu ambayo inampandisha Daraja
mtumishi husika katika kada husika kutoka Daraja la chini kwenda Daraja la juu
kiutendaji na kimaslahi.
Fomu ya upimaji utendaji kazi ni Fomu yenye kutoa tathmini
ya utendaji wa kazi wa mtumishi baada ya
utekelezaji wa majukumu yake kupitia Hati Makubaliano ya utekelezaji wa
majukumu ya mtumishi, uwezo na ustadi
pamoja na vipimo vya tabia kwa ujumla.
Baada ya kukamilika kwa tathmini ya upimaji wa utendaji kazi
ya mtumishi husika na kufanikiwa kupata alama nzuri na kuendelea kwa miaka
mitatu (3) mfululizo, tathmin hiyo itamuwezesha mtumishi kuweza kupandishwa
cheo, kupatiwa nyongeza ya mishahara na kupewa tuzo, aidha itamuwezesha
kushushwa cheo, kupewa barua ya onyo na kutopatiwa
“Upimaji utendaji kazi Lazima uwe wazi na wa ushirikishwaji,
Ili kupandishwa Cheo italazimika ziwepo ripoti za tathmin za utendaji kazi kwa
muda usiopungua miaka mitatu (3) mfululizo zenye alama jumla 65% kwa
kila mwaka”alisitiza Maulid.
Aidha zoezi la
upandishwaji vyeo katika Utumishi wa Umma ni utekelezaji wa maelekezo ya
Sera ya Utumishi wa Umma ya mwezi
Oktoba, 2010 kama ilivyofafanuliwa katika mkakati wa kisera.
Ndugu Maulid amesisitiza suala la mtumishi anapopandishwa
cheo kupewa barua ili afahamu stahiki zake kwani cheo kinakwenda sambamba na
stahiki bila stahiki mtumishi atakuwa ameongezewa majukumu.
Katika risala yao Wakuu wa Divisheni na Wakuu wa vitengo waishukuru
Wizara ya Katiba na Sheria kwa kuridhia kufanyika kwa mafunzo hayo ambayo
yatatoa fursa kwa kila mshiriki kutekeleza vyema majukumu yake kwa kufuata
kanuni na taratibu zote za Kiutumishi.
Jumla ya mada mbili zilizojadiliwa ni upimaji utendaji kazi ambayo
imejumuisha maana ya upimaji utendaji kazi, madhumini ya upimaji utendaji kazi,wajibu
wa mamlaka husika, hati ya makubaliano, sehemu za hati ya makubaliano, fomu ya
upimaji utendaji kazi, sehemu za fomu ya upimaji utendaji kazi.
Upandishwaji cheo iliyojumuisha maana ya upandishwaji vyeo,
madhumini ya upandishwaji vyeo, dhana ya upandishwaji vyeo, walengwa wa
upandishwaji vyeo, vigezo vya upandishwaji vyeo, wajibu wa mamlaka husika katika upandishwaji
vyeo, fomu ya upandishwaji vyeo, sehemu za fomu ya upandishwaji vyeo.
No comments:
Post a Comment