Habari za Punde

Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar Yawaaga Wafanya Kazi Wao Waliostaaf Ukumbi wa Sheikh Idrissa Abdulwakil Kikwajuni Zanzibar.

Waziri Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Mohamed Aboud Mohamed akimkabidhi zawadi Mfanyakazi Mstaafu wa Idara ya Watu wenye Ulemavu Kisiwani Pemba Moh’d Othman Omar kwenye hafla ya kuagwa rasmi.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Mohamed Aboud Mohamed akizungumza katika hafla ya kuwaaga Wafanyakazi 24 Waliostaafu  wa Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar iliyofanyika katika Ukumbi wa Sheikh Idriss Abdulwakil Kikwajuni Mjini Zanzibar.
Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Nd. Abdullah Hassan Mitawi akitoa maelezo kwenye hafla ya kuwaaga Wafanyakazi 24 Waliostaafu  wa Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.
Mfanyakazi Mstaafu wa Huduma Idara ya Faragha Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Bibi Safia  Ahmada Foum akipokea zawadi kwenye hafla ya kuagwa rasmi.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar.Mhe.Mohammed  Aboud Mohammed kati kati waliokaa vitini akiwa katika picha ya pamoja na Wafanyakazi Wastaafu wa Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar iliyofanyika katika Ukumbi wa Sheikh Idriss Abdulwakil Kikwajuni Mjini Zanzibar.

Picha na – OMPR – ZNZ.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Mohammed Aboud Mohammed amesema mawazo, Ushirikiano, Uzoefu na utu wa Wafanyakazi waliomaliza muda wao wa Utumishi ndani ya Ofisi hiyo ambao kwa sasa Wastaafu utaendelea kuthaminiwa muda wote
Alisema kazi kubwa iliyofanywa na Wastaafu hao katika muda wao mrefu wa Utumishi itabakia kuwa Dira kwa watendaji wa sasa katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.
Mh. Mohamed Aboud Mohamed alisema hayo katika hafla fupi ya kuwaaga Wafanyakazi 24 Waliostaafu  Utumishi wa Umma wa Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar iliyofanyika katika Ukumbi wa Sheikh Idriss Abdulwakil Kikwajuni Mjini Zanzibar.
Alisema hakuna jambo zito na lenye Heshima kubwa miongoni mwa Jamii kama  Mtumishi wa Taasisi ya Umma au hata ile ya Binafsi anayeomba ajira, kufanya kazi na hatimae anastaafu katika misingi ya amani na upendo.
Waziri Aboud alisema kitendo cha kuwaaga wastaafu hao  ni ishara ya kuthamini Utumishi wao wa Kizalendo uliowajengea Heshima. Hivyo aliwashauri kuelewa kwamba maisha yao ya baadae yatakuwa salama wakiendelea kuamini uwepo wa Muumba wao anayendelea kuwapa riziki kwa njia nyengine ya kihalali.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwahakikishia Wastaafu hao wa Ofisi hiyo kwamba uzoefu na Utalaamu waliokuwa nao unaweza ukatumiwa pale utapohitajika na kuwaomba wasione taabu kuutoa kwa faida ya Kizazi Kipya.
 Mheshimiwa Aboud aliwakumbusha Watumishi wanaoendelea na majukumu yao wazingatie Uwajibikaji ulioshiba Upendo miongoni mwao na kuepuka majungu ili utekelezaji wa kazi zao uwe rahisi kuwafikia Wananchi.
Alifahamisha kwamba pale inapotokea hitilafu au migongano miongoni mwao hasa kwa Watendaji wa Kizazi Kipya  ni vyema busara zikatawala zaidi katika kuitafutia suluhu migongano au hitilafu hizo.
Mapema Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Nd. Abdulla Hassan Mitawi aliwaeleza Wastaafu hao kwamba Kustaafu ni tukio la Kisheria ambalo Mtumishi analazimika kulitekeleza wakati unapowadia licha ya kwamba baadhi yao wana nguvu na akili timamu.
Nd. Mitawi aliwashauri na kuwaomba Wastaafu hao wa Taasisi zilizo chini ya Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kuunda Jumuiya yao ya Wafanyakazi waliostaafu ili kujenga nguvu zitakazowezesha Ule Utaalamu walionao kutumiwa pale utapohitajika.
Alisema Ofisi hiyo itakuwa tayari kusaidia mazingira ya uundwaji wa Jumuiya hiyo kwa vile wengi kati ya Wastaafu hao bado wamejaaliwa kuwa na nguvu za kutosha, akili pamoja na uzoefu unaoweza kutumiwa katika baadhi ya Taasisi hizo.
Akitoa shukrani kwa niaba ya Wastaafu wenzake wa Taasisi zilizo chini ya Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Ndugu Mahfoudh Hamza Mlekwa alisisitiza umuhimu wa Watendaji kuzingatia Utiifu na uvumilivu utakaowawezesha kufanya kazi zao kwa ufanisi zaidi.
Nd. Mlekwa alisema Wafanyakazi wanaoendelea na Utumishi hasa wale wa Kizazi Kipya lazima wakubali kuwa na ustahamilivu katika kupambana na changamoto wanazokutana nazo vyenginevyo Utumishi wao unaweza kuwa na mashaka muda wote.
Jumla ya Wafanyakazi 24 wa Taasisi na Vitengo mbali mbali vya Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kutoka Ofisi Kuu Vuga, Pemba na Dar es salaam wamemaliza muda wao wa Utumishi kwa kutimiza Umri wa Miaka 60 iliyowekwa kwa mujibu wa Sheria na Kanuni za Utumishi Serikalini.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.